SERIKALI YASISITIZA KUFUTWA HATI MASHAMBA YA MKONGE
SERIKALI
imesisitiza kufuta baadhi ya hati miliki za mashamba ya mkonge katika
Mkoa wa Tanga na kugawia wananchi. Waziri wa Kilimo, Chakula na
Ushirika, Christopher Chiza, aliliambia Bunge jana kuwa tayari baadhi ya
mashamba yamepelekwa Ofisi ya Rais kwa ajili ya kufutiwa hati miliki.
Chiza pia
alisema wakulima wengi wameshindwa kuendeleza mashamba hayo kutokana na
kuwapo migogoro kwa wamiliki kutumia mashamba hayo kujipatia mikopo
kutoka kwenye benki
Akitoa
mfano wa utekelezaji wa hilo, Chiza alisema kuwa serikali imefanikiwa
kurejesha mashamba ya Pongwe, na tayari ardhi hiyo imepimwa na kugawiwa
kwa wananchi.
“Tunawafuatilia
wawekezaji wengine katika sekta ya mkonge ili tujue changamoto
zinazowakabili kabla ya kuwanyang’anya na kuwatafuta wawekezaji wengine
kwa ajili ya kuendeleza mashamba,” alisema.
Alisema
kuna baadhi ya wawekezaji ambao wamechukua mikopo benki kwa kutumia
mashamba kama udhamini na wameshindwa kulipa mikopo hiyo, jambo ambalo
limelazimisha benki kushikilia hati miliki.
Chiza
alielezea uamuzi wa kubinafsisha mashamba makubwa ulifikiwa na serikali
kati ya mwaka 1996 na 1999 na kutekelezwa na Tume ya Kurekebisha
Mashirika ya Sekta ya Umma (PSRC).
Alisema
lengo lilikuwa ni kuinua uzalishaji, lakini baadhi yao wameshindwa na
kutolea mfano mashamba ya Marungu, Pongwe, Amboni na Kilimangwido.
Chiza
alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Amina Mohamed Mwidau
(CUF) aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani na mashamba ya mkonge
katika Wilaya ya Tanga na Pangani ambayo hayazalishi tena.
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment