WAZIRI MKUU KUTOA MIZINGA 25 KWA KIKUNDI CHA SANAA
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda ameahidi kutoa mizinga ya nyuki 25 ya kisasa na ya
kibiashara kwa ajili ya kikundi cha sanaa cha kata ya Mamba wilayani
Mlele mkoani Katavi ili waweze kuzalisha mali na kujiendesha wenyewe.
Alitoa ahadi hiyo jana jioni
(Jumatano, Desemba 19, 2012) wakati akizungumza na wakazi wa kata ya
Mamba kwenye uwanja wa mpira akiwa katika siku ya saba ya ziara yake
jimboni kwake Katavi wilayani Mlele, mkoani Katavi.
“Nitawapa mizinga 25 ya kuanzia
ili muongeze na ile miwili mliyopewa na Dk. Kikwembe (Mbunge wa Viti
Maalum mkoa wa Katavi)… nataka ninyi muwe chachu ya mabadiliko hapa
mamba ili vijana wengine na wazee waige kutoka kwenu,” alisema.
Aliwataka wabadili mtazamo wao
katika kufuga nyuki kwa kuweka mizinga ardhini au kwenye mabanda badala
ya kuitundika kwenye miti. “Mnapaswa kufuga kisasa ili muweze kuikagua
mara kwa mara, sasa ukiitundika juu ya mti utaendaje kuchungulia kama
nyuki wameingia kwenye mzinga au la? Utajuaje kama masega yaliyomo yana
asali ya kutosha? Alihoji.
Alisema wanapaswa watambue kwamba nyuki anafugwa kama ilivyo kwa viumbe wengine kama vile kuku, mbuzi, bata au ng’ombe.
“Faida mtakayopata hapa ni kuwa
karibu na msitu wa Lyamba lya Mfipa. Tungeweka mizinga pale chini ya
msitu jioni hii, kesho asubuhi mngekuta nyuki wameshaingia na kuanza
kazi,” aliongeza.
Kesho (Ijumaa, Desemba 21, 2012)
Waziri Mkuu atakwenda kata ya Usevya ambako atazindua mradi wa umemejua
kwenye sekondari ya kata ya Usevya na kuhutubia wananchi.
No comments:
Post a Comment