HOTUBA YA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 4 OKTOBA, 2013
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WANANCHI, TAREHE 4 OKTOBA, 2013
Ndugu Wananchi;
Namshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa
rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza mwezi Septemba
salama na kuwasiliana kwa kutumia utaratibu wetu huu mzuri. Naomba radhi
kuzungumza nanyi siku ya leo kwa sababu nilikuwa safari na nilirejea
jioni ya tarehe 30 Septemba, 2013. Awali nilifikiria nisiseme, nisubiri
mwisho wa mwezi wa Oktoba. Lakini, baada ya kupata taarifa ya
yaliyojiri, nimeshauriwa na nimekubali angalau niyasemee baadhi ya mambo
huenda itasaidia. Niwieni radhi nisipoyasemea baadhi ya mambo siyo kwa
kuyapuuza, bali kwa kuepuka hotuba kuwa ndefu mno. Nitayatafutia mahali
pengine pa kuyasemea.
Uhusiano na Rwanda
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwezi
wa Julai, nilizungumzia hali ya uhusiano wetu na Rwanda kutokuwa mzuri
na tatizo la ujambazi na wahamiaji haramu katika Mikoa ya Kigoma, Geita
na Kagera. Nafurahi kusema kuwa kwa yote mawili kuna maendeleo ya kutia
moyo.(P.T)
Tarehe 5 Septemba, 2013, nilikutana na
kuzungumza na Mheshimiwa Rais Paul Kagame wa Rwanda mjini Kampala.
Tuliitumia fursa ya ushiriki wetu katika Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu
kuzungumzia uhusiano baina yetu na nchi zetu. Mazungumzo yalikuwa
mazuri na sote tulikubaliana kuwa yaliyopita si ndwele tugange yajayo.
Kwa sababu hiyo tulielewana kuwa tutengeneze mazingira yatakayosaidia
kutuliza hali na kurudisha nchi zetu katika uhusiano mwema kama
ilivyokuwa siku zote. Nawaomba ndugu zangu hususan wanasiasa, watumishi
wa umma, wanahabari na wenye mitandao ya kijamii na blog na wananchi kwa
ujumla tusaidie kuimarisha uhusiano mwema baina ya Rwanda na Tanzania
na watu wake.
Majambazi na Wahamiaji Haramu
Ndugu Wananchi;
Katika hotuba hiyo pia nilisema kuwa
tutachukua hatua thabiti dhidi ya majambazi na wageni wanaoishi nchini
bila ya kuzingatia taratibu zinazohusika. Niliwataka majambazi
wajisalimishe wao na silaha zao kwa hiari. Wale wanaoishi nchini bila ya
kuwa na kibali halali wahalalishe ukaazi wao au warejee makwao. Nilitoa
siku 14 kuanzia tarehe 29 Agosti, 2013 wafanye hivyo kwani baada ya
hapo tungeanzisha operesheni maalum ya kushughulika na watu wa makundi
yote mawili.
Ndugu Wananchi;
Kumekuwepo na mafanikio ya kutia moyo.
Kwa upande wa wahamiaji wanaoishi nchini kinyume cha sheria watu
wapatao 21,254 waliondoka kwa hiari. Hali kadhalika zaidi ya ng'ombe
8,000 waliondolewa na silaha 102 zilisalimishwa. Baada ya operesheni
kuanza tarehe 6 Septemba, 2013 na kumalizika tarehe 20 Septemba, 2013,
wahamiaji haramu 12,828 walirejeshwa makwao na watuhumiwa 279 wa
unyang'anyi wa kutumia silaha walikamatwa. Aidha, mabomu 10 ya kutupa
kwa mkono (offensive hand grenades), silaha 80, risasi 780 na mitambo 2
ya kutengeneza magobole vilikamatwa. Pia, ng'ombe 8,226 walikamatwa
wakichungwa katika mapori ya hifadhi. Kwa upande wa mazao ya misitu,
mbao 2,105 zilikamatwa pamoja na nyara mbalimbali za Serikali.
Ndugu Wananchi;
Agizo la kuwataka watu wanaoishi
nchini isivyo halali wahalalishe ukaazi wao au waondoke kwa hiari au
wataondolewa lilipotoshwa hasa na vyombo vya habari vya nje ya Tanzania.
Walikuwa wanadai eti Tanzania ilikuwa inafukuza wakimbizi. Madai hayo
si ya kweli hata kidogo. Hadi kufikia tarehe 30 Septemba, 2013 wakimbizi
68,711 walikuwepo kwenye Kambi ya Nyarugusu, Mkoani Kigoma. Hakuna
mkimbizi ye yote aliyetakiwa kuondoka. Ukweli ni kwamba hakuna mtu ye
yote kati ya wale watu walioondoka kwa hiari au kusaidiwa kuondoka
wakati wa operesheni ambaye ni mkimbizi. Kama ingekuwa hivyo, wa kwanza
kulalamika wangekuwa wenzetu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa
Mataifa. Bahati nzuri jambo hilo halikutokea.
Ndugu Wananchi;
Yalikuwepo pia madai kwamba tunawaonea
na kuwatesa watu walioishi nchini miaka mingi. Ati iweje sasa ndiyo
waambiwe kuwa siyo raia. Siku zote Serikali ilikuwa wapi? Uraia
haupatikani kwa kuishi nchi ya kigeni kwa miaka mingi. Unapatikana kwa
kutimiza masharti ya kuomba na kupewa uraia. Kama mtu hakufanya hivyo
anabaki kuwa raia wa nchi aliyotoka au walikotoka wazazi wake. Ipo
mifano ya watu mashuhuri ambao walilazimika kuachia nyadhifa zao baada
ya kugundulika kuwa siyo raia. Hawakuwa wanaonewa, ndiyo matakwa ya
Katiba na Sheria za nchi yetu.
Ndugu Wananchi;
Katika kutekeleza operesheni hii
niliagiza kuwa wale watu ambao wameishi hapa nchini miaka mingi ambao
wana nyumba, mashamba au mali mbalimbali au wameoa au kuolewa na wana
watoto au hata wajukuu waelekezwe kuhalalisha ukaazi wao. Iwapo
watakataa kufanya hivyo basi wasaidiwe kurejea kwao. Pia niliagiza watu
wasiporwe mali zao wala kudhulumiwa. Sijapata taarifa ya kufanyika
kinyume na maelekezo yangu. Lakini kama wapo watu waliotendewa tofauti,
taarifa itolewe kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa au hata Ofisi ya Rais ili
hatua zipasazo zichukuliwe. Hatutaki watu wadhulumiwe au kuonewa.
Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza
Waziri wa Ulinzi na JKT, Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha na Waziri wa
Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Emmanuel Nchimbi kwa uongozi wao mzuri katika
zoezi hili. Pia, nawapongeza Makamanda na askari wa JWTZ na Polisi
pamoja na maafisa wa Idara ya Uhamiaji, Idara ya Mifugo, Idara ya
Wanyamapori, Idara ya Misitu na Idara nyinginezo za Serikali kwa kazi
kubwa na nzuri waliyofanya. Najua awamu ya kwanza imeisha tarehe 20
Septemba, 2013 na kama nilivyosema kuwa safari hii operesheni itakuwa
endelevu, muda si mrefu awamu ya pili itafuata. Nawaomba waendelee
kuchapa kazi kwa bidii, maarifa na nidhamu ya hali ya juu.
Ziara ya Canada na Marekani
Ndugu Wananchi;
Kati ya tarehe 17 na 28 Septemba, 2013
nilifanya ziara ya kikazi katika nchi za Canada na Marekani. Nchini
Canada nilitembelea Chuo Kikuu cha Guelph ambapo nilitunukiwa Shahada ya
Heshima ya Uzamivu kwa kutambua jitihada zetu tuzifanyazo kujiletea
maendeleo na mafanikio ya kutia moyo tunayoendelea kupata licha ya
changamoto zinazotukabili. Katika mazungumzo yangu na uongozi wa chuo
hicho wamekubali kuwa na ushirikiano wa karibu na Wizara zinazohusika na
Elimu, Kilimo na Mifugo pamoja na Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine,
Morogoro na Chuo Kikuu cha Dodoma. Nimewataka Mawaziri wa Wizara hizo na
viongozi wa vyuo hivyo kuchangamkia fursa hiyo bila kuchelewa.
Ndugu Wananchi;
Nchini Marekani nilikutana na
kuzungumza na maafisa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya nchi hiyo
wakiwemo Rais Barack Obama na baadhi ya Wabunge wa Bunge la Marekani.
Mazungumzo yetu yalilenga kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zetu na
mambo yalienda vizuri. Wote walituhakikishia kuwa mambo tuliyoyazungumza
na kukubaliana na Rais Barack Obama wakati wa ziara yake nchini
yanaendelea kufanyiwa kazi. Miongoni mwa hayo maombi yetu ya kupatiwa
vitabu milioni 2.4 vya sayansi na hisabati yamekubaliwa na utekelezaji
umeanza. Upatikanaji wa vitabu hivyo utamwezesha kila mwanafunzi wa
sekondari kuwa na kitabu chake.
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine kubwa na la faraja kwetu
ni kuwa mapendekezo yetu ya miradi ya umeme na barabara za vijijini za
kugharamiwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika lao la Changamoto za
Milenia yamepokelewa vizuri. Kinachosubiriwa ni miradi ipi itakubaliwa
na Bodi ya MCC na kiasi gani cha fedha kitatengwa na Bunge la Marekani
kwa ajili hiyo.
Tuzo ya Uhifadhi
Jambo lingine muhimu katika safari
yangu ya Marekani ni kutunukiwa tuzo na "International Congressional
Conservation Foundation" kwa kutambua juhudi zetu katika kuhifadhi
wanyama pori na mafanikio tuliyoyapata. Licha ya changamoto mbalimbali
tunazokabiliana nazo, tuzo hii imetupa moyo wa kuongeza nguvu katika
jitihada tunazozifanya sasa kupambana na ujangili na matatizo mengine ya
uhifadhi wa wanyama na misitu.
Ndugu Wananchi;
Kilichotupa moyo zaidi ni kauli za
utayari wa kutusaidia katika mapambano hayo zilizotolewa wakati wa
kupewa tuzo na katika mkutano wa mfuko wa Maendeleo wa Clinton na katika
mkutano maalum wa kupambana na ujangili na biashara ya meno ya tembo
duniani.
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Ndugu Wananchi;
Shabaha kuu ya safari yangu ya
Marekani ilikuwa kuhudhuria Mkutano wa 68 wa Umoja wa Mataifa
unaoendelea jijini New York mpaka Desemba, 2013. Mada kuu ya mkutano wa
mwaka huu ni kuandaa agenda ya maendeleo baada ya mwaka 2015 yaani: Post
2015 Development Agenda: Setting the Stage. Kama mtakavyokumbuka
Malengo ya Milenia yaliyoamuliwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka
2000, yanafikia ukomo wa utekelezaji wake mwaka 2015.
Katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
mwaka huu mjadala umehusu nini kifanyike baada ya mwaka 2015. Hata
hivyo, mjadala huo unaanza kwa kufanya tathmini ya utekelezaji wa yale
Malengo Manane ya Milenia ya mwaka 2000 umefikia wapi mpaka sasa na
utafikia wapi mwaka 2015 kwa kila nchi na kwa dunia kwa ujumla. Tathmini
ya jumla inaonesha kuwa kumekuwepo na jitihada kubwa ya kutekeleza
malengo haya katika kila nchi. Yapo malengo ambayo utekelezaji wake
umefikia shabaha hivi sasa na yapo ambayo upo uwezekano wa shabaha
kufikiwa ifikapo mwaka 2015. Vile vile yapo ambayo shabaha haitafikiwa.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu, Tanzania, tumefikia shabaha katika mambo yafuatayo:
(1) Lengo la Milenia namba 2 kuhusu uandikishaji wa watoto wenye umri wa kwenda shule ya msingi;
(2) Lengo la Milenia namba 3 hasa
kuhusu usawa wa kijinsia katika Shule za Msingi na Sekondari. Ukweli ni
kwamba, wasichana wanaanza kuwa wengi kuliko wavulana. Hatujafikia
shabaha kwa upande wa usawa wa kijinsia katika elimu ya juu na ni vigumu
kulifikia ifikapo 2015. Pia hatujafikia lengo kwa upande wa usawa wa
Wabunge wanawake na wanaume. Hata hivyo, kwa kutumia mchakato wa Katiba
unaoendelea sasa tunaweza kufikia lengo katika uchaguzi wa 2015 iwapo
tutaamua iwe hivyo;
(3) Lengo la Milenia namba 4 kuhusu kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga na wale wenye umri chini ya miaka mitano;
(4) Tumefikia shabaha kwa Lengo la Milenia Namba 6 kuhusu kupunguza maambukizi ya UKIMWI; na
(5) Kwa upande wa lengo namba 7 kuhusu
mazingira, tumefikia shabaha kwa upande wa upatikanaji wa maji mijini.
Bado tuko nyuma kwa maji vijijini ingawaje tunaweza kufikia lengo
ifikapo mwaka 2015 kama tutaendeleza uwekezaji tulioamua kufanya katika
bajeti ya mwaka huu. Lakini, hatutaweza kufikia shabaha kwa upande wa
usafi wa mazingira mijini na vijijini ifikapo mwaka 2015. Safari bado
ndefu sana.
Ndugu Wananchi;
Malengo ya Milenia namba 1 na namba 5
ambayo bado tuko nyuma sana ya shabaha hatutafikia lengo ifikapo 2015.
Tumeendelea kutekeleza lengo la Milenia namba 1 kuhusu kupunguza
umaskini na njaa kwa zaidi ya nusu kutoka kiwango cha mwaka 2000. Hatua
tunazochukua kuleta mageuzi katika kilimo zina lengo la kuhakikisha
usalama wa chakula na kuongeza mapato ya wakulima. Mafanikio yanaanza
kuonekana lakini si ya kiwango cha kutufikisha kwenye lengo ifikapo
mwaka 2015. Tunao, pia, mpango wa kupanua programu ya TASAF ya
Conditional Cash Transfer ili tuwafikie watu wengi maskini. Hata kama
tutafanikiwa kuutekeleza mapema mpango huu utatusogeza sana mbele lakini
bado tutakuwa chini ya lengo kwa upande wa kupunguza umaskini ifikapo
2015.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa Lengo la Milenia namba
5, kuhusu afya ya kina mama wajawazito bado tuko nyuma katika kupunguza
vifo vya kina mama wajawazito na kuongeza idadi ya wajawazito
wanaojifungua chini ya uangalizi wa wataalamu wa afya. Hatutaweza
kufikia shabaha ifikapo mwaka 2015. Mpango wa Maendeleo ya Afya ya
Msingi (2007 – 2017) una nia ya kukabiliana na matatizo haya. Tumeongeza
ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali, tumeboresha
upatikanaji wa dawa na tumepanua sana mafunzo ya madaktari, wauguzi na
wakunga mambo ambayo yamesaidia kutufikisha hatua tuliyopiga mpaka sasa.
Naamini juhudi zetu tukiziendeleza zitatusogeza mbele zaidi ingawaje
bado tutakuwa chini ya lengo. Miaka michache ijayo, tatizo hili nalo
litakuwa historia.
Ndugu Wananchi;
Lengo la Milenia namba 8 linazihusu
nchi tajiri kuongeza michango yao kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza
Malengo ya Milenia. Bahati mbaya sana mataifa tajiri hayajafikia
viwango wanavyotarajiwa kutoa na hata vile wanavyoahidi wenyewe kutoa
katika majukwaa mbalimbali. Kama wangetimiza ahadi zao, sura ya
utekelezaji wa Malengo ya Milenia ingekuwa tofauti kabisa.
Ndugu Wananchi;
Hiyo ndiyo hali ya utekelezaji wa
Malengo ya Milenia hapa nchini. Hakuna nchi ye yote duniani
iliyofanikiwa kutekeleza shabaha za malengo yote kwa ukamilifu. Ushauri
wa viongozi wote waliozungumza ulitaka mataifa yaliyoendelea yatimize
ahadi zao za kuchangia utekelezaji wa Malengo ya Milenia. Ilionekana
suala la upatikanaji wa fedha halina budi kuangaliwa kwa makini sasa na
baada ya mwaka 2015. Bila ya hivyo ufanisi utakuwa mdogo katika kuongeza
kasi ya utekelezaji kwa pale paliposalia kufikia malengo ya 2015 na
hata kwa Malengo ya baada ya mwaka 2015.
Mashambulizi ya Kigaidi ya Westgate, Nairobi
Ndugu Wananchi;
Wakati nikiwa safarini, tarehe 21
Septemba, 2013 kulitokea shambulilizi la kigaidi katika Jengo la
Biashara la Westgate, huko Nairobi, Kenya. Watu 67 walipoteza maisha na
zaidi ya 200 walijeruhiwa. Nilituma salamu za pole na rambirambi kwa
Mheshimiwa Rais Uhuru Kenyatta na wananchi wa Kenya na kuwahakikishia
kuwa tupo pamoja nao katika wakati huu wa majonzi.
Nafahamu kuwa baada ya tukio hilo watu
wengi hapa nchini wameingiwa na hofu kuhusu usalama wetu. Ni hofu ya
msingi kwani tarehe 8 Agosti, 1998 Ubalozi wa Marekani hapa nchini
ulishambuliwa na magaidi na ndugu zetu 11 wasio na hatia walipoteza
maisha.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwafahamisha kuwa tangu
shambulio la mwaka 1998, Serikali imekuwa inajenga uwezo wa vyombo vyetu
vya ulinzi na usalama kupambana na ugaidi katika nyanja mbalimbali.
Tunaendelea kujiimarisha bila kusita siku hadi siku. JWTZ, Polisi na
Idara ya Usalama wa Taifa wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa ajili
hiyo. Juhudi zetu hizo ndizo zinazotufanya tuwe salama hadi sasa.
Baada ya tukio la Kenya, vyombo vyetu
vya ulinzi na usalama vimeimarisha mikakati yao maradufu. Pamoja na
kujizatiti kwetu huko hatuwezi kusema kuwa tukio la kigaidi halitaweza
kutokea nchini. Uhakika huo hatuna kwani hata mataifa makubwa na tajiri
yameshambuliwa. Kilicho muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari na
wananchi kusaidia ili vyombo vyetu vifanikiwe zaidi.
Hali kadhalika, tumewataka watu wote
wenye shughuli zinazokusanya watu wengi kama vile maduka, maofisi,
mahoteli, migahawa n.k. waweke kamera za ulinzi nje na ndani ya maeneo
yao. Pia waangalie uwezekano wa kuweka vifaa vya upekuzi (metal
detectors and x-rays). Najua watu wanaweza kulalamikia usumbufu au
gharama, lakini gharama na hasara ya kushambuliwa ni kubwa zaidi kuliko
ya usumbufu huo.
Ndugu Wananchi;
Nawaomba muendelee kufanya shughuli
zenu bila ya hofu ingawaje msiache kuwa makini na kuchukua tahadhari.
Watu watoe taarifa kwa vyombo vya usalama wanapoona mtu au watu au kitu
cha kutilia shaka. Ni muhimu kwa usalama wake, wa kila mtu, jamii na
taifa. Maafisa husika wa vyombo vya ulinzi na usalama wataendelea
kuelimisha umma kuhusu hatua mbalimbali za tahadhari za kuchukua. Sisi
Serikalini tumejipanga kuchukua hatua zaidi kuimarisha ulinzi na usalama
wa nchi yetu na watu wake.
