VIONGOZI WA IGAD WAKUTANA ETHIOPIA

Viongozi 
wa jumuia ya maendeleo ya Afrika mashariki na pembe ya Afrika- IGAD, 
wanapanga kukutana mjini Addis Ababa, Ethiopia, Jumanne kujadili namna 
ya kuimarisha usalama na amani katika kanda yao pamoja na kuimarisha 
ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa kati ya mataifa hayo sita. Hata hivyo
 maafisa walioko karibu na mkutano huo wanasema suala la ugomvi wa Sudan
 Kusini litakua juu katika ajenda yao.
Maafisa 
wa IGAD wanasema viongozi watakaoshiriki watajaribu kutafuta njia za 
kupata suluhisho kwa mzozo huo wa Sudan Kusini na kadhalika namna ya 
kukabiliana na vitisho vinvyotolewa na kundi la wanamgambo wa ki-Islamu 
la Al-Shabab kutoka Somalia. 
        
Wizara ya
 mambo ya nchi za nje ya Marekani ilitangaza Jumatatu kwamba mjumbe 
maalum kwa Sudan na Sudan kusini, Donald E. Booth pamoja na mshauri mkuu
 wa masuala ya kisheria wa wizara hiyo Thomas A. Shannon, wanatarajiwa 
kuhudhuria mkutano wa viongozi wa IGAD. Mkutano huo wa viongozi 
utafanyika baada ya Rais Salva Kiir kukutana na kiongozi wa upinzani 
Riek Machar.
Hata 
hivyo waziri wa masuala ya nchi za nje wa Sudan Kusini, Barnaba Marial 
Benjamin, anasema mkutano kati ya Rais Kiir na Bwana Machar unafanyika 
kama sharti lililotolewa na wapatanishi kwamba viongozi hao waone kwa 
kiwango gani makubaliano ya kusitisha uhasama yametekelezwa hadi sasa.
Mkutano 
wao unafanyika mwezi mmoja baada ya wote bwana Kiir na bwana Machar 
kutia saini mkataba huko Ethiopia kuahidi tena juu ya utekelezaji wa 
makubaliano ya kusitisha uhasama waliokubaliana awali na huku 
majadiliano yanaendelea baina ya pande hizo mbili.
Wote 
serikali na waasi hivi karibuni walilaumiana kwa kuhujumu makubaliano ya
 kusitisha uhasama. Lakini bwana Benjamin anasema waasi ndio wa 
kulaumiwa kwa tukio la kushambulia vituo vya serikali. Mzozo huo 
umepelekea maelfu ya watu kupoteza makazi yao.
Bwana 
Benjamin anasema serikali ya Juba inadhamira ya dhati kuendelea na 
mazungumzo ya amani, lakini anatoa wito kwa viongozi wa kikanda 
kushinikiza waasi kuyachukulia kwa dhati majadiliano hayo. Ghasia huko 
Sudan Kusini zilizuka baada ya Rais Salva Kiir, kutoka kabila la Dinka, 
kumshutumu Makam Rais wa zamani Riek Machar anayetoka kabila la Nuer 
kujaribu kumpinduwa. Machar anakana tuhuma hizo, lakini hatimae aliunda 
kundi la waasi kupigana dhidi ya utawala wa Juba.
CHANZO:VOA
No comments:
Post a Comment