BAJETI KAA LA MOTO BUNGENI
KAMATI ya
Kudumu ya Bajeti imeonesha wasiwasi kuhusu ongezeko la haraka la deni
la taifa na kusema hali hiyo inatishia ukuaji endelevu wa uchumi.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Andrew Chenge aliliambia Bunge jana, ongezeko
la ghafla la deni la taifa kutoka Sh trilioni 23.67 Machi mwaka jana,
hadi Sh trilioni 30.56 Machi, mwaka huu, linadhihirisha wasiwasi wa
matumizi mabaya ya fedha za umma.
"Ingawa
Serikali imesema deni hilo ni himilivu, ongezeko hili la Sh trioni 1.6
kwa mwaka linatia wasiwasi kama ukusanyaji mapato na matumizi
vinawiana," alisema Chenge wakati na kushauri pawepo nidhamu katika
matumizi ya Serikali.
Chenge
ambaye alikuwa akiwasilisha maoni ya Kamati katika kujadili Bajeti Kuu
ya Serikali, alisema kumekuwapo ongezeko la deni la ndani ambalo
halijajumuishwa katika deni la taifa jambo ambalo linaonesha kuwa deni
hilo si himilivu kama ilivyosemwa na Serikali.
Serikali
imepanga kutumia Sh trilioni 4.354, ikiwa ni asilimia 21.93 ya bajeti
kuu ya Sh trilioni 19.6 kwa mwaka 2014/2015 kwa ajili ya kulipia deni la
taifa. Chenge alisema kamati inashawishika kuona kwamba serikali haina
ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato.
Aidha
alisema Serikali imepuuza ushauri wa kamati yake juu ya vyanzo vipya vya
mapato yasiyo ya kodi ambayo ni pamoja na uvuvi wa kina kirefu,
uwindaji katika vitalu, mazao ya misitu na madini.
Wiki
iliyopita, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum aliliambia Bunge kwamba
deni la taifa ni himilivu kutokana na tathimini ya madeni (DSA)
iliyofanywa mwaka juzi katika kutathimini madeni ya nchi.
Aidha,
Kamati imesisitiza kuwapo kwa usimamizi wa matumizi ya fedha za umma.
"Pamoja na Serikali kuahidi kuzingatia ushauri wa Kamati, lakini hakuna
mabadiliko yoyote na uchambuzi wa Kamati umebaini hakuna mabadiliko
katika kudhibiti mapato na matumizi ya fedha za umma," alisema Chenge.
Aidha,
Chenge alisema Kamati imebaini kuwapo kwa madeni makubwa kwa baadhi ya
wizara na taasisi za umma. Alitoa mfano wa Wizara ya Ujenzi ambayo
imekuwa na malimbikizo ya madeni hivyo kulazimu kutumia bajeti kulipia
madeni badala ya kutekeleza miradi iliyoidhinishwa kwa mwaka husika.
Kamati
pia imeishauri Serikali kuagiza maofisa Maduhuli wote nchini kulipa
madai ya wazabuni kwa wakati kuepushia Serikali malimbikizo ya madeni na
kusababisha hasara kwa makandarasi na uwezo wa makandarasi.
Nidhamu
ya matumizi Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha, James Mbatia ametaka
Serikali kutunga Sheria ya Bajeti kudhibiti ukopaji na matumizi ya
Serikali na kupendekeza kuwa mikopo yote ya serikali ipitie bungeni
kabla ya kukopa ili kujadili na kuridhiwa.
Ametaka
serikali kuonesha nia ya dhati katika nidhamu ya fedha na kupambana na
matumizi ya kifahari, ikiwa ni pamoja na matumizi ya magari ghali kwa
ajili ya maofisa wake.
Akiwasilisha
maoni ya Kambi ya Upinzani Bungeni kuhusu bajeti ya Serikali ya mwaka
2014/2015, Mbatia pia alionesha wasiwasi wa kambi yake juu ya kuongezeka
kwa deni la taifa.
Alisema
limefika kiwango ambacho si himilivu tena. " Hali hii ya ongezeko la
deni la taifa haijawahi tokea katika historia ya taifa hili," alisema.
Alisema, "
Ukuaji wa uchumi ni asilimia sita, wakati deni la taifa linaongezeka
kati ya asimilia 15 hadi 30, hivyo bila kuwa na vyanzo vipya vya mapato
italeta matatizo katika uchumi."
Katika
hatua nyingine, Kambi ya Upinzani imetaka Serikali ieleze kama fedha
zilizokopwa ndani ya miaka saba zimetumika katika maendeleo na
imechangia kiasi gani katika kuleta maendeleo.
" Kama
fedha zilizokopwa ndani ya miaka saba ambazo ni Shilingi trilioni 25,
zingeelekezwa kuinua kilimo, basi kila kata hapa nchini ingepata trekta
281 jambo ambalo lingeifanya nchi kuongeza uzalishaji wa chakula,"
alisema.
Akichangia
bajeti hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Abdallah Amour (CUF)
alipongeza hatua ya Serikali ya kufuta baadhi ya misamaha ya kodi.
Alitaka utekelezaji wake ufanywe kwa uangalifu na hatua kwa hatua.
Aidha alitaka Serikali kuwachukulia hatua wanaoibambikia Serikali madeni yasiyohalali.
Amour alitaka kufahamu ni kiasi gani kimepatikana kutokana na mfumo wa kuandika majina kwenye namba za magari.
Alishauri
kama mfumo huo haujawa na mafanikio, Serikali iangalie uwezekano wa
kupunguza tozo kutoka Sh milioni tano za sasa hadi Sh milioni mbili na
pia fursa hiyo itolewe kwa usafiri wa pikipiki.
Naye
Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine (CCM), alisema kuchelewa kwa
utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa barabara imekuwa
chanzo cha kuongeza deni la taifa.
Aidha,
alisema katika kufikia uchumi wa kati, ni vyema Serikali ikawekeza
katika kilimo na Serikali ihusike katika kutafuta masoko ya mazao hayo
huku akiishauri Serikali kuhakikisha inakuja na mkakati utakaowafanya
Watanzania kufanya kazi na kutoendelea kuwa kwenye vijiwe huku wakiwa
walalamikaji.
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment