TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Thursday, May 21, 2015

JK afungua rasmi mkutano wa siku mbili wa Open Government Partnership (OGP) 

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akifungua rasmi mkutano wa siku mbili wa Open Government Partnership (OGP) katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Mei 20, 2015.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akielezea jambo wakati akifungua rasmi mkutano wa siku mbili wa Open Government Partnership (OGP) katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Mei 20, 2015.
Mkurudenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza Bw. Brian Eyakuze akimkaribisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete kupokea tuzo maalumu ya taasisi zisizo za kiserikali kwake kwa kuwa kiongozi aliyetekeleza kwa vitendo masuala ya Serikali ya Uwazi na Ushirikiano. Hii ni wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa Open Government Partnership (OGP) katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Mei 20, 2015.
Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Twaweza Bw. Brian Eyakuze akimkabidhi Rais Jakaya Mrisho Kikwete tuzo maalumu ya Asasi za Kijamii kwake kwa kuwa kiongozi aliyetekeleza kwa vitendo masuala ya Serikali ya Uwazi na Ushirikiano. Hii ni wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili wa Open Government Partnership (OGP) katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam leo Mei 20, 2015.(Muro)

TUME ya haki za binadamu yatoa taarifa ya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Jeshi la Polisi 

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Mhe. Bahame Nyanduga akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Jeshi la Polisi za kuwapiga na kuwazalilisha Viongozi na Wafuasi wa CUF huko Mtoni Mtongani Temeke, Dar es sa Salaam.Picha na Eliphace Marwa-MAELEZO
---
Na PIUS YALULA - MAELEZO
TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imelaani vitendo vya uzalilishaji vilivyofanywa kwa Viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) Januari 27 mwaka huu (2015) wakati wa maandamano ya Chama hicho Mtoni Mtongani Wilaya ya Temeke.
Akizungumza na waandishi wa habari leo (Mei 20, 2015) Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame Nanduga, alisema uchunguzi wa tukio hilo umekamilika kwa kuzingatia kifungu cha 130[1][c],[f] na [g] cha katiba ya jamhuri ya Aidha aliongeza kuwa sheria nyingine zilizotumika kuchunguza tukio hilo ni pamoja na kifungu cha 6[1][c]na [g] vifungu 15[1][a] na 28[1][a],[b] na f vya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na.7 ya mwaka 2001, sheria ya polisi na polisi wasaidizi, sura 322, na sheria ya vyama vya siasa, sura 258.
Nyanduga alisema Tume yake imebaini ukikwaji mkubwa wa haki za binadamu waliofanyiwa viongozi na wanachama chama cha wananchi CUF katika maandamano yao ya shughuli za kichama, hivyo Tume ilibaini kuwa jeshi la polisi lilitumia nguvu kupita kiasi, ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na udhalilishaji wa wanachama wawili wa kike wa CUF.
"Tume imetoa mapendekezo kwa jeshi la polisi kuzingatia kanuni, sheria, haki za binadamu na misingi ya utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku na kuhakikisha maafisa wake wanajipanga vyema katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa operesheni zake" alisema Nyanduga
Kwa mujibu wa Nyanduga tume hiyo pia imewataka Viongozi na wanachama wa CUF kutafuta namna ya kuboresha mahusiano na jeshi la polisi, ili kuondoa mivutano isiyo na tija.Tume imepanga kuitisha mafunzo na mikutano mbalimbali kwa kushirikiana na vyama vya siasa,Tume ya Taifa ya Uchaguzi [NEC], pamoja na vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwemo Jeshi la Polisi na Magereza, msajili wa vyama vya siasa, na asasi za kiraia ili kupanga taratibu zote katika kujua haki za binadamu na utawala bora.(Muro)

