PINTO AAHIDI KUBORESHA SOKA TANZANIA AKICHAGULIWA TFF
MWENYEKITI wa Chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA), Juma Abbas Pinto ametoa taarifa kwa
vyombo vya Habarii juu ya sababu za kuwania kwake Ujumbe wa Kamati ya
Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hii hapa; (HM)
"Ndugu waandishi nagombea nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji katikauchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Kanda ya Pwani na Morogoro na nimeamua kugombea nafasi hiyo ili kuleta mabadiliko ya kweli na kuleta fikra endelevu.
Naamini kabisa nikichaguliwa katika nafasi hiyo kwa kushirikiana na viongozi wenzangu tutaleta mafanikio zaidi na hususani kupokea kijiti kwa viongozi wenzetu waliotangulia ambao wameweka mfumo mzuri wa utawala bora ndani ya shirikisho.
Ili mafanikio yaweze kupatikane ni lazima tuweke mpango endelevu kwa kuwekeza zaidi katika soka la vijana, kuandaa kozi ,warsha na makongamano yatakayotupa dira nzuri ya kukuza na kuwaendeleza vijana na mchezo wenyewe wa soka.
Kikubwa ambacho nitahakikisha ntalisimia kidedea ni kuendeleza vipaji vya wachezaji chipukizi, kuandaa makocha, waamuzi chipukizi na upatikanaji wa vifaa vya michezo ikiwemo kuhakikisha viwanja vya michezo havitumiki kwa matumizi mengine na hivi vilivyopo viweze kuboreshwa zaidi.
Lingine ni kuhakikisha mikoa yote nchini inapata haki sawa katika kugawiwa rasilimali zinazopatikana kutoka kwa wadhamini na Shirikisho la kandanda duniani (FIFA) na kuhakikisha mfumo wa kutumia tiketi za elektroniki unaanza kutumika mara moja.
Mfumo huo utasaidia kumaliza tuhuma za ubadhirifu wa mapato ya milangoni katika mechi mbalimbali zinazofanyika nchini katika viwanja mbalimbali.Zinapopatikana pesa kwa wingi ndio tutakapoweza kutumia fursa hiyo kufanya maendeleo ya mpira wa miguu.
Nafahamu majukumu mazito ambayo yanatakiwa kutekelezwa na kamati ya utendaji na nikiwa kama mjumbe nafahamu nchi yetu ambayo imekuwa ikikumbwa na changamoto mbalimbali katika uendelezaji wa michezo hasa mchezo wa soka.
Kwa miaka 13 iliyokaa Uingereza niliweza kupata nafasi ya kufanya kazi (Part time) pale BBC Swahili kwa kweli niliweza kupata ufahamu wa hali ya juu sana kuhusu mpira wa miguu na kufanya utafiti wa kina katika michezo ikiwa ni pamoja na wachezaji wake, viwanja, kanuni na mbinu mbalimbali.
Lakini mwaka 1999 niliweza kupata semina ya siku 45 nchini Brazili juu ya uongozi wa mpira wa miguu (Football Administration), hatua ambayo ilinipata weledi mkubwa sana katika uongozi wa mchezo wa mpira wa miguu.
Nina uhakika kwa hayo yote niliyoyapata kabla na baada ya kuondoka nchini, yameweza kunipa mwanga sahihi wapi tunapotakiwa kwenda, lakini pia kupata fursa ya kuweza kutumia uzoefu wangu na hiki nilichokipata kuweza kutumia ndani ya TFF.
Hivyo nimeamua kuingia TFF ili kutumia uzoefu wangu katika kuleta mabadiliko ya kweli, pamoja na kuwa mchezaji wa timu ya Pan African mwaka 1993, pia na mchezaji wa timu ya Taifa ya Vijana mwaka 1994.
Lakini kwa hivi sasa ni mjumbe wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Chama Cha soka mkoa wa Pwani, Mjumbe wa kamati ya masoko ya TFF na Mwenyekiti wa Chaa Cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA)." Chanzo: Dina Ismail
No comments:
Post a Comment