TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Saturday, March 30, 2013

UJUMBE WA LEO

WAPENDWA NAWATAKIWA PASAKA NJEMA KWA WATU WOTE MUNGU AWABARIKI NA AWALINDE KATIKA MAANDALIZI YA HII PASAKA.

PIA KWA WAKRISTO WOTE NAWATAKIA IBADA NJEMA YA PASAKA KWANI NI MUHIMU SANA KUSHIRIKI IBADA .

HATA HIVYO NAWAPA POLE FAMILIA ZOTE ZILIZOKUBWA NA MATUKIO MAKUBWA YA KUSHIKITISHA WAKATI WA MAANDALIZI YA KIPINDI HIKI, KAMA KUFIWA NA WAPENDWA WAO KATIKA JANGA LA KUANGUA KWA GHOROFA HUKO KARIAKOO , NA WENGINE WOTE WALIOFIWA NA WALE WALIOPATA MAJERAHA.

MUNGU AWAFARIJI WOTE.

MUUAJI WA PADRE MUSHI - ZANZIBAR AMEKAMATWA LEO


  Father Evalist Mushi enzi za uhai wake

Mtu anaesadikiwa kuwa ndie muuaji wa aliyekuwa Padre Evalist Mushi wa kanisa katoliki, visiwani zanzibar, amekamatwa leo alasili maeneo ya kariakoo, zanzibar.

Jeshi la polisi limethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, na kwenda nae kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.

Watu 40 wahofiwa kufukiwa baada ya jengo la ghorofa 16 kuporomoka Dar

 Watu zaidi ya 40 wanahofiwa kufukiwa na kifusi baada ya jengo la ghorofa 16 lililokuwa linajengwa kuporomoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam jana asubuhi.

Jengo lililoporomoka

Kuporomoka kwa ghorofa hilo lililokuwa katika Mtaa wa Indira Gandhi, kulizua huzuni, taharuki na simanzi kwa ndugu na jamaa waliofika kwenye eneo la tukio kutaka kufahamu nini kimetokea.

Shughuli mbalimbali katikati ya jiji hilo zilisimama kwa siku nzima baada ya jengo hilo kuanguka na kusababisha vifo vya watu watano, 13 kuokolewa huku zaidi ya watu 40 wakisadikiwa kufukiwa na kifusi cha udongo wa jengo hilo.

Jengo hilo lililokuwa likijengwa mkabala na Msikiti wa Shia Ithnasheri ulioko Barabara ya Indira Gandhi na Kampuni ya ‘Lucky Construction Limited’ lilianguka majira ya saa 2.30 asubuhi wakati ujenzi ukiendelea juu huku chini watoto wakicheza mpira na mama lishe wakiendelea na biashara zao kama kawaida.

Pamoja na vifo na wengine kujeruhiwa, magari takribani manne yalifunikwa na kifusi cha jengo hilo na kupondwa pondwa na kuwa kama chapati.

Katibu wa Msikiti wa huo wa Shia Ithnasheri, Mushtaq Damji alisema: “Leo tulikuwa na kitu kama jumuiya kwa jamii ya wahindu, tulipanga kusherehekea lakini yote yakafutika.

“Baada ya swala ya alfajiri, watu walikuwa wanazungumza hapa na pale na baada ya kupambazuka, watoto walikuwa wanacheza mpira, walikuwa 9. Sasa, bahati nzuri watoto saba wakakimbia na watoto wawili wakawa wamekwama,” alisema Damji.

Naye Mlinzi wa Msikiti huo, Athuman Nassor alisema: “Mimi nafanya kazi ya ulinzi hapa msikitini, lakini nilikuwa ninashangaa kiasi cha saruji kilichokuwa kikitumika kukorogea zege, kweli walikuwa wanazidisha mchanga.

“Niliwahi kuwaambia hata hawa vibarua, kuwa hii inayofanyika mbona siyo…,” alisema mlinzi huyo. Alisema; jana ilikuwa siku ya kumwaga zege ghorofa ya 16 na kulikuwa na vibarua wapatao 50 ambao kila mmoja alikuwa na ndoo yake tayari kuanza kazi kabla ya ghorofa hilo kuporomoka.

Mlinzi huyo alisema kuwa wakati tukio hilo linatokea alikuwa mbali kidogo na eneo la tukio na kusema kuwa bila shaka baadhi ya kinamama lishe ni miongoni mwa waliofukiwa.

Endelea kusoma Gazeti la Mwananchi

Tuesday, March 26, 2013

ALIYEMGONGA TRAFIKI ENEO LA BAMAGA NA KUFA HAPO HAPO AFIKISHWA MAHAKAMANI


Jackson  Simbo anayedaiwa kumgonga kwa gari marehemu trafiki Elikiza Nko wiki iliyopita maeneo ya Bamaga-Mwenge  jijini Dar ss Salaam amepandishwa kizimbani leo katika mahakama ya Wilaya ya Kinondoni. 

Mshitakiwa huyo ameachiwa kwa dhamana hadi kesi hiyo itakapo tajwa tena Aprili 15 mwaka huu
MWANAFUNZI WA UDSM AJINYONGA HADI KUFA

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka wa pili Kitivo cha Sheria, Joseph Bernadina (25), amejinyonga kwa kutumia kamba na kukutwa ameifunga juu ya mti, katika eneo la Yombo chuoni hapo.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Utawala, Profesa Yunus Mgaya, alithibitisha  kutokea kwa tukio hilo na kwamba alipata taarifa hizo jana asubuhi.

Aliongeza kuwa Jumamosi iliyopita alipokea simu kutoka kituo cha polisi cha chuo hicho akielezwa kuwa kuna mwanafunzi alitishia kujiua, lakini aliwahishwa hospitali na kupatiwa ushauri kutoka kitengo maalum cha washauri wa chuoni hapo na kuruhusiwa Jumapili.

“Nilikuja tena kushituka leo asubuhi napokea simu kutoka kwa mshauri wa wanafunzi kuwa kuna wanausalama wamemkuta mwanafunzi akiwa amejinyonga juu ya mti huku akiwa na karatasi kwenye mfuko wa sharti ikimtambulisha pamoja na ujumbe uliosema, kifo chake kisihusishwe na mtu yeyote kwani amejiua kwa ridhaa yake --asisumbuliwe mtu yeyote kwani nimefanya hivi kwa maamuzi yangu mwenyewe pia nizikwe kwetu--” alisema.

Profesa Mgaya alisema taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa na Uongozi wa chuo kwa kushirikiana na ndugu wa marehemu na kwamba Chuo kitagharamia kuusafirisha mwili kama alivyoomba katika ujumbe aliouacha wa kupelekwa wilayani Ludewa Mkoa wa Iringa.

Naye rafiki wa marehemu, Daniel Mwamlima, alisema marehemu hakuwahi kuzungumza chochote kilichoashiria kuwa ana matatizo wala mgogoro na mtu yeyote.  Alisema walimuacha hospitalini Jumamosi na kesho yake kumchukua, lakini  baadaye aliwatoroka.

“Sasa leo (jana) asubuhi tulipata taarifa za mwanafunzi kujinyonga mbaya zaidi tukakuta ni yeye,” alisema Mwamlima.

Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho (DARUSO), Yasini Athumani, alisema wamezipokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa tukio na alisema uchunguzi wa awali umebaini kwamba marehemu aliwahi kuwa na historia ya kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupata matibabu ya ugonjwa wa msongo wa mawazo.
WAIMBAJI WA MUZIKI WA INJILI SOLOMONI MUKUBWA NA NTABOBA WATUA DAR

 Mwimbaji wa nyimbo za injili, Solomon Mukubwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu maandalizi yake katika tamasha la Pasaka 2013.


Mwimbaji wa nyimbo za injili, Faraja Ntaboba akiimba kwa hisia moja ya nyimbo zake mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam .

Mwenyekiti wa Kamati Maalumu inayoratibu tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu maandalizi ya tamasha hilo.

DAR ES SALAAM, Tanzania

WAKATI muimbaji Sipho Makhabane wa Afrika Kusini akitarajiwa kutua Ijumaa, waimbaji wa nyimbo za injili kutoka Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wamewasili jana jijini Dar es Salaa, tayari kwa ajili ya kutumbuiza katika Tamasha la Pasaka, litakaloanza Machi 31 kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Kamati Maalumu inayoratibu tamasha hilo la kimataifa, Alex Msama aliwataja waimbaji waliowasili jana kuwa ni Solomoni Mukubwa (Kenya) na Faraja Ntaboba (DRC).

Msama aliwataka wapenzi, mashabiki na wadau wa muziki wa injili kujitokeza kwa wingi katika tamasha hilo, ambalo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ili kuunga mkono juhudi za kampuni yake kuandaa tamasha hilo kwa malengo mbalimbali ikiwemo kueneza injili ya Mungu na kusaidia makundi maalumu.

Kuhusu waimbaji, Msama alisema kuwa hadi kufikia Ijumaa, wakali wote wa nyimbo za injili kutoka nje watakuwa wamewasili jijini tayari kwa tukio hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Dar es Salaam na mikoa yote ambayo tamasha huilo litarindima.

Aidha, mkali wa aina hiyo ya muziki kutoka Kenya, Mukubwa, alisema kuwa amejiandaa vya kutosha katika tamasha la mwaka huu ambalo limebeba ujumbe wa Upendo na Amani.

“Wakati wa Uchaguzi wa Nchini Kenya tuliimba na kuhamasisha Amani na Upendo na kwa kupitia tamasha hili tutaimba nyimbo za kuhamasisha Amani na Upendo hapa Tanzania,” alisema Mukubwa. 

Naye mwimbaji kutoka DRC, Ntaboba alisema kuwa, watu wajitokeze kwa wingi katika tamasha hilo na kupata burudani itakayokwenda sambamba na mafundisho ya dini.

Msama aliongeza kuwa idadi ya waimbaji imeongezeka baada ya kujitokeza kwa nyota mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Ntutuma kutoka Kenya, ambapo baada ya tamasha hilo kutikisa kwenye jijini Dar es Salaam, itakuwa zamu ya Dodoma, Iringa, Mbeya, Mwanza kabla ya mashambulizi kuhimishwa mkoani Mara.
JK AKAGUA MIRADI YA UZALISHAJI JKT RUVU

8E9U3345
Rais Jakaya Kikwete akikagua mradi wa ufugaji kuku katika kambi ya Ruvu JKT jana (picha na Freddy Maro).
8E9U3392
Rais Jakaya Kikwete akikagua mradi wa ufugaji kuku katika kambi ya Ruvu JKT jana (picha na Freddy Maro).
JK AFUNGA RASMI MAFUNZOYA JKT YA MUDA MFUPI KWA WABUNGE RUVU JKT

