CCECC YA CHINA YAONYESHA NIA KUJENGA RELI YA KATI
KAMPUNI ya ujenzi na uhandisi wa
majengo ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC)
imesema iko tayari kuja Tanzania na kujenga upya reli ya kati ili iwe ya
kisasa zaidi endapo wataombwa wafanye hivyo. (HM)
Hayo yamesemwa jana jioni (Ijumaa, Oktoba 18, 2013) na Rais wa CCECC, Bw. Yuan Li alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jijini Beijing, China. Waziri Mkuu jana alikuwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo.
Akizungumza na Bw. Li pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Tanzania alioambatana nao, Waziri Mkuu alimweleza Bw. Li kwamba hivi sasa reli hiyo imechakaa hali inayofanya mizigo mingi kutoka bandarini isafirishwe kwa barabara na hivyo kuongeza gharama kwa wasafirishaji.
Alisema hali hiyo inachangia mzigo kwa Serikali kwani kumekuwa na uharibifu mkubwa wa barabara kutokana na uzito wa magari yanayobeba mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi nchi jirani kwa sababu wanaitegemea sana bandari hiyo kwa kupokelea mizigo.
Alipoulizwa ni uzito kiasi gani unaruhusiwa kwenye barabara za nchini China, Bw. Li alijibu ni tani 25 (axle load) hali iliyomshtua Waziri Mkuu ambaye alilazimiak kumweleza mgeni wake kwamba barabara za Tanzania haziwezi kudumu kwa miaka mingi kwani hivi sasa zinaruhusu magari yenye uzito wa tani 56 kupita kwenye barabara zake.
Alisema kutokuwepo kwa usafiri madhubuti wa reli imekuwa ni kikwazo kikubwa cha usafiri kati ya Dar es Salaam na Kigoma na Tabora hadi Mwanza lakni pia kutoka Tabora hadi Mpanda. "Kukamilika kwa reli hii ambayo ni uti wa mgongo wa Taifa letu, kutasaidia hapo baadaye kufungua milango na Burundi, Rwanda na DRC lakini pia tutaweza kupeleka mizigo hadi Uganda kwa kupitia Mwanza," alifafanua.
Kwa upande wake, Bw. Li alimweleza Waziri Mkuu kuwa tayari wameanza mazungumzo na Wizara ya Uchukuzi na iwapo watafikia muafaka wako tayari kuja kuijenga reli hiyo.
Akitoa mfano wa zoezi kama hilo, Bw. Li alisema kutokana na mkopo wa benki ya Exim ya China, Septemba mwaka huu, wameanza ujenzi wa reli kati ya Djibouti na Sudan Kusini pamoja na reli nyingine ya kuunganisha Djibouti na Ethiopia ambapo zote mbili zinatarajiwa kukamilika baada ya miaka miwili.
"Hatuwezi kufumua reli yote kwa mara moja. Ninachoona hapa, ujenzi wake itabidi uende kwa awamu kwa sababu una gharama kubwa lakini kwa kuanzia tunaweza kuanza Dar es Salaam hadi Morogoro, awamu ya pili tukatoka Morogoro hadi Dodoma na kuendelea ili usafiri wa treni uwe ukiendelea wakati ujenzi wa reli nao ukiendelea," alishauri.
Kampuni ya CCECC ndiyo iliyojenga reli ya Tanzania hadi Zambia (TAZARA) yenye urefu wa kilometa 1,860 na madaraja 320. Ujenzi wake ulianza mwaka 1970 na kukamilika mwaka 1976.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, (OWM) Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa Zanzibar, Bw. Abdallah Jihad Hassan; Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Juma Maalim na Naibu Waziri wa Fedha, Bibi Saada Salum Mkuya.
Pia amefuatana na Balozi wa China, Luteni Jenerali (Mst.) Abdulrahaman Shimbo, Wakuu wa mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Simiyu; wabunge wawili, Bw. Godfrey Zambi (Mbozi) na Dk. Titus Kamani (Busega) na viongozi wakuu wa Tanzania Private Sector Foundation, Bw. Reginald Mengi, Bw. Salum Shamte na Bw. Godfery Simbeye.
No comments:
Post a Comment