SAINI ZAKUSANYWA KUMNG'OA MAKINDA

Spika wa 
Bunge, Anne Makinda (kulia) akizungumza na Mbunge wa Viti Maalumu, Clara
 Mwatuka na Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msola katika Viwanja vya 
Bunge, mjini Dodoma jana.PICHA NA EDWIN MJWAHUZI
Mbunge wa Nzega, Dk Khamis 
Kigwangalla, (CCM), leo anatarajiwa kuanza kukusanya saini za wabunge 
akitafuta kuungwa mkono katika hoja ya kutokuwa na imani na Spika wa 
Bunge, Anne Makinda kwa madai kwamba amekuwa akikiuka kanuni za Bunge.
Dk Kigwangalla aliibua hoja ya 
kutokuwa na imani na Spika katika kikao cha wabunge wote cha kuelezea 
shughuli zitakazofanywa na Bunge katika mkutano wa 13, kilichofanyika 
juzi jioni kwenye ukumbi wa Pius Msekwa.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti 
wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, jana 
alithibitisha kuwapo kwa mjadala huo katika kikao cha wabunge, lakini 
hakuwa tayari kueleza kwa undani na badala yake alisema kwamba leo 
ataanza kukusanya saini za wabunge kwa ajili ya kukamilisha hoja ya 
kutokuwa na imani na Spika Makinda.
Chanzo chetu kutoka katika kikao hicho
 cha wabunge kilibainisha kuwa Kigwangalla alihoji kuhusiana na 
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge (CCM-Bariadi 
Magharibi) kuteuliwa na Spika wakati katika kamati nyingine wenyeviti na
 makamu huchaguliwa na wajumbe wa kamati husika.(P.T)
Pia Dk Kigwangala alisema Spika 
Makinda alivunja kanuni kwa kuwapa posho ya Sh430,000 kwa siku wajumbe 
wa kamati inayoongozwa na Chenge wakati wajumbe wa kamati nyingine 
wamekuwa wakipewa Sh130,000.
"Anachokifanya Spika ni matumizi 
mabaya ya fedha za umma, inakuwaje wengine wafanye kazi hata bila posho 
lakini wao (Kamati ya Bajeti), walipwe posho ya Sh430,000 kwa siku?" 
chanzo hicho kilimkariri Dk Kigwangalla akihoji. Hata hivyo, Katibu wa 
Bunge, Dk Thomas Kashililah akizungumza na gazeti hili jana alisema 
mazingira ya kamati fulani kupata malipo ya ziada tofauti na viwango vya
 kawaida hutokea pale uongozi wa kamati husika unapoomba kwa Spika.
"Si kweli kwamba Kamati ya Bajeti 
inalipwa fedha za ziada kila wakati, hapana, ni pale tu wanapoomba 
malipo hayo kutokana na sababu ambazo lazima Spika aridhike nazo. 
Ieleweke kuwa siyo kamati hiyo tu, kwa sasa Kamati ya Katiba, Sheria na 
Utawala ambayo inachambua miswada mingi nayo imekuwa ikiomba na baada ya
 Spika kuridhia basi nao wanapewa," alisema Dk Kashililah.
Katibu huyo wa Bunge alieleza kuwa 
zaidi ya kamati nane zimewahi kuomba malipo ya ziada kwa maana ya kutaka
 posho zaidi, ulinzi, usafiri na hata chakula, ikiwa zinakabiliwa na 
majukumu ya ziada pia katika mazingira tofauti nje ya utaratibu wa 
kawaida.
"Kimsingi, kamati nyingi zinapewa 
malipo tofauti, watu wanaweza kuwa na kazi mpaka saa saba au nane usiku,
 au wanakwenda kufanya kazi katika mazingira yasiyokuwa ya kawaida, 
taratibu zinamruhusu Spika kama akiridhika na maelezo ya kazi husika, 
basi anaruhusu kutekelezwa kwa maombi hayo," alisema Dk Kashililah.
Kuhusu Serukamba
Aidha, Dk Kigwangalla alinukuliwa 
akisema Spika amekiuka kanuni kwa kumchagua Mwenyekiti wa Kamati ya 
Miundombinu, Peter Serukamba (Kigoma Mjini-CCM), kuwa mjumbe wa Kamati 
ya Bunge ya Bajeti.
"Hakuna mbunge yeyote aliyepo katika 
kamati mbili lakini hata kungekuwa na sababu maalumu basi wa kuteuliwa 
angekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, 
Mahmoud Mgimwa (Mufindi Kaskazini-CCM) ambaye TRA (Mamlaka ya Mapato 
Nchini) ipo chini ya kamati yake," kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema Dk Kigwangalla 
alisema badala ya kumweka karibu katika ushiriki, Mgimwa alipokwenda 
katika kamati hiyo aliambulia kufukuzwa.
Akizungumzia suala hilo, Dk Kashililah
 alisema Serukamba pamoja na wabunge wengine kadhaa waliteuliwa na Spika
 kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kamati hiyo wakati wa kipindi cha 
Bajeti Kuu ya Serikali.
Aliwataja wabunge wengine walioteuliwa
 kushiriki katika Kamati ya Bunge ya Bajeti kuwa ni John Cheyo (Bariadi 
Mashariki-UDP), Salahe Pamba (Pangani - CCM) na Hamadi Rashid Mohamed 
(Wawi - CUF).
Kanuni za Bunge
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge katika 
toleo la mwaka 2007, kifungu cha 137(1), ili kumwondoa Spika madarakani,
 mbunge anayetaka kuwasilisha hoja hiyo atatakiwa kuwasilisha taarifa ya
 maandishi ya kusudio hilo kwa Katibu, akieleza sababu kamili ya kutaka 
kuleta hoja hiyo.
Kifungu kidogo cha pili kinasema baada
 ya kupokea taarifa ya maandishi ya kusudio la kumwondoa Spika kwenye 
madaraka, Katibu atapeleka taarifa hiyo kwenye Kamati ya Haki, Maadili 
na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kujadiliwa.
Kifungu cha tatu kinabainisha kuwa 
endapo kamati hiyo itaridhika kuwa zipo tuhuma mahususi dhidi ya Spika 
zinazohusu uvunjaji wa masharti ya ibara husika za Katiba, sheria au 
kanuni zinazoongoza shughuli za Bunge, basi kamati hiyo itaidhinisha 
hoja hiyo ipelekwe bungeni ili iamuliwe.
Kanuni zinasema Naibu Spika, atakalia 
Kiti cha Spika wakati wa kujadili hoja ya kutaka kumwondoa Spika 
madarakani na Spika atakuwa na haki ya kujitetea wakati wa mjadala na 
kwamba ili kumwondoa zinahitajika kura zisizopungua theluthi mbili ya 
idadi ya wabunge wote
No comments:
Post a Comment