8E9U3088Amiri Jeshi Mkuu,Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo ya muda mfupi kwa viongozi mbunge wa viti maalum Ester Bulaya leo katika kambi ya RUVU JKT.Rais Kikwete amefunga rasmi mafunzi hayo leo  yaliyofanyika kwa wiki tatu.(Picha na Freddy Maro)

8E9U3018
Wabunge Halima Mdee na Ester Bulaya pamoja na wenzao wakila kiapo wakati wa kuhitimu mafunzo ya muda mfupi yaliyofanyika katika kambi ya jeshi la Kujenga Taifa Ruvu JKT huko kibaha Mkoani Pwani leo
WANAFUNZI 10,000 WALIOKATA RUFAA YA KUFELI MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012, WAMEFELI TENA


Wakati tume ya kuchunguza matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012 ikiendelea na kazi, imebainika kuwa wanafunzi waliokata rufaa kutaka mitihani yao isahihishwe upya wamefeli zaidi baada ya
kusahihishiwa.Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambazo zimethibitishwa na baadhi ya maofisa, wanafunzi waliokata rufaa wamefeli zaidi na hata walioongezewa alama matokeo hayakubadilisha madaraja waliyopata awali.Habari zinaeleza kuwa, wanafunzi waliokata rufaa NECTA kutaka mitihani yao isahihishwe upya ni takribani 10,000 na kwamba baraza bado limetoa muda zaidi kwa wengine wanaotaka kukata rufaa.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya NECTA viliieleza NIPASHE kuwa mitihani kwa wanafunzi waliokata rufaa ilianza kusahihishwa Machi 12 na kuhitimishwa Machi 15, mwaka huu na kwamba wengi wamefeli zaidi.“Baada ya wanafunzi kadhaa kukata rufaa, NECTA iliamua kuwaita walimu waandamizi katika masomo yote na kuanza kufanya kazi ya kusahihisha mitihani hiyo upya kwa umakini, kilichowashangaza walimu hao ni kuona kiwango cha kufeli kimeongezeka,” alisema ofisa mmoja wa NECTA ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini kwa maelezo kuwa siyo msemaji wa baraza hilo.

Wakizungumza na NIPASHE, baadhi ya walimu walisema walioshiriki kusahihisha mitihani hiyo walisema kuwa maoni yaliyokuwa yanatolewa na baadhi ya watu kwamba matokeo mabaya ya mtihani huo yalitokana na uchakachuaji, hayakuwa ya kweli.Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Joyce Ndalichako, akizungumza na NIPASHE jana alithibitisha kuwa mitihani ya wanafunzi waliokata rufaa ilianza kusahihishwa Machi 12 mwaka huu.

Dk Ndalichako alisema hata hivyo, hana taarifa kama matokeo ya wanafunzi hao yanaonyesha kuwa wanafunzi wengi wamefeli zaidi kwa kuwa alikuwa safarini kikazi.“Unavyozungumza na mimi nipo Arusha na wageni, sifahamu kama baada ya kusahihishwa upya mtihani wa wanafunzi waliokata rufaa matokeo yamekuwaje, nitafahamu baada ya kurejea Dar es Salaam Jumatano wiki hii,” alisema Dk Ndalichako ambaye hata hivyo, hakutaja idadi ya wanafunzi waliokata rufani.Dk Ndalichako alisema suala la kufeli zaidi wanafunzi waliokata rufaa linawezekana kutokea kwa sababu kila mwaka imekuwa ikijitokeza hali kama hiyo, hivyo ni jambo la kawaida
NIPASHE
CGP JOHN MINJA ATETA NA WAKUU WA JESHI LA MAGEREZA BARANI AFRIKA, NCHINI ZAMBIA
CGP-MINJA b81f3
Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali, John Minja (waliokaa wa kwanza kulia) akiwa na wakuu wa jeshi hilo wa nchi mbalimbali barani Afrika (waliokaa) pamoja na maofisa wao (waliosimama) baada ya kufanya mkutano wa Taasisi za Urekebishaji Barani Afrika (ACSA). Wakuu hao wa taasisi hiyo walifanya mkutano wao katika Hoteli ya Sun iliyopo mjini Livingstone, nchini Zambia mwishoni mwa wiki, wakijadili masuala mbalimbali ya kuyaboresha majeshi yao. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Monday, March 25, 2013

WEMA SEPETU AFANYA KUFURU, BAADA YA KUMFANYIA MBWA WAKE SHOPPING YA MILLION 6, PIA AMEMTOA KAJALA JELA KWA SHILLING MILLION 13

KWA wale wenye hali ngumu kimaisha wataishia kusema; ni kufuru iliyoje kwani staa wa filamu za Kibongo, Wema Isaac Sepetu hivi karibuni amewafanyia mbwa wake wawili ‘shopping’ iliyogharimu dola 4,000 za Kimarekani (zaidi ya Sh. milioni 6.5 za madafu).
Sehemu ya shopping kwa mbwa wa Wema Sepetu.
Wema aliteketeza kiasi hicho cha fedha kwa kuwanunulia mbwa hao pafyumu, viatu na nguo, alivyoagiza kutoka nchini China, lengo likiwa ni kuhakikisha wanaishi katika mazingira mazuri.
Viatu kwa ajili ya mbwa wa Wema.
Akizungumzia ‘shopping’ hiyo nyumbani kwake Kijitonyama, jijini Dar, Wema alisema: “Kiukweli nawapenda sana hawa mbwa, ukinipasua roho yangu utawakuta ndiyo maana nataka wavae na kunukia vizuri, kinyume chake siwezi kuwa na amani.
Wema Sepetu.
“Najua watu wanaweza kushangazwa na kitendo cha mimi kutumia kiasi hicho cha fedha lakini sioni kama ni tatizo kwani ni kitu ambacho kinanipa furaha katika maisha yangu.”
 
