MADAKTARI WANAFUNZI 300 KUTOKA NCHI MBALIMBALI KUKUTANA ARUSHA WIKI IJAYO
Na: Heka Wanna na Shakila Galus-MAELEZO_DAR ES SALAAM
ZAIDI ya wanafunzi 300 wa udaktari
kutoka nchi mbalimbali duniani wanatarajiwa kufanya mkutano wa
kimataifa utakaojadili jinsi ya kutatua migogoro katika sekta ya Afya
kwenye ukanda wa Afrika.
Hayo yalisemwa na Rais wa Chama
cha Wanafunzi wa Udaktari Tanzania(TAMSA) Francis Tegete wakati
akizungumza na waandiishi wa habari jana jijini Dar es salaam.
Alisema kuwa washiriki wa mkutano
huo watajadiliana jinsi ya kuboresha rasilimali watu ,sera za afya na
miundo mbinu ya kutolea huduma ya afya katika nchi zao ili kutimiza
malengo ya Melinia .
Alisema kauli mbiu ya mkutano huo
inalenga kujadili migogoro ya afya barani na jinsi ya kuitatua kwa
ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi hasa wanaoishi katika mazingira
magumu na vijijini.
Tegete aliongeza kuwa mkutano huo
utakuwa muhimu kwa wanafunzi wa udaktari nchini kupata fursa ya
kubadilishana uzoefu na wenzao wa jinsi gani wanavyoweza kusaidia katika
utoaji wa huduma za afya ikiwemo upunguzaji wa vifo vya watoto na mama
wajawazito.
Alisema kuwa mkutano huo
utafunguliwa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt Hussein Mwinyi
siku ya Jumanne tarehe 18 na kumalizika 22 Disemba mwaka huu jijini
Arusha.
Baadhi ya washiriki wanatoka
Marekani , Uingereza, Lebanon, Sierra Leone , Uganda, Kenya , Rwanda,
Burundi, Congo, Korea Kusini, Sudan, Zambia , Ethiopia na Sweden .
No comments:
Post a Comment