Mchakato wa Katiba Mpya
Ndugu Wananchi;
Kama mtakavyokumbuka, Bunge lilitunga
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Novemba, 2011. Sheria hii imeweka
mchakato mzima wa kupata Katiba hiyo na kuunda taasisi zake. Mwezi Mei,
2012, Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa na imekamilisha hatua tatu
muhimu katika mchakato huo. Hatua hizo ni kupokea maoni ya wananchi,
kutayarisha rasimu ya kwanza ya Katiba Mpya na kupokea maoni ya Mabaraza
ya Katiba ya Wilaya na ya taasisi. Hivi sasa Tume inaandaa mapendekezo
ya Rasimu ya Pili ya Katiba itakayopelekwa kwenye Bunge Maalum. Baada ya
tafakuri zake, Bunge Maalum litatoa rasimu ya mwisho ya Katiba ambayo
itapelekwa kwa wananchi kwa ajili ya uamuzi wa mwisho kupitia kura ya
maoni. Baada ya hatua hiyo, ndipo tutakapokuwa tumepata Katiba Mpya.
Ndugu Wananchi;
Baada ya Bunge la Novemba, 2011
kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kulikuwepo na madai ya kutaka
sheria hiyo iboreshwe kutoka vyama vyote vya siasa vikiwemo vyama vya
upinzani na Chama tawala. Majadiliano yalifanyika baina ya Serikali na
vyama hivyo pamoja na shirikisho la asasi za kiraia. Makubaliano
yalifikiwa kuwa marekebisho yafanyike kwa awamu. Awamu ya kwanza
ihusishe Tume ya Mabadiliko ya Katiba kisha hapo yafanyike marekebisho
yanayohusu Bunge Maalum na mwisho Kura ya Maoni.
Kama ilivyokuwa kwa mabadiliko
yaliyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba, safari hii nayo vyama vya siasa
vilitoa mapendekezo yao. Yalifanyika mazungumzo kati yao na Serikali na
maelewano kufikiwa kuhusu maeneo ya kufanyiwa marekebisho. Serikali
ilitayarisha rasimu ya Muswada na kuuwasilisha kwa wenzetu wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Ndugu Wananchi;
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilitoa
mapendekezo yake na ushauri kwenye maeneo mawili. Kwanza kwamba uteuzi
wa wajumbe wa Bunge Maalum ufanywe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa kushauriana na kuafikiana na Rais wa Zanzibar. Pili
walishauri kwamba kama Bunge Maalum litashindwa kufikia maamuzi ndani ya
siku 70 zilizopendekezwa, liweze kuongezwa muda hadi kufikia siku 90.
Maeneo mengine ya Muswada waliafikiana nayo.
Ndugu Wananchi;
Kwa kuzingatia utaratibu wa kutunga
Sheria, Serikali ilifikisha Muswada kwa Spika wa Bunge ambaye nae
aliuwasilisha kwenye Kamati ya Kudumu ya Katiba, Sheria na Utawala. Kama
ilivyo ada, Kamati hiyo ilifanya vikao na wadau na kupokea maoni yao
kuhusu Muswada. Nimeambiwa kulikuwa na mjadala wa kina na mapendekezo
mazuri yalitolewa na wadau. Kisha hapo Wajumbe wa Kamati walikaa wenyewe
kujadili Muswada walikuwepo pia Wabunge ambao si Wajumbe wa Kamati
walioshiriki kwa vile Kanuni zinaruhusu. Nimeambiwa pia kwamba mjadala
ulikuwa mpana na wa kina zaidi. Mapendekezo kadhaa yalitolewa na Wajumbe
kuhusu vifungu mbalimbali vya Muswada.
Ndugu Wananchi;
Nimefahamishwa kuwa Wabunge wa vyama
vyote walichangia na kwamba baadhi ya nyakati mambo yalipokuwa ugumu
mawazo mazuri ya baadhi ya Wabunge wa upinzani yalisaidia kupata
ufumbuzi. Nimeambiwa pia kwamba Wajumbe wa Kamati na upande wa Serikali
walikubaliana kwa maeneo mengi isipokuwa machache ambayo walikubaliana
kwa pamoja wayapeleke Bungeni ili Wabunge nao wayajadili na kuyapatia
ufumbuzi.
Ndugu Wananchi;
Baada ya Kamati kumaliza kazi yake,
Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mathias Chikawe aliwasilisha
Muswada Bungeni. Akafuatiwa na Mheshimiwa Gosbert Blandes kwa niaba ya
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala,
kutoa maoni ya Kamati. Baadaye Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Mheshimiwa
Tundu Lissu alitoa maoni yake.
Ndugu Zangu;
Baada ya watu hao watatu kutoa maoni
yao ilitarajiwa kuwa Wabunge wangeanza kujadili Muswada. Naambiwa mambo
hayakuwa hivyo. Badala yake kukazuka malumbano baina ya Spika na baadhi
ya Wabunge wa Upinzani wakitaka Muswada usijadiliwe. Ilifikia wakati
hoja hiyo ikabidi iamuliwe kwa kura ambapo ilishindwa. Katika hali
isiyotarajiwa, Wabunge wote wa upinzani wakatoka nje ya Bunge isipokuwa
wawili. Kitendo hicho kimewanyima Wabunge wengi wa upinzani fursa ya
kutetea hoja zao walizozitoa kupitia hotuba ya Msemaji wa Kambi ya
Upinzani. Pia wamejinyima nafasi ya kusema mambo mengine wakati wa
mjadala na Kamati ya Bunge zima.
