TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Friday, June 13, 2014

BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/2015 

HOTUBA YA MHESHIMIWA WAZIRI WA FEDHA, SAADA MKUYA SALUM (MB) AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA KWA MWAKA 2014/15

 
UTANGULIZI:
 
1.       Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa hapaBungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha kwa mwaka 2014/15.
 
2.       Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumshukuruMwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuniwezesha kuwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya mwaka 2014/15. Aidha, natoa shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuniteua kuwa Waziri wa Fedha. Ninaahidi kwamba nitatekeleza jukumu hili kwa weledi na uadilifu. Vile vile, nawapongeza Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Mhe. Adam Kighoma Ali Malima (Mb) kwa kuteuliwa kuwa Naibu Mawaziri wa Wizara ya Fedha. Kadhalika, namshukuru pia aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Janeth Zebedayo Mbene (Mb) kwa utendaji kazi wake mahiri na tunamuombea Mwenyezi Mungu ampe nguvu na afya njema katika kazi zake mpya Wizara ya Viwanda na Biashara. Nichukue pia fursa hii kumpongeza Bw. Rished M. Bade kwa kuteuliwa kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.

 
3.       Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewemwenyewe, Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kuongoza vyema majadiliano ya Bunge la Bajeti.
 
4.       Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kuishukurukwa namna ya pekee Kamati ya Kudumu ya Uchumi, Viwanda na Biashara chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Luhaga Joelson Mpina (Mbunge wa Kisesa) na Makamu wake Mhe. Dunstan Luka Kitandula (Mbunge wa Mkinga) kwa maoni, ushauri na mapendekezo waliyoyatoa kwa Wizara wakati wa kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Fedha. Aidha, nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti Mhe. Andrew John Chenge (Mbunge wa Bariadi Magharibi) pamoja na Kamati nzima kwa ushauri wao. Katika uandaaji wa hotuba hii, Wizara imezingatia ushauri na mapendekezo ya Kamati hizo pamoja na ushauri na maoni ya hoja mbalimbali zilizotolewa wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara kwa mwaka 2013/14.

 
5.       Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, Wizara ilipatapigo kwa kuondokewa na kiongozi wetu mkuu Marehemu Dkt. William Augustao Mgimwa. Tunawashukuru Viongozi wa Serikali, Waheshimiwa Wabunge, Washirika wa Maendeleo, Taasisi mbalimbali pamoja na wananchi kwa ushirikiano waliotupa kipindi chote cha msiba. Tumeendelea kuenzi misingi imara aliyotujengea marehemu katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Aidha, tunapenda kutoa pole kwa ndugu na jamaa kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Chalinze Marehemu Saidi Ramadhani Bwanamdogo. Vile vile, napenda kutoa pole kwa Mheshimiwa Zuberi Zitto Kabwe kwa msiba wa mama yake mzazi aliyefariki tarehe 01 mwezi Juni, 2014. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.
 
6.       Mheshimiwa Spika, tarehe 27 mwezi Mei 2014, Wizaraya Fedha ilipata pigo tena baada ya kifo cha mke wa Katibu Mkuu - Hazina. Kwa namna ya kipekee naomba nitumie tena fursa hii kutoa pole kwa Dkt. Servacius Likwelile kwa kufiwa na mkewe. Hata hivyo Dr. Likwelile ameendelea kutekeleza majukumu yake katika kipindi chote cha msiba.Wizara inatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa familia yake kwa msiba wa mpendwa wao. Namuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.

 
7.       Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza, Mhe. YusufSalim Hussein Mbunge wa Chambani, Mhe. Godfrey William Mgimwa (Mbunge wa Kalenga) na Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (Mbunge wa Chalinze) kwa kuchaguliwa kwao.
 
8.       Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee napendakutoa pongezi zangu za dhati kwa Mhe. Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Mpanda Mashariki kwa hotuba yake nzuri ambayo imetoa mwelekeo wa shughuli za Serikali kwa mwaka 2014/15.
 
9.       Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu nitaanzakuelezea mapitio ya utekelezaji wa mipango ya Wizara katika mwaka 2013/14. Nitaelezea pia mikakati mbalimbali ambayo Wizara imeweka kwa mwaka 2014/15 ili kuendelea kuboresha utekelezaji wa majukumu yake ya msingi yakiwemo: usimamizi wa Bajeti ya Serikali; ukusanyaji mapato ya Serikali; usimamizi wa misaada na mikopo; ulipaji wa Deni la Taifa; usimamizi wa matumizi ya fedha za umma; usimamizi na udhibiti wa ununuzi wa umma; usimamizi wa utekelezaji wa MKUKUTA; na usimamizi wa mashirika na taasisi za umma.

 
10.   Mheshimiwa Spika, mwisho nitawasilisha bajeti yamwaka 2014/15 kwa mafungu saba ya wizara ya fedha ambayo ni fungu 7, 10, 13, 21, 22, 23 na fungu 50 pamoja na fungu 45 la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
 
11.   Mheshimiwa Spika, naomba sasa uniruhusu nisomemaelezo haya kwa muhtasari na hotuba yote kama inavyoonekana kwenye vitabu vya hotuba iingie kwenye Hansard.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2013/14 NA MALENGO YA MWAKA 2014/15
 
12. Mheshimiwa Spika, malengo yaliyozingatiwa katika utekelezaji wa majukumu ya wizara pamoja na utekelezaji wake kwa mwaka 2013/14 ni kama unavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa nne na wa tano.
 
Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa
 
13.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, kupitiaTekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, Wizara ya Fedha katika maabara ya utafutaji wa rasilimali fedha iliwekewa malengo yafuatayo: kuongeza mapato mapya ya kodi ya shilingi trilioni 1.16; kuongeza mapato mapya yasiyo ya kodi ya shilingi bilioni 96.7; kudhibiti matumizi; na kutafuta fedha za utekelezaji wa miradi ya Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa katika sekta zinazotekeleza miradi hiyo.

14.   Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Aprili 2014, ukusanyaji 
wa mapato kutoka vyanzo vilivyoibuliwa chini ya BRN umefikia shilingi bilioni 338 sawa na asilimia 29.14 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.16. Matokeo yasiyoridhisha yalisababishwa na baadhi ya mapendekezo ya BRN kutokutekelezwa katika mwaka 2013/14. Mapendekezo hayo ni kubadilisha mfumo wa ushuru wa bidhaa zisizo za petroli kutoka specific kwenda advalorem (makisio shilingi bilioni 386) na kuanzisha kodi ya zuio ya asilimia tano kwenye bidhaa zinazotoka nje ya nchi (makisio shilingi bilioni 225.6). Kwa vile ukusanyaji wa mapato ndio msingi wa kufanikiwa kwa BRN, Serikali inachambua vyanzo mbadala vya kufidia mapato haya ili kuhakikisha lengo kuu la kuongeza mapato kwa shilingi trilioni 3.48 linafikiwa ifikapo mwaka 2015/16.

 
Mwenendo wa Uchumi
 
15. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara kupitia Benki Kuu iliendelea na jukumu la kuandaa, kusimamia na kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kuwa na kiwango kidogo cha mfumuko wa bei kwa ajili ya kuhakikisha gharama za maisha haziongezeki. Kutokana na juhudi hizi, mfumuko wa bei umeshuka kutoka wastani wa asilimia 16 mwaka 2012 hadi kufikia wastani wa asilimia 7.9 mwaka 2013. Katika kipindi hiki uchumi umeendelea kuimarika huku ukuaji halisi wa Pato la Taifa ukiongezeka kwa asilimia 7.0 katika kipindi cha mwaka 2013 ikilinganishwa na asilimia 6.9 katika mwaka 2012. Shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kiasi kikubwa ni pamoja na mawasiliano asilimia 22.8, huduma za kifedha asilimia 12.2, ujenzi asilimia 8.6, na uuzaji bidhaa wa jumla na rejareja asilimia 8.3. Katika mwaka 2014/15, Wizara kupitia Benki Kuu itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kuhakikisha kwamba lengo la msingi la utulivu wa bei na ukuaji wa uchumi linadumishwa.

 
Uandaaji na Usimamizi wa Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali
16. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara imeratibu uandaaji wa Mwongozo wa Mpango na Bajeti kwa kipindi cha 2014/15 – 2016/17 kwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kusambaza kwa wadau mwezi Desemba kama ilivyopangwa. Aidha, Wizara imeandaa na kuchapisha vitabu vya bajeti ya Serikali vya mwaka 2014/15 (Volume I, II, III na IV) kama vilivyowasilishwa Bungeni kwa ajili ya mjadala wa Bunge la Bajeti la mwaka 2014/15 unaoendelea; kitabu cha tafsiri rahisi ya bajeti ya Serikali (Citizen’s Budget) kwa mwaka 2013/14; na

 
Kitabu cha Budget Background and Medium Term Framework
 
2013/14 – 2015/16.
 
