TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Monday, October 21, 2013

TUME YA WARIOBA YAOMBA MUDA ZAIDI 

warioba_1_bc902.jpg
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeomba kuongezewa muda wa mwezi mmoja kutokana na ugumu wa kazi ya uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na wananchi na asasi mbalimbali.
Tume hiyo inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba ilitakiwa kufanya kazi kwa miezi 18 kwa mujibu wa Sura ya 83 ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Maana yake ni kuwa Tume hiyo iliyoanza kazi Mei 1, mwaka jana ilitakiwa kukamilisha kazi yake Novemba 1, mwaka huu.
Ikiwa maombi hayo ya Tume yatakubaliwa ina maana watatakiwa kukabidhi ripoti yake Desemba 1, mwaka huu.
Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Augustine Ramadhan aliliambia gazeti hili kwa simu jana kuwa wamepeleka serikalini maombi ya kuongezewa muda wa kufanya kazi.
Hata hivyo, Jaji Ramadhan alisema kuwa wameomba muda zaidi kutokana na kukabiliwa na kazi kubwa ya kuchambua maoni hayo.(P.T)
Alisema hakuwa na taarifa ya majibu ya kama ombi lao limekubaliwa au la.
"Hatukuomba miezi miwili kama sheria inavyotuelekeza, tumeomba mwezi mmoja na mpaka Ijumaa nilipotoka ofisini sikuwa na taarifa kama kibali kilikuwa kimetolewa, labda kesho (leo) nikienda ofisini nitafuatilia kufahamu kama kimetoka," alisema Jaji Ramadhan.
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alikiri kuwa tume hiyo imeomba kuongezewa muda.
"Ni kweli barua ya Tume imeletwa, tumeipokea na inafanyiwa kazi," alisema Rweyemamu kwa kifupi.
Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe akizungumza kwa njia ya simu; baada ya kuulizwa ikiwa Serikali imetoa kibali hicho au la alisema, "Sizungumzi na waandishi leo." Simu ikakatika.
Ahadi ya Warioba yashindwa kutekelezeka
Hatua hiyo inatofautiana na ahadi ya Jaji Warioba, ambaye mara nyingi amekuwa akisisitiza kuwa tume yake itamaliza kazi yake katika muda uliopangwa.
Jaji Warioba alitoa ahadi hiyo kwa mara ya mwisho wakati akizungumza na vyombo vya habari Septemba 26, mwaka huu.
"Mipango ya tume ni kukamilisha kazi hii ndani ya muda uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika Sura ya 83," alieleza Jaji Warioba wakati huo.
Tume imefuata sheria
Tume imeomba kuongezewa muda kama inavyoelekezwa kwenye kifungu cha kidogo cha (4) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
"Endapo Tume itashindwa kukamilisha kazi yake ndani ya kipindi kilichoelezwa katika kifungu kidogo cha (3), Rais kwa makubaliano na Rais wa Zanzibar, anaweza kuongeza muda usiozidi miezi miwili ili kuiwezesha Tume kukamilisha na kuwasilisha ripoti," kinaeleza kifungu kidogo hicho.
Bunge la Katiba na Kura ya Maoni sasa kuchelewa
Kutokana na ombi hilo la tume, maana yake sasa mkutano wa Bunge la Katiba utasogezwa mbele.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitakiwa kukabidhi kazi yake Novemba 1, lakini kwa kuomba muda ina maana wataathiri ratiba ya mkutano wa Bunge la Katiba.
Bunge la Katiba lilitakiwa kukutana katikati ya mwezi Novemba kujadili Rasimu ya pili ya Katiba baada ya kuwasilishwa na tume.
Maana yake sasa Bunge la Katiba kuna uwezekano mkubwa likakutana mwakani au Desemba mwishoni.
Pia suala hilo litaathiri mpangilio wa kura ya maoni, ambayo inatakiwa kuitishwa baada ya Bunge la Katiba kupitisha rasimu.
Ombi hilo kwa kiasi kikubwa linaweza kuathiri mchakato wa kupata Katiba ya Tanzania Bara ikiwa Katiba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Serikali tatu itapitishwa na wananchi.
Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment