KANUNI KUDHIBITI MATUMIZI MABAYA YA MTANDAO

WAZIRI wa
 Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa
 wizara yake inatayarisha Kanuni, zitakazodhibiti matumizi mabaya ya 
mtandao wa intaneti, ikiwemo uwekezaaji wa picha chafu mtandaoni.
“Serikali
 ipo tayari kuleta Kanuni za Online Content na za kudhibiti picha 
chafu,” alisema Profesa Mbarawa, alipojibu swali la nyongeza Mbunge wa 
Mkanyageni, Habib Mnyaa (CUF). Swali la msingi liliulizwa na Mbunge wa 
Mchinga, Said Mtanda (CCM).(Martha Magessa)
        
Mbarawa alisema Kanuni hiyo inatungwa na italetwa bungeni hivi karibuni ili kutoa mwongozo na kudhibiti matumizi ya intaneti.
Waziri 
huyo alisisitiza kuwa Tume ya Mawasiliano nchini (TCRA) ina mtambo na 
kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, wana uwezo wa kuchunguza na kubaini
 kiini na chanzo cha picha chafu na matumizi mengine mabaya ya intaneti.
Katika 
swali lake la nyongeza, Mtanda alisema bunge lilishapitisha Sheria ya 
Usajili wa Simu, ambayo iliipa meno TCRA kuwa msimamizi wa mambo yote 
yanayohusu simu na intaneti nchini.
Mtanda 
alisema TCRA wana uwezo huo, lakini wameshindwa kusimamia sheria hiyo na
 ndiyo maana kuna matumizi mabaya ya intaneti hivi sasa. Baada ya majibu
 hayo ya Mbarawa, Spika wa Bunge, Anne Makinda alimhoji Waziri huyo kuwa
 “ Na yaliyotokea juzi, mmefanya nini?”.
Papo 
hapo, wakasimama wabunge kadhaa akiwemo Mbunge wa Mbinga Magharibi, John
 Komba (CCM), waliotaka kuuliza maswali ya nyongeza.
Hata 
hivyo, Spika alisema muda uliotengwa kwa ajili ya swali hilo, ulikuwa 
umeisha, hivyo wabunge hao ikiwemo Komba, walilazimika kuketi chini, 
bila kupata fursa ya kutoa dukuduku zao.
Katika 
swali lake la msingi, Mtanda alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na 
serikali kukomesha wimbi kubwa la mmomonyoko wa maadili kupitia njia 
mbalimbali, hasa kupitia picha chafu katika mitandao.
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment