SERIKALI KUCHUKUA HATUA ILI KUMILIKI HIFADHI ZA MADINI YA MAKAA YA MAWE
Waziri wa Nishati na Madini akimsikiliza Balozi wa China Bw. Lu Youqing (katikati), kushoto ni Mkalimani aliyeongozana na balozi huyo.
Na:Mohamed Saif
Waziri wa Nishati na
Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa serikali inajipanga kuanza
kuchukua hatua ili kuiwezesha kumiliki hifadhi yote ya madini ya makaa ya mawe iliyopo
nchini kwa kuwa madini hayo ni ya kimkakati.
Kwa mujibu wa Profesa
Muhongo, madini yote ya kimkakati (strategic minerals), yakiwemo makaa ya mawe
yanapaswa kuwa chini ya umiliki wa serikali ili iweze kudhibiti uvunwaji wake
na biashara yake kwa ujumla kwa malengo mahsusi yaliyopangwa kwa manufaa ya
watanzania.
Akifafanua zaidi,
Mheshimiwa Waziri alisema taratibu zote zikikamilika na serikali kutwaa umiliki
wa hifadhi ya madini hayo, itaweza kudhibiti matatizo mbalimbali yanayojitokeza
katika sekta husika likiwemo la baadhi ya wamiliki wa maeneo yenye madini hayo kuyashikilia
kwa muda mrefu wakisubiri kuingia ubia na wawekezaji wengine au kuuza madini
hayo nje ya nchi hali inayosababisha watu makini wenye nia ya kuwekeza katika
maeneo hayo kushindwa kufanya hivyo kwa kukosa maeneo na hivyo kuchelewesha
maendeleo kwa wananchi.
Waziri alitoa kauli
hiyo jana ofisini kwake jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na watendaji
toka Kampuni ya Sichuan Hongda ya China waliofika kumtembelea wakiongozana na
Balozi wa China hapa nchini Mheshimiwa Lu Youqing kwa lengo la kujadili masuala
mbalimbali yanayoigusa sekta ya nishati nchini ikiwemo mradi wa makaa ya mawe
wa Mchuchuma.
Katika mazungumzo
hayo, Balozi Youqing aliweka bayana kuwa katika mradi huo, kampuni ya Sichuan
Hongda inatarajia kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 600 na kwamba megawati
400 kati ya hizo zitaingizwa kwenye gridi ya Taifa ifikapo mwaka 2018. Alisema
megawati 200 zitatumika kuendeshea mitambo.
Kwa upande wake,
Waziri Muhongo aliliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kufanya
mazungumzo na kampuni hiyo ili mradi huo uanze mara moja. Alisema mradi huo
umechukua muda mrefu pasipo kuwa na mafanikio na hivyo akasisitiza kuwa umefika
wakati sasa watanzania waone mradi huo ukianza kutekelezwa ili wafaidi matunda
yake.
Aidha, Profesa
Muhongo aliitaka Tanesco kuanza mazungumzo na kampuni hiyo kuhusu ujenzi wa
miundombinu ya kusafirisha umeme kutoka Mchuchuma hadi Mbeya akifafanua kwamba
suala la uzalishaji umeme lazima liende sambamba na uboreshaji wa miundombinu
ya usafirishaji pamoja na usambazaji ili kupata matokeo chanya.
No comments:
Post a Comment