TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Monday, October 21, 2013

MSAIDIZI WA DK. KIKWETE ATUMIKA KUTAPELI BUTIAMA

Jakaya-Mrisho-Kikwete_dc369.jpg
NA MASHAKA MGETA
  • Vijana wachangishwa mamilioni kujiunga jeshi bandia
  • Walipigishwa kwata, wakakimbizwa mchakamchaka kijijini
  • DC afunguka, asema askari mstaafu wa JWTZ anahusika
Siku za hivi karibuni, kumekuwapo na utapeli unaofanywa na baadhi ya watu, miongoni mwao wakitajwa kuwa miongoni mwa ama washirika wa 'vigogo' serikalini wanakusanya fedha kwa njia haramu ili kutoa ajira kwa vijana.
Hali hiyo imejitokeza hivi karibuni wilayani Butiama, na kuthibitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Angelina Mabula.
Vyanzo kadhaa vya taarifa vimelidokeza NIPASHE Jumapili kuwa katika tukio hilo, Afisa mstaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Dickson Malemo, anatajwa kuwa mhusika wa utapeli huo. Malemo anadaiwa kuutangazia umma kwa njia zisizo rasmi, kuwa ametumwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Jumanne Sagini, aorodheshe majina ya vijana wanaotaka kujiunga kwenye majeshi ya ulinzi na usalama.(P.T)
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Afisa huyo, aliifanya kazi hiyo pasipo kificho, akisema Sagini, ambaye anatokea kitongoji cha Nyamimisye wilayani humo, amepata nafasi 21 za vijana kujiunga kwenye majeshi hayo.
Hata hivyo, nafasi hizo hazikupaswa kutolewa 'mfano wa sadaka', bali mhitaji alitakiwa kuchangia fedha kuanzia Sh. 500,000 hadi zaidi ya Shilingi milioni moja ili kupata nafasi hizo.
"Tulitangaziwa kwamba kuna nafasi za ajira majeshini na watu waliokuwa na uwezo walitoa fedha ili vijana wao waingizwe," kilieleza chanzo kimoja katika kitongoji cha Nyamimisye.
Kutokana na 'kiu ya ajira' inayowakabili vijana, baadhi ya wazazi, ndugu na jamaa wenye asili ya nje ya wilaya hiyo na mkoa wa Mara, waliwasiliana na ndugu zao na kuwaleta Butiama ili waorodheshwe.
Mbali na Malemo, mtuhumiwa mwingine anatajwa kuwa ni Bwana Miti aliyetambulika kwa jina moja la Chikonya wakati wengine wawili majina yao hayakujulikama mara moja.
IDADI ILIPOTIMIA
Taarifa zinaeleza kuwa, idadi ya vijana takribani 21 ilipotimia, huku Afisa huyo na wenzake wanaokadiriwa kuwa wanne, walifungua kambi hewa kijijini Butiama, na kutoa mafunzo ya awali kwa vijana waliojiandikisha.
Vijana hao wanadaiwa kuwekwa kwenye nyumba kadhaa zilizopo kijijini humo na nyakati za asubuhi, walikimbizwa mchakamchaka hadi barabara kuu inayokwenda na kutoka Mwanza, eneo la Nyamimisye.
"Tuliwaona vijana wakikimbia mchakamchaka na waliporejea Butiama, tukaambiwa walikuwa wanapigishwa kwata, walionekana kufurahia ajira kabla ya kuajiriwa," kilieleza chanzo kingine.
Ingawa ni hivyo, NIPASHE Jumapili ilifanikiwa kuwapata baadhi ya vijana wanaotajwa kukabiliwa na kadhia hiyo, lakini hawakuwa tayari kutajwa ama kunukuliwa gazetini.
"Tumeambiwa suala hili ni la hatari sana kwa maisha yetu hasa kwa atakayebainika kuzungumzia mambo yalivyotutokea," alikaririwa mmoja wa vijana hao akisema.
SIRI ILIVYOFICHUKA
Kufichuka kwa kashfa hiyo kulitokea moja ya Jumapili zilizopita, baada ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mabula, kumpa 'lifti' mmoja wa wazazi waliochangia fedha kwa ajili ya 'ajira hewa' hizo.
Wawili hao walikuwa wakitokea kusali kwenye Kanisa Katoliki, parokia ya Kiabakari wilayani.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, mzazi huyo alimuuliza Mkuu wa wilaya kuhusu mipango ya safari ya vijana hao, kwa vile wahusika walitangaza kuwa vijana hao wangesafirishwa na kiongozi huyo.
Kuhoji kwa mzazi huyo, kunatajwa kufungua njia ya kufichuka kwa kashfa hiyo ambapo Mabula, alichukua hatua ya kufuatilia na kufanikisha kukamatwa watuhumiwa wanne.
MKUU WA WILAYA 'AFUNGUKA'
Akithibitisha kuwapo kwa tukio hilo, Mabula, aliliambia gazeti hili kuwa Sajini (Katibu Mkuu-Tamisemi), alihusishwa kwa kutajwa na kwamba hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa alikuwa sehemu ya mpango huo.
"Jina la huyu Sagini limetumiwa na watu kwa nia ovu lakini si kwamba amehusika, lakini mpaka sasa tumeshawakamata watuhumiwa wanne na mmoja anatafutwa," alisema.
Mabula, alisema kutumiwa kwa jina hilo kunatokana na jinsi kiongozi huyo, akiwa mwenyeji wa wilayani humo, anavyofahamika.
"Inaonekana watuhumiwa walitumia jina hilo kutaka kuaminiwa kirahisi ili wafanikishwe uovu wao," alisema Mabula.
Kwa mujibu wa Mabula, uchunguzi wa awali ulithibitisha kuwa kila kijana, alitozwa kuanzia Shilingi 500,000 hadi zaidi ya milioni moja.
FAILI LAFIKISHWA KWA MWANASHERIA WA SERIKALI
Hata hivyo, Mabula, aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu jana, kuwa faili lenye tuhuma hizo limefikishwa kwa Mwanasheria wa serikali, ili kuchukua hatua zinazostahili.
"Nimeambiwa na wasaidizi wangu kwamba faili lipo kwa Mwanasheria wa serikali na wakati wowote watafikishwa mahakamani," alisema.
SAGINI ATOA TAMKO ZITO
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka mjini Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Juma Sagini alikiri kupata taarifa hizo, ambapo alitaka watu wote waliohusika na utapeli huo wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Alisema yeye kama mtendaji wa serikali mwenye wajibu wa kusukuma maendeleo ya Watanzania, hawezi kufanya jambo hilo ambalo misingi yake ni kutapeli wananchi na kuchukua kidogo walichochuma kwa jasho lao.
Sajini alisema alitaka wananchi wa Butiama kutokubali kutoa pesa kwa jambo lolote linalohusu kupata ajira za serikalini kwani wakati wa kufanya hivyo taratibu zote za kuajiri zinawekwa wazi na hazihitaji kutoa rushwa.
"Niweke wazi kwamba walioibiwa pesa ni wananchi wa kijiji nilipozaliwa, nimeumizwa sana siwezi kuwakandamiza ndugu zangu hata kidogo, nataka watu hao waeleze nia yao ilikuwa nini," alisema Sagini kwa masikitiko.
Alisema anaamini hana maadui wa kisiasa kwa sababu hana ndoto ya kugombea ubunge, bali watu hao ni sehemu ya 'mtandao' uliosambaa nchini wanaotumia majina ya viongozi kujipatia pesa.
"Nashukuru DC ameniambia tayari baadhi wamekamatwa, wabanwe waseme kwa nini walifanya jambo hilo," aliongeza kusema.
BAADHI YA MATUKIO YA UTAPELI WA AJIRA
Januari 11, mwaka huu, vijana zaidi ya 160 walitapeliwa fedha na madalali 'wanaouza' ajira katika ofisi nyeti za serikali hasa zinazohusu ulinzi na usalama.
Matapeli hao wamekuwa wakiuza ajira za Idara ya Usalama wa Taifa, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Julai 13, mwaka huu, polisi mkoani Dodoma iliwashikilia watu wawili waliokuwa wakitapeli wananchi kwa kutoa vipeperushi vinavyoonesha nafasi za kazi mbalimbali za ajira kutoka kwa kampuni inayojulikana kama Granton Market Dubai (BJM).
Zaidi ya watu 300 mkoani Dodoma na mikoa mingine wanadaiwa kutapeliwa katika sakata la mlolongo wa kuahidiwa ajira; huku mmoja wao akitapeliwa Sh 400,000.
*Taarifa hii imeandaliwa na Mashaka Mgeta na Moshi Lusonzo
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment