SHERIA MPYA YA UVUVI NAMBA 7 YA MWAKA 2010 YAJADILIWA ZANZIBAR
NA: RAMADHANI ALI/MAELEZO
Washiriki wa semina ya Uelewa juu ya Athari za uvuvi
haramu na udhibiti wake unaotokana na sheria mpya ya uvuvi namba 7 ya mwaka 2010
wameeleza kutoridhika na ushirikiano mdogo wanaopata kutoka Idara ya
uvuvi.
Wakitoa michango katika semina
iliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika Hoteli ya Zanzibar
Beach Resort, Mbweni, washiriki hao ambao ni Majaji, mahakimu na waendesha
mashtaka wamesema tatizo hilo limepelekea kesi nyingi zinazohusu
uvuvi haramu kufutwa kwa kukosa ushahidi.
Wamesema tatizo la kesi za uvuvi haramu
zinazopelekwa kwenye vyombo vya sheria ni ushirikiano mdogo unaotolewa na
Idara ya Uvuvi kwa wapelelezi, Waendesha Mashtaka na Mahakimu
wanaosimamia kesi hizo.
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kusini Unguja
Jongo Juma Jongo amesema ili kupunguza tatizo la uvuvi harama Zanzibar, Idara ya
uvuvi inapaswa kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo vifaa vya kuvulia ili kuweza
kuendeleza maisha yao.
Amesema utaratibu wa sasa unaofanywa na Idara hiyo ya
kutoa zana chache za uvuvi kwa wavuvi wa kijiji kizima hauwezi kuwakomboa wavuvi
kuacha uvuvi usiotakiwa.
Ameshauri baada ya wavuvi kupatiwa vifaa
vinavyokubalika, Idara iweke bandari rasmi kwa ajili ya wavuvi
kuuza samaki na wale watakaopatikana na makosa ya kuvua kinyume na
sheria washughulikiwe.
Akizungumzia sheria mpya ya uvuvi namba 7 ya mwaka 2010,
Mkurugenzi wa Idara ya uvuvi Mussa Aboud Jumbe amesema lengo ni kuwaongezea
kipato wavuvi na kulinda rasilimali za baharini kwa ajili ya kizazi cha sasa na
kizazi kijacho.
Amesema uvuvi wa kutumia baruti, mabomu, sumu ama nyavu
za macho madogo yanaharibu mayai ya samaki na samaki wadogo ambao
hawajafikia kiwango cha kuvuliwa.
Mkurugenzi wa Idara ya uvuvi amewaeleza washiriki wa
semina hiyo kuwa Serikali inampango wa kuliongeza eneo la Hifadhi ya Ghuba ya
Menai kutoka bahari ya Mzuri hadi kufikia kijiji cha Bwejuu, Kati Mashariki ya
kisiwa cha Unguja ambapo vijiji 27 vitaingizwa katika Hifadhi
hiyo.
Aidha amesema Serikali inafikiria kuligawa eneo la
Hifadhi ya Kisiwa cha Mnemba na Ghuba ya Chwaka na kuanzisha eneo la hifadhi
mpya ya Tumbatu.
Mapema akifungua Mkutano huo Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Abdillah Jihad Hassan amesema sheria mpya namba 7 ya mwaka 2010 iliundwa baada
ya kupata michango ya Kamati za uvuvi za vijiji vyote vya Unguja na
Pemba.
Amesema sheria hiyo ni mali ya wavuvi wenyewe na hakuna
sababu ya kwenda kinyume na wanapaswa kuilinda na kuitekeleza kwa
vitendo.
No comments:
Post a Comment