KESI TANO ZA MABILIONI USWISI ZA CHUNGUZWA
Tanzania
imeomba msaada kwa taasisi iitwayo International Centre for Asset
Recovery – ICAR (Kituo cha Kimataifa cha Urejeshaji Mali) ya Uswisi
kuchunguza kesi tano zinazohusu watu na taasisi zinazotuhumiwa kuficha
mabilioni ya fedha nchini humo.
Itakumbukwa
kuwa baada ya kuibuka kwa sakata la mabilioni hayo ya Uswisi, Serikali
iliunda kikosi kazi chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick
Werema kulifanyia kazi.
Gazeti
hili lilifuatilia suala hilo hadi Uswisi na kubaini kuanza kwa uchunguzi
huo, huku fedha nyingi zikitajwa kwamba zinatokana na vitendo vya
rushwa.
Akizungumza
na mwandishi wetu mjini Bern, Uswisi hivi karibuni, Mtafiti wa Sheria
wa ICAR, Andrew Dornbierer alisema: "Tuna makubaliano na Serikali ya
Tanzania hasa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), tunachunguza
kwa kina kesi za rushwa na utoroshwaji wa fedha, hivyo tuko katika
ukusanyaji wa taarifa. Siwezi kukupa mifano ya moja kwa moja kwa sababu
bado tunazifanyia kazi na tunadhibitiwa katika utoaji wa taarifa."
Mkurugenzi wa ICAR, Gretta Fenner Zinkernagel alithibitisha uwepo wa kesi hizo za Tanzania.(P.T)
"Ni kweli
tumeombwa na Serikali ya Tanzania kusaidia kuchunguza baadhi ya kesi...
zilikuwa zimeshachunguzwa lakini kutokana na uwezo wao mdogo
tunawasaidia. Kwa harakaharaka naweza kusema tunazo kesi tano hivi... ni
kesi za watu binafsi na taasisi na zinahusu masuala ya fedha. Hatuwezi
kutaja majina kwa sababu tunakatazwa kabisa na mkataba wetu na taasisi
tunazofanya nazo kazi."
Licha ya
kutotaja majina, Zinkernagel alisema wanaochunguzwa katika kesi hizo
wanahusishwa na kampuni hewa zilizoanzishwa kwa lengo la kuchota fedha
kisha kwenda kuzificha nje ya nchi.
"Kuna
watu wenye masilahi binafsi na wamekuwa wakipokea rushwa au wamekuwa
wakitumia mashirika kwa ubia au kampuni kivuli na ushirika mwingine wa
kimataifa ili kusafirisha fedha kwenda kwenye kampuni fulani kwa lengo
la kuzificha. Ni kampuni zinazotumiwa na wafanyabiashara kuhamisha fedha
haramu na mwisho hujisafisha," alisema.
Jaji Werema
Jaji
Werema alikiri Tanzania kuiomba ICAR kufanya uchunguzi huo lakini
akakataa katakata kutaja watu wala kampuni zinazofanyiwa uchunguzi.
"Hatuwezi
kutaja majina ya watu waliofunguliwa kesi kwa sababu kwanza tutakuwa
tumeingilia haki zao kisheria. Pili, tunaweza kuwataja lakini baadaye
ikabainika kuwa si kweli, bali ni tuhuma tu na wakaja kutushtaki na
tatu, tutakapowataja watu hao tuliowafungulia kesi tutaharibu upelelezi
wetu.
"Katika
kesi hizi, kisheria, tunafanya kazi zetu kwa utaratibu ili tusiharibu
upelelezi na tupate mambo mengi. Mnadhani tumekaa kimya hatufuatilii
lakini tunafanya kazi yetu. Siku ikifika mtaona na mtasikia."
Soma Zaidi>>>>>>>Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment