BODI YA CHUO CHA HABARI ZANZIBAR YAZINDULIWA
Picha ya pamoja ya wajumbe wapya wa Bodi hiyo wakiwa na Waziri wa Habari Utamaduni,Utalii na Michezo Saidi Ali Mbarouk.(Picha na Makame Mshenga)
Na: Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar
Waziri wa Habari Utalii Utamaduni
na Michezo Said Ali Mbarouk amesema kuwa juhudi na utendaji kazi mzuri
wa wajumbe wa Baraza la Chuo cha Uwandishi wa habari Zanzibar ndizo
zitakazokipa sifa nzuri na ubora wa hali ya juu Chuo hicho.
Ameyasema hayo jana huko katika
ukumbi wa Chuo cha Habari Vuga mjini Zanzibar wakati akizindua Bodi mpya
ya Baraza la Chuo hicho.
Waziri Mbarouk amesema ubora wa
taaluma inayopatikana Chuoni hapo inatokana na juhudi za makusudi ambazo
zinapaswa kufanywa na Wajumbe wa Bodi hiyo mpya ambao wana wajibu wa
kushauri na kuelekeza namna bora ya kukiendeleza Chuo.
Amesema kushindwa kuwajibika kwa
Bodi hiyo kutakifanya chuo kushindwa kutimiza malengo yake na kuwafanya
wahitimu wake kuhitimu bila ya vigezo vinavyokubalika hasa katika
kipindi hiki cha ushindani.
“ Ili twende na wakati uliopo
hivi sasa lazima Chuo kitoe wataalamu waliobobea katika fani za habari
za kisasa na wenye vipaji vya kuweza kukabiliana na soko la ajira kwa
faida yao na Taifa kwa ujumla” Alisema Waziri.
Waziri huyo aliwataka wajumbe wa
bodi hiyo kukikuza na kukiendeleza chuo hicho kwa ufanisi mkubwa ili
kuwa mfano wa kuigwa katika vyuo vingine.
Alisema kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ina matumani makubwa na Bodi hiyo mpya na kwamba
itaweza kukabiliana na changamoto ambazo zinaweza kujitokeza katika
kipindi chote cha uwepo wa Bodi hiyo.
Alizigusia
baadhi ya Changamoto zinazokikabili Chuo hicho kuwa ni pamoja na Uhaba
wa Madarasa na Ofisi na kuwataka Wajumbe wa Bodi hiyo kufikiria na
kupanga namna bora kukukabiliana na jambo hilo.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Chande Omar aliishukuru Serikali
kwa kuteuliwa na kuahidi kuwa watatekeleza kazi zao ipasavyo kwa mujibu
wa sheria zinavyoelekeza.
Amesema kuwa watajitahidi kufanya kazi kwa mashirikiano ya hali yajuu ili kutimiza malengo ya Chuo kama yalivyopangwa.
Bodi
hiyo iliyoteuliwa ina jumla ya Wajumbe saba ambao ni Saleh Yusuf
Mnemo,Salim Said Salim, Ali Nasor Sultan, Najma Khalfani Juma,Yussuf
Omar Chunda na Asha Bakari Makame na Mwenyekiti wao Chande Omar Omar.
No comments:
Post a Comment