17. Mheshimiwa Spika, utekelezaji zaidi na malengo kwa mwaka 2014/15 ni kama unavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ukurasa wa saba mpaka ukurasa wa tisa. 
 
Usimamizi wa Misaada na Mikopo
 
18. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara ilifanikisha kusainiwa kwa mikataba 18 kwa ajili ya misaada na mikopo nafuu yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 958.027 kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Aidha, Wizara imeendelea kuratibu ukamilishaji wa Mwongozo mpya wa Ushirikiano wa Maendeleo - Development Cooperation Framework ambao utachukua nafasi ya Mkakati wa Pamoja wa Misaada Tanzania (MPAMITA). Mwongozo huu una lengo la kusimamia ushirikiano wa maendeleo baina ya Serikali na Wadau wa Maendeleo na kuendeleza mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji wa MPAMITA. Lengo la ujumla ni kupatikana ufanisi katika misaada kutoka kwa Washirika wa maendeleo na kubainisha wajibu wa kila mdau wa maendeleo wakiwemo raia, wabunge, asasi zisizo za kiserikali na sekta ya habari.

 
19. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara imepanga kufanya yafuatayo: kuzindua Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo na kuandaa mpango kazi wake pamoja na kuhamasisha matumizi yake kwa Washirika wa Maendeleo, Wizara, Idara Zinazojitegemea, Serikali za Mitaa, Taasisi Binafsi na Waheshimiwa Wabunge; kutathmini utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali inayotekelezwa kwa fedha toka Washirika wa Maendeleo kwa nia ya kuhakikisha kwamba thamani ya fedha inapatikana katika miradi hiyo; kushiriki kwenye majadiliano na Jumuiya za kikanda na kimataifa; na kuendelea kutafuta fedha za misaada na mikopo nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, na Misaada ya Kiufundi kutoka kwa Mashirika ya Kimataifa na nchi wahisani.

 
Ulipaji wa Deni la Taifa
 
20.   Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa limeendeleakusimamiwa na Sheria ya Madeni ya mwaka 1974 na marekebisho yake ya mwaka 2004. Wizara imeendelea kutoa kipaumbele katika ulipaji wa madeni kwa wakati ili kuepuka malimbikizo ya riba. Katika kipindi cha Julai, 2013 hadi Aprili, 2014 malipo ya deni la ndani yalifikia shilingi bilioni 1,694.53 ambapo kati ya malipo hayo riba ni shilingi bilioni 581.20 na Mtaji (principal rollover) ni shilingi bilioni 1,113.33. Aidha, deni la nje limelipwa kwa kiasi cha shilingi bilioni 340.22, kati ya kiasi hicho malipo ya riba ni shilingi bilioni 201.52 na deni halisi principal ni shilingi bilioni 138.70.
 
21.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizaraitaendelea kulipa madeni ya ndani na nje kwa wakati ikiwa ni pamoja na kulipa kwa wakati madeni mbalimbali ambayo serikali imeingia mikataba (Contractual Liabilities) na madai ya dharura (Contingent Liabilities) pindi yanapotokea.

 
Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma
 
22.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kujenga uwezowa usimamizi wa matumizi ya fedha za umma kwa kudhamini mafunzo ya muda mrefu kwa watumishi 313 wa kada ya uhasibu, ugavi na kompyuta kutoka kwenye wizara, idara za serikali, sekretariati za mikoa, manispaa, halmashauri za miji na wilaya waliopo vyuoni na watumishi 218 walipewa mafunzo ya muda mfupi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi wa matumizi ya fedha za umma. Aidha, Wizara imeendelea kusambaza Mfumo wa Malipo wa Kielektroniki -TISS. Mikoa hiyo ipo katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 11.
 
23.   Mheshimiwa Spika, utekelezaji zaidi na malengo yamwaka 2014/15 upo katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 12 na 13.

Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma - Public Finance Management Reform Programme (PFMRP)
 
24. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma imekamilisha utafiti wa mfumo wa kupeleka fedha kwenye Serikali za Mitaa, mpango wa utekelezaji wa utafiti huo umeandaliwa na utekelezaji wake utaanza mwaka wa fedha 2014/15. Aidha, utafiti juu ya mifumo ya fedha inayotumiwa na Serikali kwa lengo la kuiunganisha mifumo hiyo ili kuboresha usimamizi wake umekamilika. Vile vile, Wahasibu 522 kutoka Wizara mbalimbali, hazina ndogo na sekretarieti za mikoa walipata mafunzo juu ya Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Taarifa za Hesabu katika Sekta ya Umma na watumishi wengine 34 ambao wanasimamia programu hii kutoka katika wizara na taasisi walipata mafunzo ya kusimamia Mabadiliko na Kuandaa Mipango Mkakati -Change Management and Strategic Planning.
 
Mafunzo haya yalilenga kuwajengea uwezo wa kuandaa mipango na bajeti inayolenga katika kutekeleza maboresho ya usimamizi wa fedha za umma.

25. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara itaendelea kuboresha usimamizi wa fedha za umma kwa kuendelea na utekelezaji wa Awamu ya Nne ya Programu ya PFMRP kwa kufanya yafuatayo: kupitia na kuboresha mifumo ya kifedha na kuangalia njia bora ya kuiunganisha baada ya utafiti kukamilika; na kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani katika wizara, idara, wakala za Serikali na halmashauri za Serikali za Mitaa juu ya ukaguzi wa mifumo ya fedha, usimamizi na ukaguzi wa vihatarishi, ukaguzi wa bajeti na mishahara, na ukaguzi wa miradi.
 
Sera ya Ununuzi wa Umma
 
 
26. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa sera na udhibiti wa ununuzi wa umma, rufaa za zabuni za umma na huduma ya ununuzi serikalini ni kama unavyooneshwa katika kitabu changu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 14 hadi ukurasa wa 18.
 

Usimamizi wa Mali ya Serikali
 
27. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara iliendelea kuandaa Sera ya Mali ya Umma. Lengo la sera hii ni kusimamia na kutoa miongozo ya udhibiti wa mali ya umma. Aidha, Wizara ilifanya uthamini wa mali ya Serikali katika mikoa mitano na wizara mbili, hivyo kufanya wizara, idara zinazojitegemea na wakala wa Serikali zilizofanyiwa uthamini kufikia 42. Katika kipindi hicho, usimikaji wa mfumo wa uhakiki wa mali ya umma ulikamilika. Vile vile, Wizara iliendelea na zoezi la kuondosha mali chakavu katika wizara na idara za Serikali ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.58 zilikusanywa kutokana na mauzo ya vifaa hivyo na shilingi milioni 12.83 kutokana na utoaji wa leseni za udalali. Utekelezaji zaidi na malengo kwa mwaka 2014/15 ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 18.

Mpango wa Millenium Challenge Account Tanzania (MCA-T)

28. Mheshimiwa Spika, Programu ya Millenium Challenge Account Tanzania iliendelea na ukamilishaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji, nishati ya umeme na maji. Miradi yote ya barabara imekamilika isipokuwa sehemu ya Laela- Sumbawanga katika barabara ya Tunduma-Sumbwanga ambayo inatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka 2014. Miradi ya umeme na maji imekamilika na ipo katika kipindi cha uangalizi. Aidha, kutokana na utekelezaji wa kuridhisha, Tanzania imekidhi vigezo na hivyo itanufaika na awamu ya pili ya msaada wa Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC). Katika awamu ya pili, miradi itakayofadhiliwa ni ya umeme na barabara za vijijini Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Ukaguzi wa Ndani
 
29. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara imetekeleza yafuatayo: kutoa Mwongozo wa Kamati za Ukaguzi katika Sekta ya Umma kwa lengo la kuhakikisha utendaji wenye tija kwa Kamati zote za Ukaguzi; kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wakaguzi wa ndani 458, wajumbe wa Kamati za Ukaguzi na wadau wa ukaguzi wa ndani wapatao 567; kufanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo 11; ukaguzi wa orodha ya malipo ya mishahara; na kuhakiki madai mbalimbali yaliyowasilishwa wizarani kabla ya kulipwa. 
 