Wabunge waliokuwepo waliendelea
kuujadili Muswada na kutoa hoja na mapendekezo ya kuuboresha. Walifanya
hivyo wakati wa mjadala na wakati wa kupitia kifungu kwa kifungu. Baadhi
ya hoja na mapendekezo yalikubaliwa na mengine yalikataliwa. Miongoni
mwa yaliyokubaliwa na Wabunge, kwa mfano, ni kuhusu elimu ya mtu
atakayekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum na lile la ukomo wa uhai wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Kwa maoni yangu madai ya Kambi ya
Upinzani yanazungumzika na hata baadhi yangeweza kukubalika kama Wabunge
wake wangekuwepo Bungeni na kushiriki mchakato wote wa kujadili na
kupitisha Miswada Bungeni. Bahati mbaya hawakuwepo, hivyo hapakuwepo na
mtu wa kusema mawazo yao. Baada ya kupoteza fursa yao halali, kutaka
kupata ufumbuzi nje ya Bunge ni jambo lisilowezekana. Haya ni masuala
yanayohusu Bunge ambayo hujadiliwa na kuamuliwa Bungeni na si
vinginevyo. Kuandamana nchi nzima au kuchukua hatua za kutotii sheria
kama Mwenyekiti wa CHADEMA, Mheshimiwa Freeman Mbowe anavyotaka,
hakutaleta mabadiliko wanayoyataka katika sheria hii. Naamini na wao
wanautambua ukweli huo.
Ndugu Wananchi;
Kuna msemo wa wahenga kuwa "historia
hujirudia". Naomba hekima ziwaongoze viongozi wa CHADEMA, CUF na
NCCR-Mageuzi na zituongoze sote kutumia utaratibu tulioutumia mwaka
2012. Kulipotokea mazingira kama haya pande zote zilikaa pamoja na
kuzungumzia hoja moja baada ya nyingine na kukubaliana nini kifanyike na
kifanyike vipi. Baada ya kuridhiana hatua zipasazo za kisheria na
kanuni zilichukuliwa na kumaliza mzozo.
Ndugu Wananchi;
Kufanya kinyume cha hayo hakutaleta
ufumbuzi wa mzozo huu. Tutaliingiza taifa kwenye matatizo yasiyokuwa ya
lazima. Tukikataa kufanya hayo Watanzania wanayo kila sababu ya kuhoji
dhamira zetu na kutilia shaka nia zetu. Watakuwa na haki ya kuuliza nia
ni hii yetu sote ya kupata Katiba Mpya kwa kutumia njia za kikatiba na
kisheria au tuna dhamira nyingine iliyojifisha?
Kama dhamira yetu ni kutaka kupata
Katiba mpya kwa mujibu wa Katiba na Sheria, ushauri wangu na rai kwa
ndugu zetu wa CHADEMA, CUF na NCCR-Maguezi ni kuwa waachane na mipango
ya maandamano na kufanya ghasia. Badala yake watumie njia halali
zinazotambulika kikatiba na kisheria kujenga hoja za kufanya marekebisho
wanayoyaona wao yanafaa kuboresha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba. Tukifanya hivyo tutakuwa tunajenga badala ya
kubomoa. Tutaliponya taifa. Sisi katika Serikali tuko tayari.
Ndugu Wananchi;
Napenda pia kuzisemea baadhi ya hoja
zilizotolewa na Kambi ya Upinzani. Kwanza kabisa nasema kuwa
nimesikitishwa sana na madai na tuhuma za uongo eti katika uteuzi wa
Tume ya Katiba sikuheshimu mapendekezo ya TEC, CCT na walemavu.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Siyo tu kauli hiyo ya Mheshimiwa Tundu
Lissu ni uzushi na uongo mtupu bali pia ni ya unafiki, fitina na
uzandiki wa hali ya juu. Nasema hivyo kwa sababu, sipendi kuamini kuwa
Mheshimiwa Mbunge amesema yale kwa kutokufahamu ukweli au kwa bahati
mbaya. Amesema yale kwa makusudi mazima ya kupotosha ukweli ili pengine
isaidie kujenga hoja yake ya kutaka Rais asiteue wale Wajumbe 166 wa
Bunge Maalum.
Napenda ieleweke kuwa siishabikii kazi
hiyo, lakini kwa kutimiza wajibu na maslahi ya taifa nikiagizwa na
Sheria za nchi nitafanya. Nasema hivyo kwa sababu nafahamu ni kazi
ngumu. Kama kazi ya uteuzi wa Wajumbe 30 wa Tume haikuwa rahisi hata
kidogo, hii ya uteuzi wa watu 166 itakuwa ngumu zaidi. Ile ya Tume
ilikuwa ngumu kwa namna mbili. Kwanza, kwamba taasisi zilizoomba na
waombaji walikuwa wengi mno kuliko nafasi za kujaza yaani 15 Zanzibar na
15 Bara. Zanzibar ziliomba taasisi zaidi ya 60 na waombaji walikuwa
zaidi ya 200 wakati Bara kulikuwa na taasisi zaidi ya 170 zikiwa na
waombaji zaidi ya 500. Kupata watu 30 kutoka orodha kubwa kiasi hicho si
mtihani mdogo. Pili kwamba tulitakiwa kuunda Tume inayoasili sura ya
taifa, yaani watu wa nchi yetu kwa maeneo, vyama vya siasa, dini,
wanawake, vijana, walemavu, wafanyakazi, wasomi, Wabunge, Wawakilishi,
wanasheria, wafanyabiashara, wakulima, asasi za kiraia n.k.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na changamoto hizo, lakini
tulifanikiwa kuunda Tume iliyopokelewa vizuri na jamii na kufanya watu
wengi hata wale ambao hawakuteuliwa wahisi kuwakilishwa. Tulifanyaje?
Kwanza kabisa tulihakikisha kuwa tunapata wawakilishi wa vyama vya siasa
vyenye wawakilishi Bungeni na kwenye Baraza la Wawakilishi na tunapata
wawakilishi wa mashirika ya dini zetu kubwa yaani, TEC, CCT na BAKWATA.
Ndiyo maana nikasema kuwa kwa Mheshimiwa Tundu Lisu kudai kuwa
mapendekezo ya TEC na CCT hayakuheshimiwa ni uongo wa mchana usiokuwa na
kichwa wala miguu.
Baada ya hapo ndipo tukaangalia
waombaji wa makundi na taasisi nyingine. Tulijitahidi sana kupata watu
ambao wanawakilisha kundi zaidi ya moja. Tulifikiria hivyo kwa sababu ni
ukweli ulio wazi kuwa si kila taasisi iliyoomba itapata mwakilishi
kwani hata tungependa iwe hivyo nafasi hazikuwepo. Kwa kutumia utaratibu
huu makundi mengi yamepata uwakilishi kutokana na watu waliopendekezwa
na makundi mengi. Tumefanya kazi kubwa sana ya kuwianisha mambo na
makundi ya maslahi mbalimbali nchini.
Ndiyo maana naiona mantiki ya Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishirikiana na Rais wa Zanzibar wa
kuwateua Wajumbe wa Bunge Maalum. Dhana kuwa kila kikundi kiteue
chenyewe watu ingefaa sana kama kungekuwepo na nafasi za kutosha kila
kundi nchini. Hilo haliwezekani, labda tuwe na Bunge Maalum lisilokuwa
na ukomo wa wajumbe.
Ndugu Wananchi;
Mimi na Rais wa Zanzibar tumekuwa
tunajiuliza baada ya kazi ngumu na nzuri tuliyoifanya na iliyopongezwa
na wengi ya kuteua Tume ya Mabadiliko ya Katiba nini kilichoharibika
sasa hata tuonekane hatuaminiki kuteua hawa 166? Kama ni kwa sababu za
Mheshimiwa Tundu Lissu, nimeshasema hazina ukweli wowote. Ninapojiuliza
kwa nini aseme uongo nashindwa kupata jibu linaloingia akilini. Wakati
mwingine nafikiria kuwa ni hiana. Lakini nadhani ni hila za kisiasa
zenye nia ya kutaka kupata watu wa kutetea maslahi ya chama chake. Kama
hiyo ndiyo shabaha basi amekosea sana.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Hatutengenezi Katiba ya Chama fulani
bali Katiba ya nchi, Katiba ya watu wa vyama vyote na wasiokuwa na vyama
ambao ndiyo wengi kuliko wote. Lazima tuongozwe na ukweli huo na tuwe
na msimamo huo wakati wote. Lazima tukumbuke kuwa si watu wote
wanaostahili au kuwa na sifa ambao wataomba na kupata nafasi ya kuwa
Wajumbe, hivyo wale wachache watakao bahatika lazima wawasemee wote.
Wanatakiwa kusikiliza na kuwakilisha mawazo ya wote hata wale wasiokuwa
wa Chama chao au kundi lao.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri hii ndiyo sifa kubwa
iliyooneshwa na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Wamewasimamia
na kuwasemea watu wote bila ya kubagua. Natambua kuwepo kwa baadhi ya
watu ambao hawafurahii msimamo huo na matokeo ya kazi yao. Watu hao
kuwalaumu Wajumbe wa Tume kwa ajili hiyo ni kuwaonea na kutowatendea
haki. Tunataka watakaokuwa Wajumbe wa Bunge Maalum nao waige mfano huu
mzuri. Wajali maslahi mapana ya taifa letu na watu wake badala ya kujali
yale ya taasisi zao au makundi yao.