Mmoja wa Mbwa wa Wema Sepetu.
Mbwa wa staa huyo aliowapa majina ya Van na Gucc wamekuwa ni gumzo kutokana na jinsi anavyowahudumia huku akiajiri watu maalumu wa kuhakikisha wanavaa, kula na kulala pazuri.


.
Mfuko wa pesa tasilim Sh. million 13 zilikwenda kuchukuliwa benki kwa ajili ya kumdhamini msanii mwenzao Kajala baada ya kuhukumiwa kwenda jela miaka 5 ama kulipa faini hiyo.
.
Wema akihojiwa na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo
.
Kajala akiwa huru baada ya kukamilishwa kwa taratibu zote
Mungu amzidishie Wema kwa kile alichokitoa katika kufanikisha msanii mwenzake kuwa huru, ni jambo kubwa alilolifanya na anahitaji pongezi ,Ikiwa tutakuwa na moyo kama huo wote basi kila mmoja duniani angeishi kama mfalme
JAMBAZI SUGU AUAWA KWA KUPIGWA RISASI MBEYA WAKATI AKIJIANDAA KUTEKA MAGARI


Mwili wa Jambazi sugu  Emanuel Blasius Mdendemi ukiwa umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa Mbeya



Baadhi ya polisi na waandishi wa habari wakiwa nje yajengo la kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa Mbeya

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika Mkutano alioufanya na waandishi wa Habari Ofisini kwake ambapo alisema tukio hilo lilitokea  jana majira ya Saa 10(kumi) Alfajiri

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani akionyesha baadhi ya siraha alizokutwanazo jamabazi huyo aliyeuwawa



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani akionyesaha hirizi iliyofungwa katika bunduki aliyokuwa anatumia jambazi huyo kama kinga katika matukio yake 

Hii ndiyo hirizi iliyofungwa katika bunduki aliyokuwa anatumia jamabazi huyo jamani waganga wakienyeji acheni hizo kuwadanganya watu matokeo yake ni kuongeza uhalifu nchini hakika nao tutawashughulikia kwani wamekuwa chanzo cha uhalifu nchini hayo yamesemwa na kamanda Diwani




Kamanda Diwani akiongea na waandishi wa habari

MTU mmoja ambaye anasadikiwa kuwa ni jambazi ameuawa kwa kupigwa risasi na Askari wa Jeshi la Polisi akiwa kwenye harakati za kuteka magari katika Eneo la Mlima Nyoka Jijini Mbeya baada ya kutokea kwa majibizano ya kurushiana risasi.
  
Jambazi huyo ni miongoni mwa watu waliokuwa wakitafutwa na Jeshi la Polisi Mkoani hapa akituhumiwa kuhusika na mauaji ya Askari Polisi mwenye namba G 68 PC Jafari yaliyotokea  Februari 6, Mwaka huu  katika eneo la Matundasi Wilayani Chunya.
  
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Diwani Athumani amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika Mkutano alioufanya na waandishi wa Habari Ofisini kwake ambapo alisema tukio hilo lilitokea  jana majira ya Saa 10(kumi) Alfajiri
  
Kamanda Diwani alisema kabla ya tukio majambazi wapatao wanne  tayari walikuwa wameweka mawe barabarani kwa nia ya kuteka magari ili wafanye uporaji katika eneo hilo la Mlima Nyoka ambalo limekuwa na matukio kadhaa ya watu kuporwa mali zao.
  
Alisema Jeshi la polisi baada ya kupata habari za kutegwa mawe, askari walifika kwa wakati kwa kuwa polisi walikuwa jirani na eneo hilo na kuweka mtego kwa kuwa majambazi hawakuwa wameonekana kwa wakati ule.
  
Aliongeza kuwa baada ya muda majambazi walipoona taa za gari walijitokeza tayari kushambulia lakini kabla ya hapo polisi walitoa amri ya kujisalimisha kinyume chake wakaanza kupiga risasi ovyo ndipo mashambulizi ya polisi yakafanywa.
  
Diwani alisema katika mapambano hayo alijeruhiwa jambazi mmoja kwa risasi kiunoni na ubavuni kulia na wengine watatu walifanikiwa kutoroka ambapo Marehemu alipowahishwa hospitali kwa matibabu daktari alibaini kuwa amekwisha fariki.
  
Alisema  jambazi huyo alikutwa na silaha moja SMG yenye namba  AB huku namba  nyingine zikiwa zimefutwa na magazine yake ikiwa na risasi ishirini na mbili (22) pamoja na mapanga mawili([2).
  
Aliongeza kuwa baada ya  Marehemu kufanyiwa upekuzi maungoni mwake jambazi huyo alikutwa na kitambulisho cha mkazi chenye namba B.0010453 chenye jina la Emanuel Blasius Mdendemi aliyezaliwa mwaka 1984 eneo la Matamba wilayani Makete Mkoa wa Iringa makazi yake ni Uwemba Mkoani Njombe.
  
