WIZARA YA NISHATI NA MADINI YAJIPANGA KUWAINUA WACHIMBAJI WADOGO
Wizara ya Nishati na Madini
imetenga jumla ya shilingi bilioni 8.9 kwa dhamira ya kuwainua wachimbaji
wadogo wa madini nchini ili kukuza kipato chao na hivyo kuboresha maisha yao.
Aidha, jitihada za kuwainua
wachimbaji wadogo zinalenga pia kuinua pato la taifa kutokana na kuongezeka
kiwango cha kodi na tozo mbalimbali zinazopaswa kulipwa na wachimbaji hao kwa
serikali.
Hayo yamesemwa na Waziri wa
Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo alipokuwa akizungumza na wajumbe
waliohudhuria mkutano mkuu wa mwaka wa wachimbaji wadogo wa madini nchini,
uliofanyika mjini Dodoma tarehe sita na saba mwezi huu.
“Tunayo dhamira ya dhati
kuwasaidia ili maisha yenu yaboreke na pia ili kukuza pato la taifa hili”,
alisisitiza Waziri Muhongo na kuongeza kuwa Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO) ndilo limepewa jukumu la kusimamia mipango ya uendelezaji wachimbaji
wadogo kwa kushirikiana na taasisi nyingine mbalimbali zinazohusika na sekta ya
madini.
Hata hivyo Profesa Muhongo
amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini kuhakikisha wanasajili biashara
zao, kuanisha mapato yao, pamoja na kulipa kodi na tozo mbalimbali zinazowahusu
ili taifa liweze kunufaika na rasilimali hiyo ya madini.
Alisisitiza kuwa wachimbaji watakaofuata
vigezo hivyo ndiyo tu watakaopata misaada ya aina mbalimbali ikiwemo mafunzo na
mikopo kutoka serikalini na wadau wengine wa maendeleo.
Kwa upande wao, wajumbe
waliohudhuria mkutano huo wa siku mbili, ambao ni viongozi na wawakilishi wa
vyama vya wachimbaji madini kutoka mikoa yote nchini, waliahidi kuyafanyia kazi
maagizo hayo ya Waziri kwa manufaa yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment