SERIKALI YATENGE SH.BILLION MOJA KUJENGE DARAJA LA KAVUU
SERIKALI
imetenga kiasi cha sh. bilioni moja kwa ajili ya kazi za awali za
ujenzi wa daraja la mto Kavuu linalounganisha kata za Mamba, Kasansa,
Majimoto, na kijiji cha Inyonga yalipo makao makuu ya wilaya mpya ya
Mlele.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu
Mizengo Pinda jana jioni (Jumatano, Desemba 19, 2012) wakati akizungumza
na wakazi wa kata ya Mamba kwenye uwanja wa mpira akiwa katika siku ya
saba ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.
Waziri Mkuu alisema Serikali ina
nia ya kufungua mawasiliano kati ya bonde la Rukwa na mikoa ya
kaskazini ambako kuna uhaba wa chakula. “Bonde hili linasifika kwa
uzalishaji mkubwa wa nafaka kwa hiyo kujengwa kwa daraja hilo ni
ukombozi mkubwa wa kufungua soko kwa mazao mnayozalisha huku,” alisema.
Alisema katika mwaka huu wa
fedha, barabara ya kutoka Sitalike kupitia Kibaoni, Majimoto, Mamba hadi
Kasansa yenye urefu wa kilomita 33.5 imetengewa sh. milioni 837/- na
kwamba wakandarasi wawili wamekwishapatikana ili kuifanyia ukarabati
barabara hiyo.
Kuhusu barabara ya Majimoto hadi
Inyonga yenye urefu wa kilometa 135, Waziri Mkuu alisema zimetengwa sh.
milioni 943/- kwa ajili ya ujenzi wa madaraja katika barabara hiyo.
Alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa
fedha hizo, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Katavi,
Mhandisi Isaack Kamwelwe alimthibitishia Waziri Mkuu kuwepo kwa fedha
hizo.
“Fedha zimeshatengwa na leo
nimepokea kibali cha kutangaza zabuni za ujenzi wa daraja hilo. Zabuni
zitatangazwa kuanzia Januari 2013,” alisema.
Kutokuwepo kwa daraja la Kavuu
kunawafanya wakazi waishia bonde la Rukwa (maeneo ya Majimoto na Mamba)
kila wanapotaka kwenda Inyonga, walazimike kupitia Mpanda yaliko makao
makuu ya wilaya yao ambako ni zaidi ya kilometa 350.
Kesho (Ijumaa, Desemba 21, 2012)
Waziri Mkuu atakwenda kata ya Usevya ambako atazindua mradi wa umemejua
kwenye sekondari ya kata ya Usevya na kuhutubia wananchi.
No comments:
Post a Comment