“Jambazi huyu amebainika kuwa ni miongoni mwa majambazi waliokuwa kwenye mtandao wa majambazi uliokamatwa hivi karibuni kuhusiana na matukio waliyofanya Mikoa mbalimbali ikiwemo Mbeya,Njombe na Iringa.aidha amebainika kushiriki katika tukio la mauaji ya askari polisi PC Jafari wa kituo cha Mkwajuni – Chunya tarehe 06.02.2013.” Alisema Kamanda Diwani.
  
Aliongeza kuwa  ufuatiliaji wa majambazi waliotoroka unaendelea kufanywa ambapo pia  anatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za wahalifu hao azitoe bila kuchelewa kwa jeshi la polisi ili zifanyiwe kazi.

Pia  amewatahadhalisha majambazi na wahalifu wa makosa yeyote kuachana na uhalifu kwa kuwa ni biashara isiyo na faida badala yake wafanye shughuli halali kupata maendeleo ambazo fursa zake ni nyingi.

Picha na Mbeya yetu 
ISHA MASHAUZI NAYE AKIRI KUTUMIA MADAWA YA KULEVYA

STAA wa muziki wa taarab na mkurugenzi wa Mashauzi Classic, Aisha Ramadhan ‘Isha Mashauzi’ ameibua gumzo na kushangaza mashabiki baada ya kukiri kuwa yeye ni mtumiaji wa pombe kali na madawa ya kulevya aina ya mirungi

Ishu hiyo ilijiri Alhamisi ya wiki iliyopita wakati akihojiwa na mtangazaji wa Redio Times FM, Hadija Shaibu ‘Dida’ kupitia kipindi chake cha Mitikisiko ya Pwani ambapo alisema mirungi na pombe kali ndiyo starehe yake kwani inampa stimu kabla hajapanda jukwaani na katika maisha yake ya kawaida nje ya usanii.

Mashauzi alifunguka hayo baada ya Dida kumtaka atoe ufafanuzi juu ya skendo ya kuvuta bangi inayomkabili ambapo alisema siyo kweli kwamba anavuta bangi ila akakiri kuwa anakula sana mirungi na kugida ulabu. Aliongeza kwamba kwa kuwa hana mume, mtoto wala hataki kuwa na familia, mirungi na pombe ndiyo vitu vinavyompa furaha maishani mwake.
CHID BENZI AMTANDIKA MAKOFI NGWEA

Mkali wa vina na mashairi kutoka pande za Ilala anayefahamika kwa jina maarufu la 'Chid Benz' ameanza kupata sifa mbaya baada ya kumpiga mwanamuziki mwenzake 'Ngwea' nje ya ukumbi wa  Ambassador Lounge ulioko kwenye jengo la Benjamini Mkapa tower Posta usiku wa kuamkia Machi 22.

Kupigwa kwa 'Ngwea' kulikuja baada ya 'Chid' kumzingua 'Dully' alipokua akiingia ambapo mwisho wake aliamua kuondoka.
 
 Alipoondoka 'Dully', 'Ngwea' akamuuliza inakuaje unamzingua kubwa lao, ndipo 'Chid' alipopaniki na kuanza kutoa lugha chafu huku akitaka kutokumsikiliza 'Ngwea', inasemekana 'Ngwea' aliamua kukaa kimya lakini 'Chid' aliendelea kungea kwa hasira na kusema "ndio nimemzingua kwani yeye nani" na kumbadilikia 'Ngwea'.
 
'Ngwea' aliamua kuondoka kwenye ukumbi huo lakini alipofika chini ya ghorofa ndipo 'Chid' alipomfuata na kuanza kumshambulia mwanamuziki mwenzake huyo na baadaye kumjeruhi kwa chupa mkononi. 

Lakini baada ya hapo 'Ngwea' aliweza kufika hospitali na kuweza kupatiwa matibabu ya jeraha hilo la chupa.
RAIS WA CHINA X I JINPING AWASILI NCHINI KWA ZIARA YA SIKU MBILI
 Rais wa China, Mhe. Xi Jinping na mke wake wakiteremka kwenye ndege mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam jana kwa Ziara ya Kitaifa ya siku mbili hapa nchini.
 Mhe. Rais Xi Jinping akikagua Gwaride maalum lililoandaliwa kwa heshima yake.
 Mhe. Rais  Xi Jinping na mwenyeji wake Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwasalimia baadhi ya kina mama wa Dar es Salaam waliofika Uwanjani hapo kwa ajili ya mapokezi.
 Mhe. Rais Xi Jinping na Mhe. Rais Kikwete wakiwa katika Jukwaa maalum wakati nyimbo za mataifa yao zilipokuwa zikipigwa sambamba na mizinga 21 kwa heshima ya Mhe. Rais Xi Jinping.
 Mhe. Rais Xi Jinping na mwenyeji wake Mhe. Rais Kikwete kwa pamoja na wake zao wakifurahia burudani iliyokuwa ikitolewa  na moja ya vikundi vya burudani vilivyokuwa uwanjani hapo mara baada ya Rais Xi Jinping kuwasili nchini.
Mhe. Rais Xi Jinping na Mhe. Rais Kikwete wakiondoka uwanjani hapo mara baada ya mapokezi.
(Picha Zote na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa)
KAJALA AHUKUMIWA MIAKA MITANO JELA AMA KUTOA FAINI YA MILLIONI 13
 
Msanii Kajala Masanja.

Leo imesomwa hukumu ya kesi iliyokuwa inamkabili mcheza filamu za Kitanzania anayefahamika kwa jina la 'Kajala Masanja' na mumewe mbele ya Hakimu 'Sundi Fimbo' kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es salaam.
 
 Katika hukumu hiyo 'Kajala amehukumiwa kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya shilingi milioni 13 na mumewe kwenda jela miaka saba au kulipa faini ya shilingi milioni 200. 
 
Kajala alikuwa anakabiliwa na kesi ya kuuza nyumba iliyowekwa kizuizini na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) baada ya mumewe 'Faraji Agustino' kukumbwa na makosa ya kutakatisha fedha haramu.

Hata hivyo baada ya hukumu hiyo kutolea mahakamani hapa, mwanadada mwenye michejo mingi hapa Bongo anayefahamika kwa jina la Wema Sepetu' aliweza kujitolea yeye mwenyewe kiasi cha Tsh. milioni 13 kutoka mfukoni mwake kwa ajili ya kumlipia msanii mwenzake wa filamu 'Kajala' asiweze kutumikia adhabu ya kifungo hicho cha miaka 5 jela.

 
 Hii ni mara ya pili kwa msanii 'Wema Sepetu' kujitolea kiasi kikubwa cha fedha kusaidia msanii mwenzake.!

LIVE MATCH CENTRE: TANZANIA 3 - 1 MOROCCO


Dk 90+4 FULL TIME! TAIFA STARS 3-1 MOROCCO
Dk 90+3 Morocco inapata bao. TAIFA STARS 3-1 MOROCCO
Dk 90 Taifa Stars imefanya mabadiliko, ametoka Samatta ameingia John Bocco.
Dk 87 Ulimwengu anaumia baada ya kuangushwa na beki wa Morocco. Anatibiwa na kurudi uwanjani.
Dak 86: Taifa Stars 3-0 Morocco
Dk 80 RED CARD..! Achchakir Abderrahm wa Morocco anaonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumtolea lugha chafu mwamuzi Helder Martins wa Angola.
Mbwana Samatta anaiandikia Tanzania bao la 3.
Dk 68 Morocco inafanya mabadiliko, ametoka Barrada Abdelaziz ameingia El Bahri Brahim.
Dk 67 GOOO....! Samatta anaifungia Taifa Stars bao la pili akimalizia mpira aliopenyezewa kutoka katikati ya uwanja baada mbio mabeki wa Morocco.
Dk 65 Yondani anavuruga vizuri mpira wa Eladoua Issam wa Morocco aliyekuwa anaenda kufunga.
Dak 63: Athuman Iddi anaingia kuchukua nafasi ya Mrisho Ngassa
Dk 61 Ngassa anachelewa kuunga krosi safi ya Samatta.
Dk 50 Taifa Stars inalishambulia zaidi lango la Morocco, uwepo wa Ulimwengu umeongeza kasi ya ushambuliaji ya Taifa Stars.
Dk 45 GOOO....! Thomas Ulimwengu anaifungia Taifa Stars bao la kwanza baada ya kuuwahi mpira ulioshindwa kuokolewa na mabeki wa Morocco na kufunga. TAIFA STARS 1-0 MOROCCO
Dk 45 Taifa Stars inafanya mabadiliko, ametoka Mwinyi Kazimoto ameingia Thomas Ulimwengu.
Dk 45 KIPINDI CHA PILI KIMEANZA!
Dk 45 HALF TIME! TAIFA STARS 0-0 MOROCCO.
Dk 45 Barrada Abdelaziz anaonyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea vibaya Samatta.
Dk 41 Beki wa Taifa Stars, Kelvin Yondan amejitahidi kuharibu mipira mingi ya adui.
Dk 41 Beki wa Taifa Stars, Kelvin Yondan amejitahidi kuharibu mipira mingi ya adui.
Dk 38 Eladoua Issam wa Morocco anapiga kichwa chepesi kinachotoka nje kidogo ya lango la Taifa Stars.
Dak 35: Starz 0 - 0 Morocco
Dk 33 Beki wa Taifa Stars, Shomari Kapombe anaichambua ngome ya Morocco na kupiga shuti kali linalotoka nje ya lango.
Dk 31 Kaseja anadaka shuti kali la Achchakir Abderrahm.
Dk 25 Straika wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anakosa bao la kichwa akiunga krosi ya Mrisho Ngassa.
Dk 24 Kipa wa Taifa Stars, Juma Kaseja anaokoa shuti kali lililoelekezwa langoni kwake.
Dk 18 Kiungo wa Taifa Stars, Salum Aboubakar 'Sure Boy' anapiga shuti kali kuelekea lango la Morocco lakini kipa Lamyaghri Nadir anaudaka mpira.
Dk 14 Beki wa Taifa Stars, Aggrey Morris anaukosa mpira kwa kichwa kuelekea lango la Morocco baada ya Taifa Stars kupata kona.
Dakika ya 9 timu zinashambuliana sana huku zikisomana.

Mpira umeanza hapanuwanja wa taifa.

