BUNGE LAONGEZWA MUDA KUJADILI VAT,ARDHI
Dodoma.
Bunge limeongeza muda wa vikao kwa siku tatu zaidi ili kutoa nafasi kwa
wabunge kujadili Muswada wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), ambao
unalenga kuondoa misamaha ya kodi.
Kwa mujibu ya ratiba ya awali, vikao
vya Bunge vilivyoanza Mei 6, mwaka huu vilikuwa vimalizike Juni 27,
mwaka huu lakini sasa ratiba hiyo imesogezwa hadi Juni 30, mwaka huu.Wiki iliyopita, Spika wa Bunge, Anne Makinda alikaririwa akisema kuwa Bunge litaongeza muda ili kujadili muswada huo na ripoti ya kamati teule iliyoundwa kuchunguza migogoro ya ardhi nchini.
"Kwa mujibu wa kanuni zetu, hatuingizi kitu kingine katika Bunge la Bajeti zaidi ya bajeti, lakini tunaangalia uwezekano wa kuongeza muda baada ya bajeti kwa siku chache kwa sababu ya mambo yanayotakiwa kufanyika. Naambiwa kuwa Serikali inataka kuleta sheria inayohusiana na VAT."
Hivi karibuni akiwa bungeni, Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alitishia kukusanya sahihi za wabunge kumwondoa Spika Makinda iwapo muswada huo hautawasilishwa katika Bunge hili la bajeti ili kufuta misamaha ya kodi.
Mbunge huyo alisema katika bajeti iliyopita, nchi ilipoteza Sh1.5 trilioni kwa misamaha ya kodi kiwango ambacho ni sawa na kile kilichopungua katika Bajeti ya Serikali mwaka jana.
"Kama hawajaleta muswada kiofisi, mimi siwezi kufanya chochote lakini nimesikia kuwa Serikali inataka kuleta muswada huo," alisema Makinda.
Kuhusu ripoti ya migogoro ya ardhi nchini, Makinda alisema kuongezwa kwa siku hizo kutawawezesha wabunge kuijadili.
Alisema kamati ya Bunge iliyopewa kuchunguza migogoro hiyo ilikwenda mbali zaidi na kuona vitu vingi yakiwamo matatizo yaliyopo katika mfumo.
Kamati hiyo teule iliundwa Novemba 9, mwaka jana na Makinda, kuchunguza migogoro inayowahusisha wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Wajumbe waliounda kamati hiyo ni Profesa Peter Msola aliyekuwa Mwenyekiti na wajumbe Jenista Mhagama Magdalena Sakaya, Joseph Selasini na Christopher Ole Sendeka.
Kamati hiyo ilipewa jukumu la kuchunguza kasoro zilizopo katika matumizi ya ardhi na kupeleka mapendekezo bungeni, ambayo yatapunguza na kuondoa migogoro ya muda mrefu yanayoendelea kati ya wakulima, wafugaji, wawekezaji na watumiaji wengine wa ardhi.(E.L)
No comments:
Post a Comment