TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Tuesday, June 3, 2014

LISU ARUSHA KOMBORA LINGINE KWA MAWAZIRI 

lissupx b4f46
Na Hudugu Ng'amilo
Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Binilith Mahenge, jana walituhumiwa kutumia vibaya nafasi zao kwa kuweka fedha nyingi za miradi ya maji katika maeneo wanakotoka, huku sehemu zenye matatizo ya huduma hiyo zikitengewa fedha kiduchu.
Ilielezwa bungeni jana kuwa Profesa Maghembe ambaye ni Mbunge wa Mwanga, Kilimanjaro, wizara yake imetenga Sh1.4 bilioni kwa ajili ya miradi ya maji, ambazo ni zaidi ya mara saba ya Sh190 milioni zilizotengwa kwa ajili hiyo katika Wilaya ya Ikungi, Singida.
Akichangia Bajeti ya Wizara ya Maji jana, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alihoji kile alichokiita upendeleo wa wazi katika ugawaji wa fedha za maji, unaoipa kipaumbele baadhi ya mikoa wanakotoka mawaziri.
Pia aliitaja Wilaya ya Makete, Njombe anakotokea Dk Mahenge ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Maji kuwa imetengewa Sh1.9 bilioni na kusema: "Upendeleo wa aina hii haufai kwa sababu utaleta matatizo na siyo haki hata kidogo."
"Profesa Maghembe atueleze sababu za kutenga bajeti hii kwa upendeleo, huku mikoa isiyokuwa na vyanzo vya maji, mito ya kudumu na mabwawa ya maana imepewa bajeti kidogo ikilinganishwa na ile yenye mifumo mizuri ya maji," alisema Lissu.
Alisema licha ya Profesa Maghembe katika hotuba yake kutaja mikoa ya Dodoma, Singida, Simiyu na Shinyanga kuwa inakabiliwa na upungufu wa maji, imetengewa kiasi kidogo cha fedha, huku mikoa inayopata mvua za kutosha na vyanzo vya uhakika vya maji ikitengewa mabilioni ya fedha.
"Dodoma imetengewa Sh7.2 bilioni, Singida Sh3.2 bilioni, Shinyanga Sh3.2 bilioni na Simiyu Sh2.8 bilioni, wakati mikoa yenye vyanzo vya maji na mvua za kutosha imetengewa fedha nyingi; mfano ni Tanga Sh10.7 bilioni, Kilimanjaro Sh6.3 bilioni, Mbeya Sh9.2 bilioni na Mtwara Sh7.5 bilioni," alisema.
Lissu alisema hali hiyo inaweza kutafsiriwa kuwa mawaziri hao wanatumia mamlaka yao kujipendelea na kuhoji kama huo ndiyo utaratibu wa Serikali ya CCM... "Kama utaratibu wa mgawanyo wa fedha ndiyo huu sisi tunaotoka mikoa yenye ukame tutapataje maji?"
Jana Profesa Maghembe aliendelea kuwa katika wakati mgumu, baada ya kuandamwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika ambaye alimwita kuwa ni mzigo kutokana na kutokutolewa kwa fedha za miradi ya maji.
Mnyika alionyesha kushangazwa na wabunge wenzake kuunga mkono bajeti ya wizara hiyo, licha ya kuwa ndogo na fedha za miradi zimekuwa hazitolewi kama inavyotakiwa.
"Kwa kufanya hivi sidhani kama tunamsaidia Profesa Maghembe ambaye ni CCM. Fedha zilizotengwa mwaka jana kuisaidia wizara hii hazijatoka na za bajeti hii hazitatoka kwa kiwango cha kuwezesha utekelezaji. Namna bora ya kumsaidia ili viongozi wa CCM wasiendelee kumwita mzigo ni kuikataa bajeti hii ili Serikali irudi mezani na kujiuliza."
Mnyika alisema kuwa hata ahadi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa Serikali itaongeza Sh80 bilioni kwa wizara hiyo kabla ya Mei 31 mwaka huu nayo haijatekelezwa na kusisitiza kuwa wabunge wakiipitisha bajeti hiyo watakuwa wameuziwa mbuzi kwenye gunia.Alisema kuwa hata miradi ya maji jijini Dar es Salaam ambayo Profesa Maghembe aliahidi kuwa itakamilika mpaka sasa hakuna kilichofanyika.
Mbunge wa Mbozi Magharibi (Chadema), David Silinde alisema Profesa Maghembe amechota mabilioni ya fedha na kuyapeleka katika miradi ya maji kwenye jimbo lake la uchaguzi wakati maeneo mengine ameyaacha licha ya kuwa yana kipaumbele na kwamba anatumia miradi ya Serikali kujinufaisha kisiasa.
"Ukitaka takwimu zote ninazo hapa, idadi ya watu kwako ni wachache kuliko hata kwangu lakini kwa vipindi viwili mfululizo umekuwa ukijitengea mabilioni ya fedha, wewe ni mzigo kabisa," alisema Silinde.
Mwandosya amtetea
Wakati akijibu hoja za wabunge, Profesa Maghembe hakugusia tuhuma hizo na badala yake Profesa Mwandosya alimtetea akisema miradi hiyo katika wilaya za Same, Mwanga na Korogwe ilianza wakati yeye (Mwandosya) akiwa Waziri wa Maji... "Si kweli kwamba Profesa Maghembe anapendelea jimbo lake kwa sababu hakuwa waziri wa wizara hiyo wakati mradi huo unaanzishwa. Wananchi wa Same, Mwanga, Korogwe na Simanjiro wana haki ya kupata maji kama wananchi wa sehemu nyingine yoyote. Mwacheni waziri atekeleze majukumu yake ili watu hawa wapate maji".
Alisema mradi wa maji wa Same, Mwanga na Korogwe ni muhimu sana kwa sababu utakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 400,000 ambao hawapati maji kabisa.
Alisisitiza kuwa yuko tayari kubeba lawama juu ya mradi huo na si Profesa Maghembe, kwani waziri huyo anafanya kazi nzuri ya kutekeleza mradi huo ambao ulikuwapo hata kabla hajapelekwa katika wizara hiyo.
CHANZO MWANANCHI.

No comments:

Post a Comment