WAZIRI MKUU AKAGUA MRADI WA UMWAGILIAJI UGALLA
WAZIRI
 MKUU Mizengo Pinda ametembelea mradi wa umwagiliaji wa Ugalla na kusifu
 juhudi za wananchi wa kata hiyo katika wilaya mpya ya Mlele mkoani 
Katavi.
Alikuwa akizungumza na wakazi wa
 kijiji cha Ugalla kata ya Ugalla mara baada ya  kukagua mradi huo akiwa
 katika siku ya nne ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, 
mkoani Katavi jana mchana.
Alisema anawashukuru wakazi hao 
kwa kuibua mradi huo ili waweze kunufaika na maji ya mto Ugalla ambao 
unapita jirani. Pia aliwataka waheshimu uamuzi wao wa kutoa eneo hilo 
kwa mradi ili kuepuka migogoro ya umilikaji wa kifamilia na kiukoo.
“Ninawasihi muelewane ili 
kuepuka migogoro ya maeneo. Mkishaanza kuvuna wako watakaodai kuwa hapa 
nilipewa na babu yangu, hapa nilipewa na babu wa babu, wataanza kudai 
fidia. Ni vema mkaelewana mapena juu ya umiliki wa enepo la mradi,” 
alisema.
Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu 
ambaye ni mbunge wa jimbo hilo, Mhandisi Mkazi wa Umwagiliaji Kanda ya 
Mbeya, Bw. Elibariki Mwendo alisema wamejenga tanki la kuhifadhi maji 
lenye ujazo wa lita 530,000 ambazo zinaweza kumwagilia hekta 225.
Alisema mitambo ya kupandisha 
maji kwenye tanki hilo itaendeshwa kwa kutumia nguvu ya umeme wa jua 
pamoja na umeme unaozalishwa kwa nguvu ya upepo.
Mradi huo ulioibuliwa na 
wananchi mwaka 2007 kupitia zoezi la fursa na vikwazo vya maendeleo, 
umegharimu  sh. milioni 778. Unamilikiwa na wanachama 146 na utahudumia 
watu 3,077.
Leo (Jumanne, Desemba 18, 2012) Waziri Mkuu atakwenda kata ya Sitalike ambako atahutubia wananchi.
No comments:
Post a Comment