Kikosi cha Taifa Stars kitakachoanza dhidi ya Morocco:1.Juma Kaseja2.Erasto Nyoni3.Shomari Kapombe4. Aggrey Morris5. Kelvin Yondani6. Frank Domayo7. Mrisho Ngasa8. Sureboy9. Mbwana Samatta10. Amri Kiemba11. Mwinyi Kazimoto

KAULI YA RAIS KIKWETE KUHUSU UCHAWI KWENYE SOKA LA BONGO


Moja kati ya kauli ambazo zimeingia kwenye headlines za michezo kwa wiki iliyokwisha ni kauli ya President Jakaya Kikwete, kauli kuhusu ushirikina kwenye soka la bongo aliyoitoa wakati akizindua uwanja mpya wa club ya soka ya Azam Chamazi Dar es salaam.
 Namkariri akisema “najua mtapata tabu sana mkiwaleta hapa watasema kiwanja hiki kina namna, yote ni ushirikina tu…. ni wale ambao hawataki kuwekeza kwenye maendeleo ya mchezo, wanataka kuwekeza kwenye mambo ya kipuuzi… we tangu lini uchawi ukacheza mpira? ingekua uchawi unacheza mpira Afrika ingekua ina kombe la dunia na hatunyang’anywi, nyie hamjajua kwamba jambo hili la kipuuzi? mnawekeza pesa nyingi kwenye kamati ya ufundi hakuna chochote, haiwafikishi kokote”
 
Rais aliongeza  kwa  kusema “wekeza kwa kocha mzuri, vifaa vizuri, mafunzo mazuri, wachezaji walale mahali pazuri, Uwanja wa Azam Complex ni mzuri na wa kisasa, kuna sehemu ya mazoezi, vijana wanalala sehemu nzuri… ndio maana naamini nyinyi hakuna sababu ya kutofanikiwa"
JACK CHUZI WA BONGO MOVIE ABADILI DINI NA KUOLEWA


  Katika Hali ya Kushtusha na Kufuraisha....Staa wa Bongo Movie Jack Pentezel amewashtusha wengi baada ya Kuamua kubadili dini kuwa Muislamu kisha kuolewa na Mpenzi wake wa Muda Gadner Dibibi...
 

Sunday, March 24, 2013

RIPOTI YA POLISI KUHUSU MADAI YA KULAWITIWA WANAFUNZI WA IFM SI YA KWELI

Kamati iliyoundwa kuchunguza vitendo vya udhalilishaji na kuporwa vitu vyao  wanavyofanyiwa wanafunzi  wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), wanaoishi  katika hosteli zilizopo Kigamboni Manispaa ya Temeke imebaini hakuna wanafunzi waliofanyiwa vitendo hivyo.
 
Kamati hiyo iliyoundwa na Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Polisi jijini Dar es Salaam, Suleiman Kova baada ya kuwahutubia wanafunzi hao katika Viwanja vya Machava, ilijumuisha wanafunzi wanne wa IFM na wakuu wa upelelezi kutoka kanda hiyo .
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Englebert Kiondo, alisema kamati hiyo ilichunguza kwa kina madai hayo ya wanafunzi, lakini hakuna na hata moja walilobaini kuwa na ukweli .
Alisema suala la ulawiti walilodai wanafunzi, walijaribu kufuatilia kwa ukaribu  kutumia dawati la jinsia  ikiwamo kuwauliza wanafunzi hao ni nani alifanyiwa kitendo hicho, lakini hamna hata mmoja aliyejitokeza kusema amefanyiwa.
“Tuliwauliza wanafunzi ni nani amefanyiwa kitendo kama hiki ili tujue cha kufanya, lakini hakuna aliyejitokeza kukiri kuwa alilawitiwa tofauti na walivyodai hivyo wakati wa maandamano ,” alisema Kamanda Kiondo.
MWENDESHA PIKIPIKI AUAWA KWA KUPIGWA RISASI NA POLISI

Ruvuma, Wananchi wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wamemwua askari mmoja na kumjeruhi mwingine kwa kutumia mawe, baada ya askari hao waliokuwa doria, kumwua kwa kumpiga risasi mwendesha pikipiki (bodaboda).
Askari Polisi, PC Yohana namba 7771 alipoteza uhai katika eneo la Ngwinde kutokana na waendesha pikipiki hao kushikwa na hasira za kuuawa kwa mwenzao aliyetambulika kwa jina la Makisio Ngonyani (27), mkazi wa kijiji hicho, na hivyo kuamua kupiza kisasi.
Akizungumza na kipindi cha Radio One Stereo Nipashe, Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Deusdedith Nsimeki amethibitisha kutokea kwa tukio hilo jana majira ya saa 8 mchana na kusema kuwa askari polisi wakiwa katika sare zao, walikuwa wamemfuatilia mwendesha pikipiki aliyekuwa amevunja sheria kwa kubeba abiria wawili na aliposimamishwa alikaidi.
 
 Baada ya kumkamata ndipo iliyopotokea purukushani ambapo risasi iliyofyatuliwa na askari ilimjeruhi mtu mmoja kidoleni kabla ya kumpata marehemu kwenye paji la uso, na kusababisha kifo chake papo.
Kamanda Nsimeki amesema, baada ya kuona hivyo, wananchi walichukua miti mikavu na mawe na kuanza kumshambulia PC Yohana na kusababisha kifo chake.
Askari aliyejeruhiwa, Konstebo Venance Kamugisha yupo katika hospitali ya Songea Mjini, kwa matibabu ya majeraha aliyoyapata kichwani na kusababisha kupoteza damu (bleeding excessively).
Kamanda Nsimeki amesema jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi ili kupata ripoti kamili.
WAKILI MAWALA NYANGA AJIUA KWA KUJITUPA TOKA JUU YA GHOROFA

Imenukuliwa kutoka kwenye gazeti la Mwananchi, ARUSHA-- Giza limeukumba Mkoa wa Arusha baada ya kutokea vifo vya ghafla vya watu maarufu. Jana Wakili Nyaga Mawalla alifariki baada ya kujirusha kutoka ghorofani akiwa jijini Nairobi, Kenya alikokwenda kwa matibabu.

Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa Nyaga alikufa baada ya kujirusha kutoka katika jengo la ghorofa ya hospitali aliyokuwa akitibiwa jijini Nairobi usiku wa kuamkia jana.

Mfanyakazi wa Kampuni ya Mawalla Advocate, John Minja aliliambia gazeti hili kuwa mwili wa marehemu ulitarajiwa kurejeshwa nchini jana.

“Hali yake haikuwa mbaya, kwani juzi mchana tulizungumza naye tukitaka kwenda kumsalimia lakini, alitueleza kuwa angerejea jana nchini,”alisema Minja.

Hata hivyo, bado haijajulikana sababu za kujiua, lakini baadhi ya ndugu zake wanasema ni kutokana na msongo wa mawazo.

Taarifa za kifo cha Mawalla anayemiliki kampuni kadhaa ikiwamo Kampuni ya uwakili ya Mawalla Advocates, kimeshtua wengi akiwamo Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliyesema taifa limepoteza kijana mwenye maono, akili na mjasiriamali aliyetajirika bila kuiba.

“Nimepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Nyaga. Licha ya udogo wake kiumri, lakini alikuwa mshauri wangu kwenye mambo mengi kiuchumi, kibiashara na kijamii. Nyaga alikuwa kiongozi wa jamii asiye na mipaka katika huduma tofauti na wafanyabiashara wengi nchini walishirikiana naye,” alisema Mbowe.

Mawalla ambaye ni mtoto wa wakili wa kwanza wa kujitegemea nchini, Juma Mawalla alikuwa jijini Nairobi kwa matibabu ya kupungaza sumu mwilini kutokana na madhara ya matumizi ya dawa za shinikizo la damu kwa muda mrefu.

Wakati kifo hicho cha ghafla cha Mawalla kikitokea, Jiji la Arusha pia linaomboleza kifo kingine cha ghafla cha mfanyabiashara maarufu wa madini, Henry Nyiti kilichotokea mkoani Morogoro.

Nyiti ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Interstate yenye makao yake makuu eneo la Tengeru, wilayani Arumeru alifariki usiku wa kuamkia juzi akiwa Mahenge alikokwenda kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini na anatarajiwa kuzikwa nyumbani kwake eneo la Akheri, Arumeru keshokutwa Jumanne.

Akimzungumzia wakili Mawalla, Mbowe alisema mchango wake kwa maendeleo ya jamii hautasahaulika hasa kutokana na kujitolea kuendeleza taaluma ya uwakili kwa kudhamini tuzo ya wakili kijana kwa kutoa dola 5,000 kila mwaka kumsomesha mshindi wa tuzo hiyo.

Mbowe ambaye mwezi uliopita alipokea hati ya kiwanja chenye thamani ya Sh500 milioni iliyotolewa kwa Taasisi ya Maendeleo Arusha (ArDF) na wakili huyo kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto, alipendekeza hospitali hiyo iitwe Nyaga Mawalla Memorial Hospital kama njia ya kumuenzi.

Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema ambaye ndiye mwanzilishi wa taasisi ya ArDF, alimwelezea Mawalla kama kiongozi, tajiri na kijana aliyetumia akili, nguvu na rasilimali zake akishirikiana na viongozi wote bila kujali tofauti zao kiitikadi.

“ArDF tutauenzi na kuuthamini utu uliouonyesha Mawalla kwa kukamilisha ndoto ya kuwa na hospitali ya kisasa ya mama na watoto ili kuokoa maisha ya kundi hilo linapoteza maisha kwa kukosa huduma bora na sahihi,” alisema Lema.

Fred Lowassa, mtoto wa Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa alimwelezea wakili Mawalla kama kijana aliyeonyesha nidhamu tangu akiwa shule na aliendelea nayo hadi kwenye kazi na shughuli za kiuchumi kiasi cha kufanikiwa na kutumia utajiri wake kusaidia jamii. “Kifo hiki ni pigo siyo tu kwa Arusha bali taifa zima la Tanzania.”

Mchango wa Mawalla kwenye kuendeleza sekta ya elimu, hasa sheria umetukuka ndiyo maana alijitolea hata kufundisha bila malipo kwenye vyuo vikuu kadhaa nchini,” alisema Lowassa.

Pamoja na kujitolea kwenye shughuli mbalimbali za kimaendeleo, Mawalla pia alikuwa mfadhili wa watoto kadhaa wenye mahitaji maalumu ambapo hadi mauti yanamkuta, alikuwa akisomesha wanafunzi kadhaa katika ngazi mbalimbali kuanzia elimu ya msingi hadi chuo kikuu.

Nyumbani kwake anaishi na zaidi ya watoto saba ambao amewachukua kutoka sehemu na familia mbalimbali nchini anaowalea, kuwahudumia na kuwasomesha kama watoto wake wa kuwazaa.

Ingawa haikuweza kujulikana haraka kutokana watu walio karibu naye wote kudaiwa kuwa jijini Nairobi, mwili wa wakili huyo unatarajiwa kuletwa nchini kati ya leo na kesho na kupelekwa moja kwa moja katika chumba cha kuhifadhi maiti cha KCMC, mjini Moshi kusubiri maziko yanayotarajiwa kufanyika nyumbani kwao Marangu.