WADAU WAKUTANA KUPINGA UBAKAJI
Angelina Jolie ni mmoja wa wanaharakati maarufu wanaopinga dhuluma za kingono ikiwemo ubakaji
Viongozi
wa kimataifa wanakutana jijini London kwa wiki nzima, kwa kongamano la
kumaliza dhulma za kimapenzi katika mataifa yanayokabiliwa na mizozo
Mkutano
huo, wa siku nne umeandaliwa na Waziri wa masuala ya nchi za kigeni wa
Uingereza, William Hague na muigizaji maarufu na mjumbe maalum wa Umoja
wa mataifa, Angelina Jolie.
Kongamano
hilo linajiri huku mataifa kadhaa barani Afrika yakikabiliwa na
changamoto ya kumaliza ubakaji unaotumiwa kama silaha ya kivita.
Ni mwanzo
wa kuidhinishwa kampeni ya miaka miwili kutoa uhamasisho kuhusu
kutumiwa kwa ubakaji na unyanyasaji wa kimapenzi kama silaha wakati wa
vita.
Waandalizi
wa kongamano hilo wanasema wanataka huu uwe wakati ambapo ulimwengu
utazinduka na kutangaza kwamba unyanyasaji wa kimapenzi sio jambo
lisiloweza kuepukika wakati wa vita.
Tangu
William Hague na Angelina Jolie wazinduwe kampeni hiyo, mataifa mia moja
na arobaini na nane yameidhinisha azimio la uwajibikaji wa kumaliza
unyanyasaji huo wa kimapenzi katika mizozo.
Lakini lengo sasa ni kuchukua hatua madhubuti, kuendeleza uchunguzi na kuripotiwa kwa visa hivyo vya unyanyasaji wa kimapenzi.
Pia
katika kutoa usaidizi zaidi kwa waathiriwa na kuhakikisha kuwa usawa wa
kijinsia unahimizwa katika operesheni za siku zijazo za kulinda amani.
Kiwango
cha jukumu hilo ni kikubwa: katika miaka ya tisaini, vita vya Bosnia
vilisababisha kuwepo takriban waathiriwa elfu hamsini wa unyanyasaji wa
kimapenzi.
Takriban miongo miwili tangu vita hivyo vimalizike, ni wahalifu wapatao 60 pekee walioshtakiwa.
CHANZO:BBC
No comments:
Post a Comment