TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Saturday, October 19, 2013

WAMA YAAHIDI KUTOA VITANDA VYA KUJIFUNGULIA WAJAWAZITO NJOMBE 

wama f64e6
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipokea ua kutoka kwa Binti Witness Mwalongo anayesoma Kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari ya Mpechi iliyopo Mjini Njombe mara tu baada ya kuwasili Rest House mjini hapo tarehe 17.10.2013. Mama Salma yupo Mkoani Njombe akifuatana na Rais Kikwete aliye katika ziara ya kuutembelea mkoa wa Njombe kuanzia tarehe 17.10 hadi 23.10.2013. Chanzo: John Lukuwi (HM)


Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) imeahidi kukipatia kituo cha afya Lupembe na Hospitali ya Makambako iliyopo wilayani Njombe vitanda vya kujifungulia kina mama wajawazito viwili ili kupunguza tatizo la vifo vyao na watoto wachanga vinavyotokea wakati wa kujifungua.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi hiyo alitoa ahadi hiyo jana mara baada ya kupokea ombi la Mbunge wa jimbo la Njombe Kaskazini Deo Sanga kwa taasisi ya WAMA ili iweze kuwasaidia kina mama wanaopata huduma katika hospitali hizo vitanda viwili vya kujifungulia.
Akiongea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Wanginyi kata ya Lupembe wilaya ya Njombe katika mkoa mpya wa Njombe Mama Kikwete alisema jitihada za pamoja zinahitajika ili kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto wachanga vinavyotokea wakati wa kujifungua vinapungua hapa nchini.
"Nimekubali ombi la Mbunge wenu na ninawaahidi nitawapatia vitanda viwili vya kujifungulia kina mama wajawazito kama alivyoniomba, mimi ninataka kina mama hawa wajifungue katika mazingira salama ili vifo vyao na vya watoto wachanga vipungue", alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema takwimu zinaonyesha kuwa miaka mitatu iliyopita tatizo la vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano lilikuwa juu kwani walikuwa wanakufa watoto 578 kwa kila vizazi hai 100000 lakini hivi sasa tatizo limepungua na kufikia vifo 454 kwa kila vizazi hai 100000
hii ni kuonyesha kuwa uongozi wa Serikali ya awamu ya nne unafanya kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa tatizo hili linapungua.

Mama Kikwete pia aliwataka wakazi wa mkoa huo kujikinga na ugonjwa wa Ukimwi kwani maambukizi yako juu kwa asilimia 14.8 ukilinganisha na maambukizi ya kitaifa ambayo ni asilimia 5.1 na kusisitiza kuwa hali hiyo haikubaliki hivyo basi kila mtu achukue hatua kwani Tanzania bila Ukimwi inawezekana.
Taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika mkoa huo inaonyesha kuna jumla ya Hospitali 11, vituo vya afya 21 na zahanati 190 zinazomilikiwa na Serikali, Taasisi za dini na watu binafsi huku idadi ya wakazi ikiwa ni 702,097 kati ya hao wanaume ni 329,359 na wanawake ni 372,728.
Mama Kikwete ameambatana na mmewe Rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete katika ziara ya kikazi ya siku saba mkoani humo ambapo jana Rais Kikwete amezindua mkoa mpya wa Njombe, amezindua kiwanda cha chai cha Ikanga na kuongea na wananchi wa wilaya ya Njombe. Chanzo: Anna Nkinda, Maelezo

No comments:

Post a Comment