BALOZI WA JAPAN ARIDHISHWA NA UJENZI WA DARAJA
Balozi wa
Japan Mheshimiwa Masaki Okada (wa kwanza kushoto) akiwa na Waziri wa
Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (nyuma ya Balozi) pamoja na
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Usafirishaji nchini Rwanda
Bw. Guy Kalisa (mwenye tai nyekundu) wakikagua eneo la kituo cha pamoja
cha ukusanyaji ushuru kwa upande wa Rwanda. (HD)
Balozi wa
Japan nchini Tanzania Mheshimiwa Masaki Okada ameelezea kuridhishwa na
utekelezaji wa mradi ujenzi wa daraja la kimataifa la Rusumo na kituo
cha pamoja cha ukusanyaji ushuru katika eneo la Rusumo mpakani wa
Tanzania na Rwanda. Miradi hiyo miwili mikubwa inayofadhiliwa na
Serikali ya Japan ilianza kujengwa mwezi Machi mwaka huu wa 2013 na
imepangwa kukamilika mwezi Novemba mwaka 2014.
"Nimeridhishwa
na viwango na kasi ya utekelezaji wa mradi huu" alisema Balozi Okada
wakati alipotembelea eneo hilo la mpakani mwa Tanzania na Rwanda ambapo
alisisitiza kuwa, inatia moyo kuona fedha zilizotolewa na nchi yake
zikitumika vizuri kwa lengo la kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Naye
Meneja wa Tanroads wa Mkoa wa Kagera Injinia John Kalupale akitoa
taarifa kwa Balozi huyo wa Japan ambaye alifuatana na Waziri wa Ujenzi
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, alielezea kuwa uamuzi wa kujenga
daraja jingine katika eneo hilo la mpakani, unatokana na mahitaji halisi
ya wakati huu kwani daraja linalotumika hivi sasa lilijengwa miaka 40
iliyopita likiwa na uwezo wa kubeba tani 32. Aliendelea kueleza kuwa
ingawa miaka ishirini baada ya ujenzi wa daraja hilo kulifanyika
ukarabati mkubwa kwa lengo la kuimarisha uwezo wake, bado kumeendelea
kuwepo kwa ongezeko kubwa la magari hasa yanayosafirisha bidhaa kati ya
Bandari ya Dar es Salaam na nchini jirani ya Rwanda.
Injinia
Hitoshi Kamega ambaye ni Mhandisi Mkazi wa Kampuni mbili zilizoungana
kuusimamia mradi huo ambazo ni Chodei Co. Ltd. na Nippon Koei Co,
amelezea kuwa ujenzi wa daraja hilo la Rusumo lenye urefu meta 80 pamoja
na kituo cha ushuru, unatekelezwa na Mkandarasi Daiho Co. kutoka Japan
kwa gharama ya Shilingi bilioni 31.736.
Waziri wa
Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hata hivyo alibainisha
kujitokeza kwa mapungufu katika baadhi ya maeneo ya mradi huo ambayo
wizara yake kwa kushirikiana na Ubalozi wa Japan hapa nchini
wanayafanyiakazi ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na uwiano mzuri wakati
wa utekelezaji wa mradi huo na pale huduma zenyewe zitakapoanza
kutolewa..
Waziri
Magufuli aliyataja baadhi ya mapungufu hayo kuwa ni pamoja na kutotengwa
kwa eneo la kutosha la maegesho ya magari kwa upande wa Tanzania na
kuhitajika kwa upanuzi wa majengo ya huduma za kiutawala hasa wakati wa
kutekeleza mipango ya baadaye kwa kuzingatia ongezeko la shughuli za
kibiashara linavyoonekana katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment