MAJAMBAZI WAPORA MAITI NA KUIPEKUA
Mhudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti hospitali ya Mkoa  Singida, 
akirekebisha mapambo ya jeneza lililokiwa na mwili wa marehemu Munchari 
Lyoba, mwanafunzi wa SUA , jeneza lililovunjwa na majambazi na maiti 
kupekuliwa yakitafuta fedha zaidi baada ya kupora wasindikizaji. (Picha 
na Gasper Andrew)
            
  
WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamevamia gari lililokuwa linasafirisha maiti kutoka mjini Morogoro kwenda mkoani Mara kisha kupora takriban Sh19.8 milioni walizokuwa nazo waombolezaji.
WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wamevamia gari lililokuwa linasafirisha maiti kutoka mjini Morogoro kwenda mkoani Mara kisha kupora takriban Sh19.8 milioni walizokuwa nazo waombolezaji.
Katika tukio hilo la kusikitisha lililotokea juzi 
mkoani Singida,  majambazi hao walivunja vioo vyote vya gari pamoja na 
jeneza lililokuwa na mwili wa Munchari Lyoba aliyekuwa mwanafunzi  wa 
mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) cha Morogoro na 
kumpekua marehemu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya 
chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa wa Singida, mkuu wa 
msafara uliokuwa ukisafirisha maiti,  Makaranga alisema kuwa tukio hilo 
lilitokea juzi saa 7:30 usiku katika gari aina ya Land Cruiser mali ya 
SUA.
Akisimulia tukio hilo, Makaranga alisema kuwa 
lilitokea katika Barabara Kuu ya Dodoma – Mwanza nje kidogo ya Mji wa 
Singida kwenye kona maarufu kwa jina la Mohammed Trans kuelekea mkoani 
Mara.  
Alisema kuwa gari hilo pamoja na jeneza, 
lililobeba viongozi wa wanafunzi sita na viongozi wengine wanne 
lilipofika eneo la tukio, walikuta mawe makubwa yamepangwa barabarani na
 kuwalazimisha kusimama ndipo wakavamiwa na kundi kubwa la vijana, ambao
 walibeba bunduki mbili aina ya gobore, marungu, mashoka na mawe.  
“Walipofika walipiga kioo cha gari letu kwa mbele 
na kumparaza kwa panga usoni dereva wetu. Baada ya hapo walivunja vioo 
vyote na kutuamuru kutoa kila kitu tulichokuwa nacho,” alisema 
Makaranga.  
Makaranga alisema kuwa katika tukio hilo, aliporwa
 Sh2 milioni alizokabidhiwa azihifadhi kwa ajili ya kugharimia msafara 
huo, Sh8.8 milioni zilizochangwa na wanafunzi kama rambirambi kwa 
 mwenzao na jumla ya Sh9 milioni ambazo wasindikizaji walikuwa nazo 
mifukoni mwao.  
“Pia tuliporwa simu  zetu zote  za mikononi, viatu, laptop na mabegi yote ya nguo zetu,” alisema.  
Makaranga aliyeeleza kuwa anafanya kazi za 
kiutawala SUA, aliwataja walioumizwa na majambazi hao kuwa ni pamoja na 
yeye, dereva wao na kiongozi wa wanafunzi, Idd Idd ambao walitibiwa 
katika Hospitali ya Mkoa wa Singida na kuruhusiwa.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mwalimu Queen Mlozi, 
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa amewasiliana na 
uongozi wa SUA ili watume gari lingine na kukarabati jeneza 
lililoharibiwa na majambazi hao.
Mlozi aliongeza kuwa kwa ushirikiano wa Jeshi la 
Polisi na Kamati ya Ulinzi na Usalama, watahakikisha watu waliofanya 
unyama huo, wanakamatwa haraka iwezekanavyo ili waweze kufikishwa mbele 
ya vyombo vya sheria.  
“Nimesikitishwa sana na tukio hili, inaelekea sasa
 binadamu tunaanza kutoka kwenye utu na kuhamia kwenye vitendo ambavyo 
binadamu wa Mwenyezi Mungu hawezi kuthubutu kuvifanya. Watu wanafikia 
hata kufungua jeneza na kuanza kulisachi,” alisema  Mlozi akionyesha 
masikitiko.  
Soma zaidi: http://www.mwananchi.co.tz/habari
Soma zaidi: http://www.mwananchi.co.tz/habari

No comments:
Post a Comment