KAMPUNI YALIPA MILIONI 800/= KUTAFITI GESI
MOJA ya
kampuni nne zilizofikia makubaliano na Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa
Uwekezaji nchini (EPZA) kutoa huduma mbalimbali kwa kampuni kubwa
zinazofanya utafiti wa mafuta na gesi mkoani Mtwara, imetoa malipo ya
awali kwa ajili ya kufanikisha nia hiyo.
Kampuni
hiyo, Altus Oilfield Services FPZ ya Singapore imetoa hundi ya dola za
Kimarekani 526, 280 sawa na Sh milioni 800 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa
miundombinu ya eneo hilo.(Martha Magessa)
Mkurugenzi
Mkuu wa EPZA, Dk Adelhelm Meru aliwaambia waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam wakati wa kupokea hundi hiyo kuwa fedha hizo
zitatumika kuanza kujenga miundombinu ya msingi kama barabara, umeme,
maji na njia ya maji taka katika eneo la kampuni hiyo.
“Uwekezaji katika eneo hilo utasaidia kukuza ajira na uchumi wa nchi kuimarika zaidi,” alisema.
EPZA
inaendeleza hekta 10 za eneo huru la Bandari ya Mtwara. Mwakilishi wa
Kampuni ya MAC Group Limited aliyekabidhi hundi hiyo, Nagarayan
Sankaranarayanan alisema kampuni yake imejiandaa kuanza kufanya kazi ya
kutoa huduma kwa kampuni za utafutaji gesi na mafuta.
Eneo hilo ni kati ya hekta 110 za eneo hilo huru la bandari ambalo limetengwa na serikali kwa ajili ya uwekezaji mbalimbali.
Hekta
hizo 10 zitaendelezwa kwa kuwekewa miundombinu inayotakiwa na kisha
kugawiwa kwa kampuni za kimataifa zinazofanya kazi za kutoa huduma
mbalimbali kwa kampuni zinazofanya utafiti wa mafuta na gesi katika Mkoa
wa Mtwara.
Imeelezwa
kituo hicho cha huduma kwa kampuni zinazofanya utafiti,
kitakapokamilika kitakuwa cha kipekee si kwa Tanzania pekee, bali katika
ukanda mzima wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Kampuni
nyingine zilizoingia Mkataba na EPZA mwezi uliopita kuwekeza katika eneo
hilo, ni Slumberger Seaco Inc ya Marekani, Tans Ocean Industries and
Services LTD ya Dubai na Lenna ya Iran.
Kazi ya
kupata wawekezaji katika eneo hilo, ilianza mwaka 2010 baada ya kampuni
za utafutaji gesi na mafuta kuomba kuwepo kwa kampuni za watoa huduma.
Miongoni
mwa vitu vitakavyokuwepo katika eneo hilo, ni karakana kubwa kwa ajili
ya kufanyia ukarabati na matengenezo ya vifaa vya mafuta na gesi.
Karakana hizo zitajengwa kisasa na zitakuwa na uwezo pia wa kuhudumia nchi jirani kama vile Kenya, Msumbiji, na Afrika Kusini.
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment