Mifuko ya hifadhi ya jamii kuwanufaisha wananchi wasio katika sekta rasmi
Mkuu wa
Kitengo cha Mawasiliano na Uhamasishaji toka Mamlaka ya Usimamizi na
Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii Bi. Sarah Kibonde (Kulia)
akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu utaratibu mpya
unaowawezesha wananchi wasio katika sekta rasmi kujiunga na mifuko ya
hifadhi ya jamii,wakati wa Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Idara ya
Habari(MAELEZO) leo Jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Afisa Habari wa
Idara ya Habari(MAELEZO) Hassan Silayo.
Picha na Frank Mvungi - MAELEZO (P.T)
TAARIFA KWA UMMA
HIFADHI YA JAMII NI HAKI YAKO
1. UTANGULIZIHifadhi ya Jamii ni haki ya kila Mtanzania . Haki hii imeanishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 11(1) na Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003
2. HIFADHI YA JAMII KWA SEKTA ISIYO RASMI
Mamlaka ya Usimamizi na udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) Iinawafahamisha Wananchi wote kuwa hifadhi ya Jamii ni haki ya kila mtu na si kwa wale tu walio katika ajira rasmi. Kulingana na takwimu zilizotolewa mwaka 2012 idadi ya Watanzania ni milioni 44.9 ambao kati yao watu milioni 1.7 tu ndio waliojiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii,hii ikiwa ni asilimia 6.5 tu ya Nguvu kazi yote ya watu milioni 23.7.
Hivyo Mamlaka inasisitiza Wanachi wote wenye umri wa kufanyakazi,miaka (18-60) walio ajiriwa katika sekta iliyo rasmi au sekta isiyo rasmi(waliojiajiri) kama vile Wakulima,wafanyabiashara ndogondogo,wasusi,vinyozi,mamalishe,mafundi cherehani n.k kuwa wote wanahaki ya kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika mpango wa lazima au mpango wa hiari,kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii ifuatayo.PSPF (PSS), VSRS (GEPF), PPF (DAS), LAPF (LAPF DC Scheme) na NSSF.
3. UHURU WA MWANACHAMA KUJIUNGA NA MFUKO AUPENDAO
Kwa mujibu wa kufungu cha 30 cha Sheria ya Mamlaka,mfanyakazi ambae ameajiriwa na hajawahi kujiunga na mfuko wowote wa Hifadhi ya Jamii katika mfumo wa lazima ama wa pensheni anao uhuru wa kuchagua mfuko wowote kati ya mifuko tajwa hapo juu.
Hii inamaana kwamba mfanyakazi anapaswa kuwa mwanachama wa mfuko mmoja tu katika mpango wa lazima, lakini ana haki ya kujiunga na mpango wa hiari zaidi ya mmoja.
4. MAELEKEZO YA MAMLAKA KWA WAAJIRI, MIFUKO, WANACHAMA NA VYOMBO MBALI MBALI VINAVYOHUSIKA NA ZOEZI LA UANDIKISHAJI WANACHAMA WAPYA
1. Waajiri wote katika utumishi wa umma na sekta binafsi wanapaswa kuzingatia matakwa ya sheria kwa kuwapa fursa watumishi wapya kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ya lazima wanayoitaka. Uhuru wa mfanyakazi uheshimiwe.
2. Waajiri wote wa sekta ya umma na sekta binafsi wanapaswa kuipa Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii fursa sawa ya kuandikisha wafanyakazi wapya kuwa Wanachama wa Mifuko hiyo bila vikwazo vyovyote.
3. Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii izingatie matakwa ya Sheria ya Mamlaka wakati wa kuandikisha wanachama wapya.
Imetolewa na;
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii
S.L.P 31846
Tel:+255 222761683/8
Tovuti: www.ssra.go.tz
Dar-Es-Salaam
Tanzania.
No comments:
Post a Comment