TANZANIA YA PILI VITA DHIDI YA RUSHWA
WAZIRI wa
Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, George Mkuchika amesema Tanzania
inashika nafasi ya pili kati ya nchi tano za Shirikisho la Afrika
Mashariki katika suala la utawala bora na vita dhidi ya rushwa.
Waziri
Mkuchika aliyasema hayo wakati akizindua Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi
wa Umma iliyoanza jana kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es
Salaam.
Alisema
tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza, Serikali ya Tanzania ilitangaza vita
dhidi ya rushwa na imekuwa ikiimarisha mapambano dhidi ya adui huyo hadi
katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete.
“Katika
nchi za Afrika Mashariki suala la utawala bora na vita dhidi ya rushwa,
Tanzania tunashika nafasi ya pili, Rwanda ni ya kwanza, ya tatu ni
Uganda na ya nne ni Kenya,” alisema Waziri Mkuchika.
Waziri
Mkuchika alikuwa akizungumzia madai yanayotolewa na baadhi ya watu hapa
nchini kuwa Serikali ya Tanzania haina dhamira ya kupambana na rushwa.
Alikanusha
madai hayo na kusema kuwa Serikali ina dhamira ya kupambana na rushwa
ndio maana imepitisha Sheria dhidi ya Rushwa na kuiboresha Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ambayo sasa ina matawi kila
mkoa na kila wilaya.
Alisema
kiashiria kingine cha kuthibitisha kuwa Serikali ya Tanzania inapambana
na rushwa ni kufikishwa mahakamani kwa watu wanaotuhumiwa na rushwa.
Hata
hivyo, alibainisha kuwa mtumishi wa Takukuru hawezi kuwafikisha watu
mahakamani bila ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi. Hivyo aliwataka
Watanzania wote kutambua kuwa wana wajibu wa kupambana na rushwa kwa
kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili kufanikisha vita hiyo.
Aliwakumbusha
Watanzania kuwa mtumishi yeyote wa umma kumhudumia mwananchi ni haki
yake, hivyo mtumishi anayeomba rushwa ili atoe huduma anashiriki katika
tendo la rushwa.
Kutokana
na hali hiyo, aliwaomba watumishi wajiepushe na rushwa kwani inawanyima
watu haki na kwamba kukiwa na malalamiko anayepata haki ni yule anayetoa
rushwa. Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ya mwaka
huu inasema
“Mkataba
wa Misingi na Kanuni za Utumishi wa Umma Barani Afrika ni Chachu ya
Kuimarisha Utawala Bora na Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa
Uwazi.”
CHANZO:HABARILEO
No comments:
Post a Comment