ATHARI ZA MAFURIKO
WAZIRI WA MIFUGO WAKIWA KWENYE SEMINA NA WATENDAJI WAKE


Wednesday, May 20, 2015

Ripoti ya CAG yaanika madudu 

Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad
RIPOTI ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, imetolewa na kuwasilishwa bungeni jana huku ikiendelea kuibua madudu katika matumizi ya fedha.
Moja ya madudu hayo yamebainika katika usimamizi wa rasilimali watu katika balozi za Tanzania, ambapo watumishi waliokoma kutumikia Taifa, wameendelea kugharimiwa katika maisha yao katika nchi hizo.
Moja ya gharama iliyotajwa na Profesa Assad wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Bunge ni Sh milioni 543 zilizotumika kulipa posho ya pango kwa watumishi hao baada ya kustaafu.
Katika Ripoti ya Ukaguzi ya Serikali Kuu, Profesa Assad alikwenda ndani zaidi na kutaja orodha ya balozi hizo ambazo watumishi wake wameendelea kulipwa ingawa wamestaafu, kwa madai kuwa hakukuwa na fedha za kugharimia urudishwaji wao nyumbani.
"Maofisa hawa wastaafu, walibakia wakifanya kazi bila kuwa na mikataba kwa kuwa Serikali ilikuwa na uhaba wa fedha, kwa ajili ya kulipia gharama ya kuwarudisha nyumbani baada ya kufikia umri wa kustaafu," ameeleza Profesa Assad katika ripoti yake.
*Balozi zenyewe
Ubalozi wa kwanza kuwa na maofisa wa aina hiyo ni wa Kinshasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambapo mtumishi alistaafu tangu Machi 28, 2014 na akalipwa posho ya Sh milioni 130.8, kutokana na kufanya kazi kwa miezi 10 zaidi.
Katika ubalozi huo huo, Profesa Assad alisema mtumishi huyo huyo alipewa Sh milioni 41.2 ya kodi ya pango kwa miezi kumi aliyofanya kazi akiwa amestaafu na hana mkataba na Serikali.
Ubalozi mwingine ni wa Maputo nchini Msumbiji, ambapo mtu alilipwa posho ya kufanya kazi akiwa amestaafu ya Sh milioni 204 kwa miezi 19 zaidi baada ya kustaafu.
"Kiwango hiki cha posho ni sawa na mara tatu ya gharama ya kumsafirisha yeye, mizigo na familia yake," ameeleza Profesa Assad katika taarifa hiyo.
Katika Ubalozi wa Ottawa nchini Canada, Profesa Assad alibainisha wazi kuwa ndiko angalau kulikokuwa na mstaafu ambaye alipewa mkataba wa miaka miwili, ingawa hakukuwa na maelezo ya sababu ya kuongezewa mkataba.
Mstaafu huyo wa Canada yeye alilipwa Sh milioni 137.5, huku katika Ubalozi wa Washington Marekani, mtumishi aliyefanya kazi ya miezi mitatu tu zaidi baada ya kustaafu, akiibuka na kitita cha Sh milioni 30.
Vyama vya siasa Wakati wanasiasa wakiwa vinara wa kushutumu watumishi wa Serikali na hata viongozi wengine kwa matumizi mabaya ya fedha za Serikali, Profesa Assad amebainisha kuwa vyama vinavyoongoza kwa kupokea ruzuku kubwa kutoka serikalini, baada ya ukaguzi vimepata hati yenye mashaka.
Vyama hivyo ni CCM, Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi huku chama kimojawapo kilichojiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) cha NLD, kikiwa miongoni mwa vyama sita vilivyopata hati mbaya.
Akielezea sababu ya kutoa hati hizo kwa vyama hivyo, Profesa Assad alisema alibaini kuwa taarifa ya hesabu za vyama hivyo, zinatofautiana na misingi ya uhasibu na mfumo wa uandaaji wa taarifa za fedha.
Vyama vingine maarufu ambavyo hata havikupeleka taarifa zao za fedha kwa ajili ya kukaguliwa na CAG, ni pamoja na UDP na DP, huku chama cha ADC kinachotarajia kusimamisha mgombea urais Zanzibar, kikipata hati mbaya.
"Nashauri Msajili ya Vyama vya Siasa kwa kushirikiana na Mhasibu Mkuu wa Serikali, kuandaa mwongozo mzuri wa namna ya kuandaa taarifa za hesabu. Hii itawezesha kutoa taarifa za fedha kwa ubora unaotarajiwa," alieleza Profesa Assad.
Watumishi hewa Profesa Assad ameendelea kubainisha kuwa ndani ya Serikali kumeendelea kutolewa mishahara hewa, inayolipwa kwa watumishi waliostaafu, walioacha kazi na waliofukuzwa kazi.
"Nimebaini kuwepo kwa malipo ya shilingi milioni 141 katika taasisi saba...ambao hawakugundulika na kuondolewa katika orodha ya mishahara kwa wakati baada ya muda wao wa utumishi kufikia ukomo kinyume cha Sheria ya Umma kwa Wastaafu," amesema.
Malipo hayo yalikutwa katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Sh milioni 74, Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga Sh milioni 24, Ofisi ya Waziri Mkuu Sh milioni 13 na Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro Sh milioni 10.
Mishahara mingine hewa imekutwa katika Sekretarieti ya Mkoa wa Tanga Sh milioni 10, Idara ya Huduma za Uhamiaji Sh milioni 6 na Wizara ya Mambo ya Ndani Sh milioni 1.9.CHANZO:HABARI LEO (Muro)

Zaidi ya 6,000 wagoma UDSM 

Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala (katikati) akizungumzia moja ya migomo ya wanafunzi wa chuo hicho.
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala (katikati) akizungumzia moja ya migomo ya wanafunzi wa chuo hicho.
ZAIDI ya wanafunzi 6,000 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sehemu ya Mlimani, wanaodai fedha za kujikimu kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini (HESLB), jana waligoma kuingia darasani wakishinikiza kulipwa fedha zao.
Kwa ujumla, wanafunzi hao wanaosomea fani mbalimbali, wanadai zaidi ya Sh bilioni 2.8. Makamu Mkuu wa chuo hicho kikongwe zaidi nchini na maarufu barani Afrika, Profesa Rwekaza Mukandala alikiri kuwepo kwa mgomo huo.
Alithibitisha kuwa wanafunzi wawili walijeruhiwa na kulazwa katika zahanati ya chuo hicho, kutokana na vurugu za hapa na pale.
Alisema kutokana na vurugu hizo, kumetokea uharibifu katika hosteli za chuo hicho, ikiwemo ya Mabibo kutokana na wanafunzi hao kugoma kuhudhuria masomo, badala yake wakaanza kufanya uharibifu.
Aliongeza kuwa wanafunzi wanaokaa katika hosteli ya Mabibo, walifanya uharibifu asubuhi na uongozi umefanya ufuatiliaji na kubaini kuwa baadhi yao hawakuingia darasani, na badala yake kujikusanya katika vikundi na wengine wakijikusanya katika bwalo la chakula chuoni hapo.
"Wanafunzi walikuwa wanategemea malipo kuanzia wiki iliyopita. Ilipoanza jana (juzi) wakaleta malalamiko yao tukafanya jitihada nyingi, tukaamua chuo kitawasaidia fedha kidogo mpaka watakapopata," alisema.
Aliongeza kuwa kufikia jana Hazina (Wizara ya Fedha) waliuhakikishia uongozi wa chuo hicho fedha hizo zingelipwa kufikia jana jioni.
Katika maeneo ya chuo, askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kutoka Jeshi la Polisi walifurika kwa lengo la kuchukua tahadhari za kiusalama chuoni hapo.
Waziri wa Mikopo katika Serikali ya Wanafunzi chuoni hapo, Shitindi Venance alisema fedha za kujikimu wamekuwa wakipatiwa kila baada ya wiki nane, sawa na miezi miwili, lakini hadi sasa wamevumilia na kuchoka.
Kila mwanafunzi anastahili kulipwa Sh 450,000. Mbali na fedha za kujikimu, pia alisema zipo dalili za kucheleweshewa ama kutopatiwa fedha za mafunzo kwa vitendo kwa kuwa muda wa kupewa fedha hiyo umekaribia huku dalili zikiwa hazionekani.
Wanafunzi hao waligoma jana kuingia madarasani huku wengi wao wakibaki wakiwa wamejikusanya vikundi katika eneo la karibu na bwalo la kulia chakula huku wakiimba njaa inawasumbua.
Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisoba alikiri kuwapo kwa tatizo hilo. Aliwataka walioathirika na ucheleweshaji huo, kuwa na subira kwa kuwa taratibu za kuwalipa, zilikuwa zinafanywa.CHANZO:HABARI LEO (Muro)

 

Poroshenko amnyooshea kidole Putin

Rais wa Ukraine, Petro Poroshenko
Vladimir Putin
Rais wa Ukraine Petro Poroshenko ameiambia BBC kuwa hamuamini kiongozi wa Urusi Vladimir Putin katika harakati za kuleta Amani Mashariki mwa Ukraine.
Poroshenko anasema anahofia kwamba huenda kukawa na kutoku elewana kati ya mataifa hayo mawili.
Hata hivyo ameielezea hali hiyo kuwa ni vita kamili kati ya nchi hizo. Ameongeza kuwa awali katibu mkuu wa Marekani John Kerry alifanya mazungumzo na kiongozi huyo kabla ya mazungumzo yao na Rais wa Urusi Putin.CHANZO:BBC (Muro)

Wahamiaji kujadiliwa,Malaysia 

Wahamiaji huko Indonesia
Mawaziri wa mambo ya nje wa Thailand,Malaysia na Indonesia wanafanya mkutano wa dharula mjini Kuala Lumpur kujadili tatizo la wahamiaji haramu katika ukanda wao.
Nchi hizo tatu zinakabiliwa na shinikizo la kimataifa kuwasaidia maelfu ya wahamiaji waliokwama Baharini ambao wanahitaji chakula na maji.
Wahamiaji wengi ni waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbia Myanmar, lakini Serikali ya nchi hiyo imekataa kuhudhuria mkutano huo.
Wavuvi nchini Indonesia wamewaokoa zaidi ya wahamiaji 100 siku ya jumatano
Bado kuna hofu kuhusu usalama wa waliokwama baharini.Maelfu ya Raia kutoka Bangladesh na Waislamu jamii ya Rohingya wamekuwa katika bahari ya Andaman kwa majuma kadhaa sasa.
Thailand,Malaysia na Indonesia zimekataa kuwaruhusu kuingia katika pwani za nchi zao.CHANZO:BBC (Muro)

Rais Wa Msumbiji Felipe Jacinto Nyusi alihutubia Bunge Dodoma

Rais Wa Msumbiji Felipe Jacinto Nyusi akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo mjini Dodoma huku Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na Spika wa Bunge hilo Mh.Anna Makinda wakisikiliza.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mgeni wake Rais wa Msumbiji Felipe Jacinto Nyusi,Waziri Mkuu Mizengo Pinda,Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na viongozi waandamizi katika serikali ya Msumbiji wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Rais wa Msumbiji kulihutubia Bunge lao mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa CCM Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikweteakimtambulisha katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana kwa Rais wa Msumbiji Felipe Jacinto Nyusi wakati Rais huyo wa Msumbiji alipowasili katika makao makuu ya CCM m.Jakayajini Dodoma na kuzungumza na viongozi waandamizi .Kushoto ni Naibu katibu Mkuu wa CCM Bwana Mwigulu Nchemba.
 
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania Mh.Anna Makinda akimkaribisha Rais wa Msumbiji Felipe Jacinto Nyusi katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma ambapo Rais huyo alilihutubia Bunge hilo.
Rais Wa Msumbiji Felipe Jacinto Nyusi akipokea heshima muda mfupi baada ya kuwasili katika viwanja vya Bunge mjini Dodoma akisindikizwa na mwenyeji wake Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete.
Rais wa Msumbiji Felipe Jacinto Nyusi akisaini kitabu cha wageni ofisini kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo huku Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na Spika Mhe.Anna Makinda wakishuhudia. (Picha na Freddy Maro).(Muro)

Michuano ya COSAFA yaanza Africa Kusini

Michuano ya COSAFA,nchini Afrika Kusini
Michuano ya kumi na tano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu kusini mwa Afrika,COSAFA imezikutanisha timu za ukanda huo nchini Afrika Kusini. Michuano hiyo ilianza kutimua vumbi Jumapili mei 17 na itakamilika mei 30
Timu 12 kati ya 14 kutoka nchi wanachama wa COSAFA tayari zipo nchini Afrika Kusini kuchuana katika mashindano hayo. Angola na Comoro ambazo ni wanachama wa COSAFA hazikuweza kushiriki mwaka huu.
Nafasi zao zimechukuliwa na Ghana iliyofikia fainali za michuano ya Caf ya mwaka huu na Tanzania kutoka ukanda wa Afrika mashariki na kati ikiwa mwanachama wa CECAFA.
Timu nane zenye viwango vya chini kwa ubora kwa mujibu wa takwimu za FIFA kwa mwezi Februari, zimepangwa katika makundi mawili yenye timu nne kila moja, Tanzania ikiwemo katika michuano hiyo.
Kundi A lina timu za Zimbabwe, Namibia, Seychelles na Mauritius. Ambapo kundi B lina timu za Madagascar, Lesotho, Swaziland na Tanzania.
Katika kundi A Zimbabwe inaoongoza kundi hilo kwa kujikusanyia pointi sita baada ya michezo miwili ikifuatiwa na Namibia yenye pointi nne. Seychelles ni ya tatu na pointi moja. Mkiani ni Mauritius ambayo haina pointi.
Na katika kundi B, Madagascar na Swaziland zote zina pointi tatu, huku Lesotho na Tanzania zikiwa mikono mitupu.
Tanzania leo,Jumatano inarusha karata yake ya pili kwa kupambana na Madagascar baada ya kucharazwa bao 1-0 na Swaziland katika mchezo wake wa kwanza.
Timu za juu katika kila kundi zitasonga mbele hatua ya mtoano, ambapo timu sita za viwango vya juu zitaingia katika mashindano hayo yakiwa katika hatua ya robo fainali na kuendelea. Afrika Kusini kutokana na ubora wake itapambana na Botswana hatua ya robo fainali.CHANZO:BBC (Muro)

ELIMU YA KATIBA INAYOPENDEKEZWA, ZAMU YA WANANCHI WA WETE, PEMBA

SHEHA wa shehia ya Kipangani Ali Said Hamad akifungua mkutano wa kuelimisha katiba inayopendekezwa, ulioandaliwa na Kituo cha Hudma za Sheria Zanzibar ZLSC, tawi la Pemba, kulia ni Hakimu wa Mahakama ya Ardhi mkoa kusini Pemba Salim Hassan Bakar na kushoto ni Mratibu wa ZLSC Fatma Khamis Hemed.
MWANASHERIA wa serikali Albaghir Yakout Juma, akitoa ufafanuzi wa Katiba inayopendekezwa mbele ya wananchi wa wilaya ya wete Pemba, mkutano ulioandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC tawi la Pemba, ambao uliofanyika Jamhuri Hall wete Pemba
MMOJA wa wananchi wa wilaya ya Wete akitaka ufafanuzi wa Ibara ya 97 juu ya 'Bunge kumshitaki rais' kwenye katiba inyopendekezwa, wakati Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ZLSC walipofika kutoa elimu ya katiba hiyo kwa wananchi gazi ya wilaya. Picha na Haji Nassor, Pemba(Muro)

MAHAKAMA YA HAKI ZA BINADAMU YA AFRIKA YAWANOA WAANDISHI WA HABARI ARUSHA

Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya kimataifa la Ujerumani(GIZ)inayosaidia kujenga uwezo wa taasisi za Uongozi na Utawala bara la Afrika,Dk Iris Breutz akizungumza wakati wa semina ya siku nne ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kutoka nchi za Afrika Mashariki namna Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu(AfCPHR) inavyofanya kazi zake leo jijini Arusha,kushoto ni Jenerali Ulimwengu ambaye ni mwezeshaji na Mkuu wa Mawasiliano wa AfCPHR,Chatbar Sukhdev.
Mkuu wa Mawasiliano wa AfCPHR,Chatbar Sukhdev akitoa nasaha zake kwenye semina hiyo itakayowapa waandishi wa habari uelewa mpana wa Mahakama hiyo yenye makao yake jijini Arusha.
Baadhi ya waandishi wa habari wakijifunza mambo mbalimbali yanayohusu kulinda Haki za Binadamu barani Afrika.
Wawezeshaji wa semina hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari .(Muro)

Ramsey sasa ndio mkufunzi mkuu wa QPR

Chris Ramsey
wachezaji wa klabu ya QPR
Kilabu ya QPR imemuajiri Chris Ramsey kama mkufunzi mkuu kwa kandarasi ya miaka mitatu.
Ramsey mwenye umri wa miaka 53 alipewa kazi hiyo hadi mwisho wa mwezi Februari baada ya Harry Redknapp kujiuzulu lakini alishindwa kuizuia kilabu hiyo kusalia katika ligi kuu ya Uingereza.
''Chris alipochukua ukufunzi wa timu hii tayari tulikuwa katika matatizo makubwa'', alisema mwenyekiti wa kilabu hiyo Tony Fernandes.
Licha ya kushushwa daraja,sisi kama bodi tumefurahishwa na kazi ya Ramsey aliyofanya.
QPR imeshinda mechi tatu kati ya 14 zilizosimamiwa na Ramsey huku wakitarajiwa kucheza mechi ya mwisho dhidi ya Leicester.CHANZO:BBC (Muro)

Raheem Sterling kuipa kisogo Liverpool? 


Raheem Sterling,mshambuliaji wa Liverpool
Raheem Sterling wa Liverpool anatarajia kumuaga kocha wa klabu hiyo Brendan Rodgers na kuondoka Anfield msimu huu.
Mshambulizji huo katika ligi ya England tayari amekwisha saini mkataba mwingine wa kiasi cha Paund laki moja kwa wiki na kukanusha kuwa yeye hana tamaa na pesa,kama alivyohojiwa na BBC.
Mchezaji huyo anatarajiwa kukutana na Mkurugenzi wake Ian Ayre na Kocha wake Rodgers siku ya ijumaa,ambapo atakuwa tayari kuwaeleza kuwa sasa anapaswa kuiipa kisogo klabu hiyo.
Hata hivyo klabu hiyo ya Liverpool haijataka kusema lolote kwa sasa japo kuwa inaeleweka kuwa bado wanamhitaji mchezaji huyo kinda mwenye umri wa miaka 20 na ambaye mkataba wake unaisha mwaka 2017.
Klabu kadhaa zimeonyesha nia ya kumsajili mchezaji huyo, ikiwemo Manchester City,Arsenal pamoja na timu nyingine kubwa Ulaya zinamhitaji pia.
Hata hivyo Kaptain wa Liverpool Steven Gerrard akizungumza sikuya Ijumaa wiki iliyopita alimtaka Sterling kubakia katika timu hiyo na kusisitiza kuwa ni vizuri kuwa katika klabu ambayo kocha ana imani na wewe.CHANZo:BBC (Muro)

KITUO CHA AFYA CHA AAR HEALTHCARE CHAHAMIA BARABARA YA BAGAMOYO 

Muonekano wa jengo la Tropical Centre barabara ya Bagamoyo maeneo ya Victoria jijini Dar es salaam ambapo kituo cha AAR Healthcare kinapatikana hivi sasa katika ghorofa ya pili.
Sehemu za ndani za kituo kipya cha AAR
Kituo maarufu cha afya cha AAR Healthcare sasa kimehamia ghorofa ya pili katika jengo la Tropical Centre lililopo barabara ya New Bagamoyo road na Uporoto Street maeneo ya Victoria jijini Dar es salaam, kutoka mtaa wa Chato, na kinaendelea kutoa huduma zake bora kwa wananchi katika mazingira ya kisasa zaidi kila siku kwa kuanzia saa moja unusu asubuhi hadi saa mbili usiku.(Muro)