Serikali kuendelea kuboresha mafunzo ya JKT
Picha na Hassan Silayo - MAELEZO
WIZARA YA ULINZI NA JKT
MKUTANO NA VYOMBO VYA HABARI
Wizara ya Ulinzi na JKT itaendelea kuboresha mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria
Wizara ya Ulinzi na JKT itaendelea
kuboresha mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria. Hatua hii inafuatia
kurejeshwa upya kwa mafunzo hayo kama Serikali ilivyokuwa imeahidi.
Mafunzo hayo yaliyoanza mapema 2013
yanatarajiwa kuwahusisha vijana 41,341 waliomaliza kidato cha sita
katika shule mbali mbali nchini. Katika awamu ya kwanza vijana 5,000
(12%) walitakiwa kuhudhuria mafunzo kwa muda wa miezi mitatu kuanzia
mwezi Machi 2013 hadi Juni 2013.
Awamu ya pili ya mafunzo hayo
iliyoanza mwezi Juni JKT ilitarajiwa kuchukua vijana 10,000 (24%) na
kumaliza mafunzo yao mwezi Septemba 2013. Katika awamu ya tatu
itakayoanza mwezi Oktoba 2013 JKT itachukua vijana 15,000 (37%). Aidha,
awamu ya nne JKT itachukua vijana 11,341 (27%) mwanzoni mwa Januari 2014
na vijana hao watamaliza mafunzo mwezi Aprili, 2014 na hivyo
kukamilisha idadi ya vijana waliomaliza kidato cha sita kwa mwaka 2013.
Utoaji wa mafunzo haya kwa miezi
mitatu mitatu unafuatia maagizo ya Serikali kwani kwa muda wa miezi sita
iliyokusudiwa wakati wa kurejesha mafunzo hayo ni wazi vijana wengi
wasingepata fursa hiyo adhimu.
Changamoto kubwa zinazolikabili JKT ni
pamoja na hofu wanayokuwa nayo wazazi kutokana na visingizio
wanavyopewa na vijana baada ya kuwasili makambini. Tunawaasa wazazi
kutojengewa hofu kwa taarifa zisizo rasmi wanazopewa na watoto wao kwani
Wizara ilizifanyia kazi hofu zilizoelezwa na vijana na kubaini kuwa
hazina ukweli. Kwa mfano, mtoto anadai kuwa anaumwa na hapati matibabu,
lakini tunapofuatilia tunamkuta yupo kwenye gwaride (mzima wa afya.
Chakufurahisha baadhi ya vijana hao hao wakati wa kumaliza mafunzo
wamekuwa hawana haraka tena ya kuondoka makambini!
Pili, lipo tatizo la kukwepa mafunzo
(dodging). Mfano katika awamu ya kwanza tulitarajia kupokea vijana 5,000
lakini waliojitokeza ni 4,712 (vijana 288 wakiwa wamekwepa mafunzo).
Katika awamu ya pili kati ya vijana 10,000 ni vijana 9,510 tu ndio
waliojitokeza, (watoro 490). Tunapenda kuwahakikishia wote wanaokwepa
mafunzo kuwa wataendelea kufuatiliwa na mara watakapopatikana hatua za
kuwarejesha katika mafunzo zitachukuliwa.
Changamoto ya tatu ni kutopatikana kwa
huduma za mtandao (internet) makambini. Wizara inatambua umuhimu wa
mtandao na hivyo juhudi zitafanyika siku za usoni kuyaunganisha makambi
kwa kadri mkonga wa Taifa unavyozidi kuenea nchini. Hata hivyo, kijana
anayekuwa mafunzoni kwa miezi mitatu atajikuta hana muda wa kutumia
huduma hiyo kutokana na majukumu aliyonayo. Kwa wanaoomba nafasi vyuo
vya elimu ya juu upo utaratibu wa kuwaruhusu kutumia huduma zilizo nje
ya makambi.
Aidha, JKT linakabiliwa pia na
changamoto ya kutoa mafunzo kwa muda mrefu zaidi kutokana na maombi ya
vijana wanaomaliza na pia maombi ya waheshimiwa wabunge. Hii ni ishara
njema ya kuona umuhimu wa mafunzo yanayotolewa na kwa kadri makambi
yatakavyoongezeka nchini suala la muda wa mafunzo pia litaangaliwa.
Changamoto nyingine ni miundombinu
michache ikilinganishwa na idadi kubwa ya vijana wanaotarajiwa kumaliza
kidado cha sita na vyuo kila mwaka. Suluhisho la jambo hili litapatikana
baada ya kupanuliwa kwa makambi ya JKT.
Wizara inaendelea kushirikiana na
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kuwa na mpango utakaohakikisha
vijana wanaofaulu vizuri wanapata mafunzo mapema na kuwawezesha kujiunga
na vyuo vya elimu ya juu kwa wakati. Kwa wale wanaojiunga sasa na ambao
tayari wamedahiliwa, Wizara imewasiliana na Wizara ya Elimu na Mafunzo
ya Ufundi ili kupata orodha yao na hatimaye kuwawekea utaratibu wa
kujiunga na mafunzo hayo baada ya kumaliza masomo yao.
Imetolewa na Luteni Kanali Juma Nkangaa Issa Sipe,
Msemaji, Wizara ya Ulinzi na JKT,
Simu: 0756448787/0655878744/0784370500/0772516666.
Barua pepe:
jnisipe@modans.go.tz;
jnisipe@yahoo.com;
jnisipe@gmail.com.
No comments:
Post a Comment