DK MAGUFULI AIBUKA UPYA
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli
ametoa mwezi mmoja kwa watumishi wa Serikali ambao wanadaiwa mikopo ya
nyumba kulipa madeni yao mara moja na kuonya kwamba ikiwa watashindwa
kulipa, watanyang'anywa nyumba hizo na watakopeshwa watu wengine.
Dk Magufuli ameibuka na hoja hiyo
mpya, zikiwa ni siku chache tangu alipopigwa 'stop' na Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda kutekeleza sheria ya kuondoa msamaha wa asilimia tano kwa
mizigo inayozidi kwenye malori, hali ambayo ilizusha mvutano mkubwa
baina ya Serikali na wasafirishaji wa mizigo nchini.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la
msingi kuzindua ujenzi wa nyumba 851 za watumishi wa Serikali eneo la
Mabwepande jijini Dar es Salaam, Dk Magufuli alisema watumishi 2500
hawajalipa mikopo ya nyumba walizonunua.(P.T)
Dk Magufuli alionya kuwa atafuatilia
suala hilo na kuhakikisha madeni hayo yanalipwa mara moja, huku
akimwomba Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal kumuunga mkono kwenye
jambo hilo, ambalo ni utekelezaji wa sheria za nchi.
"Naomba ifahamike kwamba tunapojenga
nyumba kwa ajili ya kuwakopesha watumishi wa umma tunataka kuboresha
makazi yao. Pia fedha tunazokusanya zinasaidia kujenga nyumba zaidi,"
alisema Dk Magufuli. Hata hivyo alisema hadi sasa watumishi wa Serikali
4,900 ambao walikopa nyumba hizo tayari wamelipa madeni.
"Mimi nafanya kazi kwa kufuata sheria
na kila mtumishi wa Serikali anafahamu jambo hilo, hivyo watu ambao
wanajua tunawadai wakae kwa tahadhari, kwani ndani ya mwezi mmoja kama
hawatalipa tutawachukulia hatua bila kupuuzia," alionya Magufuli.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Dk
Magufuli kutangaza kunyang'anya nyumba hizo, kwani alifanya hivyo
mwishoni mwa Machi mwaka jana pale alipouagiza uongozi wa Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA), kuwapa siku saba watu wote walionunua nyumba
hizo kulipa madeni yao.
Dk Magufuli aliwataka TBA kutoa ilani
ya maandishi inayowataka wahusika walipe fedha hizo ndani ya wiki moja
vinginevyo wangenyang'anywa kwa maelezo kwamba wanachelewesha malengo ya
TBA kujenga nyumba zaidi. Hata hivyo, hakuna taarifa zozote zilizowahi
kutolewa kuhusu kutekelezwa kwa amri hiyo iliyotolewa zaidi ya miezi 18
iliyopita.
Jana, Makamu wa Rais, Dk Bilal
alimuunga mkono Magufuli akisema: "Naunga mkono tamko la Waziri wa
Ujenzi kwamba ni lazima watumishi wa Serikali ambao wanakopeshwa nyumba
walipe haraka ili fedha hizo zisaidie kujenga nyumba nyingine."
Dk Bilal alikuwa mgeni rasmi katika
shughuli ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 851, kwenye eneo
la Bunju 'B' Kinondoni, Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius
Mwakalinga, alisema ujenzi huo unafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu
ya kwanza iligharimu Sh2 bilioni na awamu ya pili Sh1 bilioni.
"Nyumba 851 zinazojengwa Bunju B ni
sehemu ya ujenzi wa nyumba 4,400 katika Mkoa wa Dar es Salaam na nyumba
10,000 kwa nchi nzima," alisema Mwakalinga.
Hafla hiyo ilisimama takriban kwa
dakika 10 wakati Dk Bilal akitaka kuhutubia baada ya jenereta kushindwa
kufanya kazi, hivyo kumlazimu kurudi kuketi kwenye kiti hadi umeme
uliporejea. Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alilazimika
kwenda kufuatilia suala hilo na mafundi waliokuwapo walifanikiwa
kuunganisha mashine za kipaza sauti na umeme wa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco), hivyo Makamu wa Rais aliendelea kuhutubia.
Uuzaji wa nyumba
Nyumba nyingi za Serikali zilijengwa
kipindi cha utawala wa ukoloni wa Wajerumani uliodumu kati ya 1885 na
1919 na ule wa Waingereza ulioanza 1919 hadi 1961.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa
nyumba za Serikali zilizouzwa nchi nzima tangu mwaka 2002 wakati wa
uongozi wa awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa ni zaidi ya 6,000.
Malengo ya kuuza nyumba ni kwamba, fedha zilizopatikana zingetumika
kujenga nyumba nyingine kwa ajili ya watumishi wa Serikali katika maeneo
mbalimbali nchini yakiwamo Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Mwanza.
Hata hivyo, uuzaji huo ulikuwa na
utata hali iliyosababisha kupingwa vikali na watu wa kada mbalimbali
wakiwamo wanasiasa na wanaharakati, kwa maelezo kwamba uliwanufaisha
vigogo.
Malalamiko pia yalijengwa kwenye hoja
kwamba nyumba hizo ziliuzwa kwa bei ndogo ambayo haikuzingatia thamani
ya ardhi husika, huku wengine wakisema hakukuwa na umakini kwani
viongozi wengi walikosa makazi na hasa wale walioteuliwa baada ya Rais
Jakaya Kikwete kuingia madarakani.
Miongoni mwa walionunua nyumba hizo ni
mawaziri wengi, kama si wote, wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, hasa
katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma, kwa kuwa walikuwa wakiishi
katika nyumba hizo.
Hali hiyo ilisababisha viongozi
mbalimbali wakiwamo mawaziri, majaji, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya,
wakurugenzi wa ngazi mbalimbali na viongozi wengine kukaa hotelini na
kuisababishia Serikali gharama kubwa.
Tatizo lingine lililoibuka ni kuwa
baadhi ya nyumba zilizouzwa zilikuwa ndani ya maeneo ya jeshi na hasa
Polisi, hivyo kuilazimisha Serikali ya awamu ya nne ilipoingia
madarakani kulazimisha kurejesha baadhi ya nyumba hizo.
Hata hivyo, kulikuwa na ugumu katika
urejeshaji kwani baadhi ya waliouziwa tayari walikuwa wamezibomoa na
kuanza upya ujenzi wake na wengine walikuwa tayari wamezipangisha kwa
mabalozi, kampuni binafsi, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs) na
nyingine kujengewa maduka ya biashar
No comments:
Post a Comment