Zanzibar Kutokushirikishwa
Ndugu Wanachi;
Nimeambiwa pia kuliwepo madai ya
Zanzibar kutokushirikishwa ipasavyo. Nimeeleza kwa kiasi gani Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar imeshirikishwa na kutoa maoni yake yaliyojumuishwa
katika Muswada. Hivyo basi napata tabu kuyaelewa madai kwamba Serikali
ya Mapinduzi Zanzibar haikushirikishwa msingi wake nini! Labda kuna kitu
sikuambiwa!
Nimeulizia kuhusu hoja ya Kamati
kutokufanya vikao Zanzibar kusikiliza maoni ya wadau wa Zanzibar.
Nimeambiwa kuwa Kanuni za Bunge hazina sharti hilo hivyo Kamati
haistahili kulaumiwa. Kama hivyo, nashauri kuwa suala hili lirudishwe
Bungeni ili Wabunge walizungumze na kulifanyia uamuzi muafaka.
Vinginevyo watu wataendelea kulauminiana isivyostahili. Hivyo basi,
kuligeuza jambo hili kuwa ni suala la kukataa Muswada au kususia vikao
vya Bunge au kufanya maandamano sidhani kama ni sawa.
Ndugu Wananchi;
Nimeambiwa pia kuwa kulikuwa na hoja
ya kutaka idadi ya Wajumbe wa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar iwe sawa
kama ilivyo kwenye Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Sababu ya idadi ya
Wajumbe wa Tume kuwa sawa inatokana na utaratibu wao wa kufikia uamuzi.
Ni kwa maelewano ya wote (consensus) na siyo kwa kupiga kura. Ndiyo
maana idadi imewekwa sawa ili sauti za pande zote zisikike sawia. Bunge
Maalum lina sharti la kufanya uamuzi kwa theluthi mbili ya kura za kila
upande kukubali. Bila ya hivyo hakuna uamuzi.
Hivyo basi, katika Bunge Maalum nguvu
si uwingi wa kura ambazo upande fulani unaweza kupata bali ni ulinganifu
sawa wa kura za kila upande peke yake. Huu ndiyo msingi unaotumika
katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa kwa lengo la
kulinda maslahi ya Zanzibar. Zanzibar ina Majimbo 50 ya uchaguzi na
Tanzania Bara ina Majimbo 189, hivyo ukiamua kwa wingi kila wakati
Wazanzibari watashindwa. Lakini, hapajakuwepo madai ya Zanzibar nao
kutaka kuwa na idadi sawa ya majimbo kama Bara au kupunguza majimbo ya
Bara yawe sawa na ya Zanzibar kwa sababu wingi si hoja. Msingi
unaotumika ni kutoa nguvu sawa za uamuzi kwa kila upande wa Muungano
wakati wa kuamua masuala ya Katiba. Hakuna mdogo wala mkubwa, wote wako
sawa. Hakuna mdogo kumezwa na mkubwa. Ndiyo msingi unaopendekezwa
kutumika kwenye Bunge Maalum hivyo hakuna kitakachoharibika kwa idadi ya
Wajumbe kutokukulingana. Nadhani inafaa ibaki ilivyo. Lakini kama
Wabunge wataamua waongeze idadi itakuwa kwa sababu nyingine siyo hii ya
mfano wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Katika orodha ya madai ya ndugu zetu
wa upinzani lipo suala la uhai wa Tume ya Katiba. Wanataka usiishe
wanapokabidhi rasimu ya pili kwa Bunge Maalum bali waendelee kuwepo
mpaka mwisho wa mchakato. Nimeulizia ilikuwaje? Nimeelezwa kuwa jambo
hili halitokani na mapendekezo ya Serikali wala ya Kamati ya Bunge ya
Katiba, Sheria na Utawala. Limetokana na pendekezo la Mbunge katika
Bunge wakati wa kupitia vifungu na kuungwa mkono na Wabunge wengi. Kwa
hiyo kuilaumu Serikali si haki. Serikali inaweza kuwa mshirika katika
hoja hii.
Nami naiona hoja ya Wajumbe wa Tume
kuwa na wajibu wakati wa Bunge Maalum hasa wa kusaidia kufafanua
mapendekezo ya Tume. Je ushiriki huo uwe vipi? Je ni Wajumbe wote au
baadhi yao ni jambo linaloweza kujadiliwa.
Ndugu Wananchi;
Naomba nimalizie kwa kuwasihi viongozi
wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi kuongozwa na hekima iliyotumika wakati
tulipokuwa na tatizo linalofana na hili kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba. Mimi naamini kama iliwezekana kufanikisha mambo wakati ule
inaweza kufanya hivyo hata safari hii. Itatufikisha pale tunapopataka
salama salimini bila maandamano, kushupaliana au uvunjifu wa amani.
Kupanga ni kuchagua, naomba sote, mmoja mmoja na kwa umoja wetu tuchague
njia ya mazungumzo na maelewano kwani itaihakikishia nchi yetu amani,
usalama na utulivu. Tukifanya hivyo historia itatuhukumu kwa wema.
Mungu Ibariki Tanzania. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment