TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Tuesday, October 22, 2013

WIZARA, HESLB ‘KUJIKAMUA ’MIKOPO

kamati_a3371.jpg
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), zitawapa mikopo wanafunzi 1,107 kutoka katika bajeti zao, baada ya wanafunzi hao kulalamika kukosa mikopo.
Bodi kuanzia leo, itawaita wanafunzi hao wanaochukua masomo ya vipaumbele yakiwamo ya Hisabati na Sayansi, ili kujaza fomu upya.
Hata hivyo kuna wanafunzi wengine waliokosa mikopo kutokana na kushindwa kujaza fomu za kuomba, lakini masomo yao si ya kipaumbele na hivyo kuachwa katika uamuzi huo.
Takriban wiki mbili zilizopita, zaidi ya wanafunzi 100 waliochaguliwa kujiunga katika vyuo vikuu mbalimbali nchini kwa mwaka huu, waliandamana kwenda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwa lengo la kukutana na waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, Dk Shukuru Kawambwa, baada ya kukosa mikopo.(P.T)
Wanafunzi hao walisema wamenyimwa mikopo bila kupewa maelezo ya msingi licha ya kuilalamikia bodi ya mikopo.
Uamuzi huo wa jana, umekuja baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, kuzibana wizara na bodi, ikitaka kujua kilichosababisha wanafunzi hao kukosa mikopo.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema jana kuwa baada ya kutafakari suala hilo, uamuzi umefikiwa kuwa wanafunzi hao waitwe kujaza tena fomu za kuomba mikopo.
" Kilichoamuliwa ni kwamba wizara na bodi zitatakiwa kutafuta fedha kwenye matumizi mengine, ili kuwapa mikopo wanafunzi hawa," alisema.
Naibu Waziri huyo alisema, "Bodi itatakiwa kutafuta fedha hizi kutoka kwenye matumizi mengine (OC), itabidi wajinyime wasisafiri na kuachana na matumizi yasiyo ya lazima. Pia watumie fedha za marejesho ya mikopo kugharimia wanafunzi hawa," alisema Mulugo.
Wanafunzi watakaofaidika na idadi yao kwenye mabano ni wale wanaochukua masomo ya ualimu wa hisabati (20), ualimu sayansi (164), udaktari tiba (111) na uhandisi umwagiliaji (7).
Wengine ni ualimu (617), sayansi kilimo (20), uhandisi (70) na sayansi ya jamii (98).
Mulugo alisema jumla ya Sh3.1 bilioni zinahitajika kuwalipia wanafunzi hao na kwamba bodi itatoa Sh 2 bilioni na wizara yake itatoa Sh1.1 bilioni.
Alisema kiasi hicho cha fedha kitakuwa kwa ajili ya chakula na malazi, vitabu viandishi na mafunzo kwa vitendo na mahitaji maalumu ya vitivo.
Mulugo alisema fedha kwa ajili ya ada za wanafunzi hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, atawaandikia wakuu wa vyuo wanakokwenda kuomba kuwa Serikali itawalipa kwenye bajeti ya mwakani katika bajeti ya 2014/15.

No comments:

Post a Comment