30. Mheshimiwa Spika, wizara kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali itaendelea kuimarisha ofisi za Mkaguzi Mkuu wa ndani kwa lengo la kusimamia matumizi ya fedha. Utekelezaji zaidi na malengo ya mwaka 2014/15 upo ukurasa wa 20 na 21 wa kitabu cha hotuba ya bajeti.
 
Ukaguzi wa Hesabu za Serikali
 


31.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Ofisi ya Taifaya Ukaguzi imetekeleza kazi zake kwa mujibu wa sheria. Ofisi imeendelea kuwa mshirika katika Bodi ya Ukaguzi ya Umoja wa Mataifa katika kukagua taasisi za Umoja wa Mataifa. Aidha, Ofisi imeendesha mafunzo kwa Kamati za Kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali na Kamati ya Bajeti kwa lengo la kuzijengea uwezo wa kuimarisha uwajibikaji na utawala bora. Vile vile, ukaguzi wa mapato na matumizi ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu unaendelea.
 
32.   Mheshimiwa Spika, malengo ya Ofisi ya Taifa Taifa yaUkaguzi kwa mwaka 2014/15 yanapatikana katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 21 na 22
 
Uratibu wa Utekelezaji wa MKUKUTA
 
33. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa MKUKUTA II kwa kufanya ufuatiliaji, tafiti, na tathmini na kuandaa taarifa ya utekelezaji na hali ya Umaskini nchini ili kuwezesha maamuzi ya kisera, kibajeti na
 
kiutekelezaji.  Kazi  ya  uandaaji  wa  Taarifa  ya  Mwaka  ya Utekelezaji wa MKUKUTA II imekamilika na kuwekwa katika tovuti ya Wizara. Aidha, Wizara inaendelea kukamilisha Taarifa ya Maendeleo ya Malengo ya Milenia. Taarifa ya awali inaonesha kuwa umaskini wa mahitaji ya msingi kwa Tanzania Bara ni asilimia 28.2 ambapo kwa Dar es Salaam ni asilimia 4.2, maeneo mengine ya mjini ni asilimia 21.7 na maeneo ya vijijini ni asilimia 33.3. Umaskini wa chakula ni asilimia 9.7 ambapo kwa Dar es Salaam ni asilimia 1.0, maeneo mengine ya mjini ni asilimia 8.7 na maeneo ya vijijini ni asilimia 11.3.

 
34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara imepanga kutekeleza yafuatayo: kukusanya na kuchambua taarifa mbalimbali kutoka katika Wizara, Idara na Wakala za Serikali ili kuandaa Taarifa ya mwaka ya Utekelezaji wa MKUKUTA II; kuandaa taarifa ya mwisho ya kutathimini utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia; kufanya mapitio ya MKUKUTA II; kukamilisha Mpango wa Utekelezaji wa Kinga ya Jamii pamoja na kuainisha viashiria vya upimaji juhudi za kinga ya jamii; na kuratibu mkutano wa kitaifa wa kujadili sera za kupambana na umaskini nchini. Pia Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaandaa mapendekezo ya hatua zitakazofuata baada ya MKUKUTA II kufikia kikomo mwezi Juni, 2015.


35.   Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mradi wa SELF IIimeendelea kutoa mikopo kwa wajasiriamali ambapo hadi kufikia Aprili 2014, mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 8.6 ilikopeshwa kwa wajasiriamali 4,943 kupitia Asasi ndogo 103. Kati ya waliokopeshwa, wanawake ni 2,040 sawa na asilimia 41 na wanaume ni 2,903 sawa na asilimia 59. Kwa wastani, urejeshwaji wa Mikopo ya Mradi wa SELF umeendelea kuwa wa ufanisi mzuri katika kiwango cha asilimia 90 hivyo kuwezesha fedha za mkopo kuzunguka na kuwafikia wananchi wengi zaidi.
 
36.   Mheshimiwa Spika, utekelezaji zaidi kwa mradi wa SELFpamoja na malengo ya mradi huu kwa mwaka 2014/15 yanapatikana katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 24. 
 
Sheria na Miswada ya Fedha
 
37. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria mbalimbali za Fedha kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2013 - The Finance Act, 2013. Lengo la marekebisho hayo ni kuweka usimamizi mzuri wa kodi na fedha za umma. Aidha, Sheria mbalimbali zilizopitishwa na Bunge ni pamoja na Sheria ya Mfuko wa Akiba wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu ya mwaka 2013 - The GEPF Retirement Benefit Fund Act, 2013 na marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa Bidhaa ya mwaka 2013 - The Excise (Management and Tariff) (Amendment) Act, 2013 yaliyopitishwa na Bunge katika Mkutano wa 13 mwezi Desemba, 2013 yaliyolenga kuondoa kodi ya ushuru wa bidhaa kwenye Sim Card.

 
38. Mheshimiwa Spika, utekelezaji zaidi wa sheria na miswada ya fedha pamoja na Ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ni kama unavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 25 hadi ukurasa wa 27.
 
Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi – PPP
 
39. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kupokea na kuchambua maandiko ya miradi inayokusudiwa kutekelezwa kwa utaratibu wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Katika mwaka 2013/14, Wizara imepokea na kuchambua miradi minne ya PPP. Katika uchambuzi wa miradi imebainika kwamba kuna upungufu katika upembuzi yakinifu pamoja na ukosefu wa Wataalam wa kufanya upembuzi huo. Aidha, Wizara imeshiriki kutoa mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Ubia Na. 18 ya mwaka 2010 pamoja na kanuni zake kwa lengo la kuweka usimamizi mzuri wa ubia.

 
40. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15 Wizara imetenga fedha za kuanzisha Mfuko wa Kuwezesha Utekelezaji wa Miradi ya Ubia -PPP Facilitation Fund.
 
Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi
 
41. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara kupitia Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu imepokea na kuchambua taarifa 46 za miamala shuku inayohusu fedha haramu na ufadhili wa ugaidi na taarifa 14 za kiintelijensia zimewasilishwa kwenye vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria. Aidha, mafunzo ya kudhibiti fedha haramu na ufadhili wa ugaidi yametolewa kwa watoa taarifa 135 na washiriki 86 kutoka katika vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu na Mali Athirika. Vile vile, mafunzo hayo yametolewa kwa washiriki 49 kutoka Mamlaka za Udhibiti. Kadhalika, masuala yanayohusiana na utoroshaji wa fedha nje ya nchi yanaratibiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia Kamati iliyoundwa na Serikali, na taarifa ya Kamati hiyo itapatikana baada ya kazi hiyo kukamilika.

 
42. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara kupitia Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu itatekeleza yafuatayo: kupokea na kuchambua taarifa za miamala shuku inayohusu utakasishaji wa fedha haramu na ufadhili wa ugaidi; kutoa mafunzo kwa vyombo vinavyosimamia utekelezaji wa sheria na kwa watoa taarifa; kutoa miongozo ya kudhibiti fedha haramu na ufadhili wa ugaidi kwa watoa taarifa; kuratibu zoezi la kutathmini mianya na viashiria vya fedha haramu na ufadhili wa ugaidi katika sekta mbalimbali nchini; na kuendelea na hatua za kujiunga na Umoja wa Kupambana na Biashara ya Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi Duniani - EGMONT Group of Financial Intelligence Units.

 
Tume ya Pamoja ya Fedha
 
43.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizarakupitia Tume ya Pamoja ya Fedha imekamilisha Stadi ya Kubainisha Mfumo Bora wa Kodi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na kuendelea na Uchambuzi wa Uhusiano wa Mwenendo wa Uchumi na Mapato ya Muungano.
 
44.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizarakupitia Tume ya Pamoja ya Fedha inatarajia kukamilisha Stadi ya Kubainisha Mwenendo wa Uchumi na Mapato ya Muungano wa Tanzania, na kufanya Stadi ya Uwekezaji katika Mambo ya Muungano. Aidha, Tume inatarajia kuhuisha Takwimu mbalimbali za Stadi zilizofanywa na Tume.
 

Habari, Elimu na Mawasiliano kwa Umma
 
45. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa wizara juu ya habari, elimu na mawasiliano kwa umma pamoja na masuala ya watumishi yanapatikana katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa 28 hadi ukurasa wa 30.
 
Usimamizi wa Mashirika na Taasisi za Umma
 
46. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imechambua na kutangaza katika Gazeti la Serikali mashirika 10 ambayo yanatakiwa kuchangia asilimia 10 ya mapato ghafi katika Mfuko Mkuu wa Serikali. Hadi kufikia Aprili 2014, kiasi cha shilingi bilioni 25.0 kimekusanywa ikiwa ni asilimia 69.4 ya makadirio ya kukusanya shilingi bilioni 36 kwa mwaka 2013/14. Aidha, katika kutekeleza zoezi la kuingia mikataba ya utendaji na Bodi za Mashirika ya Umma, Wizara inakamilisha majadiliano na Bodi za Mashirika ya Umma. Vile vile, zoezi la kumpata Msajili wa Hazina limefikia hatua za mwisho. Matarajio ni kwamba uteuzi utafanyika kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.

47.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizarainatarajia kutekeleza yafuatayo: kusimamia utendaji wa Bodi za Wakurugenzi wa mashirika na taasisi za umma na kuingia mikataba ya utendaji na Bodi za mashirika ya umma; kusimamia mikakati ya kurekebisha mashirika ya umma na kufanya tathmini na ufuatiliaji wa mashirika ya umma yaliyobinafsishwa; na kuimarisha usimamizi wa mashirika na taasisi za umma ili kuongeza mapato ya Serikali.

48.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizarakupitia Shirika Hodhi la Mali za Umma (CHC) imeendelea na zoezi la ubinafsishaji na urekebishaji wa mashirika ya Umma. Wizara inaendelea na zoezi la tathmini ya utendaji wa mashirika mengine yaliyobinafsishwa kwa lengo la kufahamu kama makubaliano ya mikataba ya mauzo yanazingatiwa na kuchukua hatua stahiki.
 
Mafao ya Wastaafu na Mirathi
 
49.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuboreshakumbukumbu za Wastaafu, kulipa mafao na michango ya kisheria kwa wakati. Hadi Aprili 2014, kumbukumbu za wastaafu 142,014 zimehifadhiwa kwenye mfumo wa kompyuta (SAPERION) na shilingi bilioni 220.79 sawa na asilimia 87 ya makadirio kimelipwa kama mafao ya wastaafu wanaolipwa pensheni na Hazina. Aidha, Wizara imefanya uhakiki wa wastaafu walio kwenye daftari la Hazina katika mikoa tisa. Vile vile, shilingi bilioni 522.86 sawa na asilimia 76 ya makadirio ya mwaka kimelipwa kama michango ya mwajiri kwa watumishi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa wanaochangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na michango ya Bima ya Afya.
 
50.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kusimamia nakuratibu shughuli za Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni wa PPF na Mfuko wa Mafao ya Kustaafu (GEPF). Utekelezaji kwa mwaka 2013/14 ni kama unavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 31 hadi ukurasa wa 34.
 
Mamlaka ya Mapato Tanzania
 
51.   Mheshimiwa Spika, hadi kufikia Aprili 2014, mapato halisiya kodi yalifikia shilingi bilioni 7,771.5 sawa na asilimia 75 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 10,395.4. Kodi zilizochangia zaidi ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani, Kodi ya Kampuni na Kodi ya Mapato ya Ajira ambazo kwa pamoja zilichangia zaidi ya asilimia 80 ya mapato hayo.
 
52.   Mheshimiwa Spika, licha ya hatua mbali mbali ambazozimechukuliwa katika kipindi cha mwaka 2013/14, kumekuwa na changamoto katika kufikia lengo la makusanyo ya mapato. Sababu zilizochangia kutofikia malengo ni pamoja na: mapato pungufu ya Kodi ya Kampuni kuliko ilivyotarajiwa kutoka kwenye baadhi ya kampuni za madini; na kushuka kwa makusanyo hususan Kodi ya Zuio kutokana na kupungua kwa makusanyo kwenye shughuli za utafiti wa gesi na mafuta. Sababu nyingine ni pamoja na kufutwa kwa Tozo ya Kadi za Simu - SIMcard levy na makusanyo hafifu kutoka kwenye Ushuru wa Bidhaa wa Huduma za Uhawilisho wa Fedha - Money Transfers. Kwa upande wa Forodha sababu zilizochangia kutofikiwa kwa lengo la makusanyo ni ukuaji mdogo wa uingizwaji wa bidhaa kutoka nje, na ongezeko la kuingiza bidhaa kupitia njia zisizo rasmi(panya roads) na bandari bubu..
 
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kudhibiti ukwepaji kodi,wizara kupitia TRA inachukua hatua kadhaa za kudhibiti upotevu wa mapato kupitia bandari bubu na panya roads, kwa kufanya upelelezi ili kuzigundua njia hizo na kuzidhibiti kwa kutumia Kikosi Kazi cha Kuzuia Magendo (Flexible Anti-Smuggling Team). Aidha, elimu kwa wafanyabiashara na wananchi wanaozunguka eneo la Pwani imeendelea kutolewa, ushirikiano na vyombo vingine vya udhibiti yaani Polisi Uhamiaji na Usalama wa Taifa umeanzishwa; na kufanya doria katika maeneo hayo.
 
53. Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuimarisha makusanyo ya kodi, Mamlaka imeendelea kufanya yafuatayo: kuimarisha matumizi ya Mashine za Kieletroniki za kutoa Risiti -
 
Electronic Fiscal Devices (EFDs) ambapo kwa sasa inakamilisha zoezi la kuwaingiza wafanyabiashara wote wanaostahili kuanza kutumia mashine hizo; kuanzisha Mfumo wa Uthamini wa Mizigo ya Forodha - Tanzania Customs Integrated System (TANCIS) ambao umeanza kutumika mwezi Aprili 2014 pamoja matumizi ya mfumo wa kuthamini magari chakavu; na kuanzisha Kitengo cha Kodi ya Kampuni za Kimataifa - International Tax Unit kwa lengo la kubaini na kudhibiti mianya ya kupotea kwa kodi inayolipwa na kampuni za kimataifa zilizowekeza nchini.
 
54. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania imeanza kutekeleza makubaliano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuweka mazingira ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Himaya Moja ya Forodha (Single Customs Territory - SCT) kuanzia Januari, 2014. Ili kuhakikisha kwamba mizigo ya nchi jirani haiuzwi nchini kinyume na utaratibu wa forodha, mfumo wa ki-eletroniki wa ufuatiliaji wa mizigo inayosafirishwa utatumika. Kupitia mfumo huu, mizigo na ama vyombo vya usafirishaji hufungwa lakili ya ki-eletroniki (electronic seal) na kifaa cha mawasilaino ambavyo huunganishwa na mfumo mkuu ili kuonesha mwenendo mzima wa usafiri hadi mzigo husika utakapovuka mpaka wa nchi. Aidha, mbinu nyingine za udhibiti saidizi kama doria, usuluhishi wa taarifa (reconciliation) na ukaguzi zitatumika ili kuongeza udhibiti.
 
Rufaa za Kodi
 
55. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa rufaa za kodi ni kama unavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 35 na 36.
 
Huduma za Kibenki
 
Benki Kuu ya Tanzania
56. Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Benki Kuu imeendelea kusimamia Sekta ya Kibenki ambapo kati ya kipindi cha Machi 2013 na Machi 2014, idadi ya benki na taasisi za fedha imeongezeka kutoka 51 na matawi 585 hadi 53 na matawi 625 kote nchini. Jumla ya mali ya sekta ya kibenki imekua kutoka shilingi trilioni 17.9 hadi shilingi trilioni 21.1. Kiwango cha mitaji kilifikia wastani wa asilimia 18.5 ikilinganishwa na kiwango cha asilimia 10 kinachotakiwa kwa mujibu wa sheria. Aidha, Mfumo wa Taarifa za Wakopaji - Credit Reference Bureau unaendelea vyema, ambapo hadi sasa kampuni mbili zimepewa leseni ambazo ni: kampuni ya Creditinfo Tanzania Limited iliyoanza kazi Juni 2013 na kampuni ya Dun & Bradstreet Credit Bureau
 
(T) Limited iliyoanza kazi Septemba 2013. Kampuni nyingine kwa jina la Transunion, nayo hivi karibuni imepewa leseni ya muda na inajiandaa kuanza kufanya kazi.

57.   Mheshimiwa Spika, Kampuni hizi kwa sasazinaandaataarifa za wateja kutoka kwenye kumbukumbu ambazo zinahifadhiwa Benki Kuu. Taarifa hizi bado zinafanyiwa uhakiki kabla ya kuanza kutumika rasmi. Mara baada ya data bank hiyo kukamilika, makampuni haya ya Credit Reference yataanza kufanya kazi hiyo kikamilifu na kwa usahihi. Benki Kuu inaendelea kuyahimiza mabenki ambayo bado hayajawasilisha taarifa kufanya hivyo.
 
58.   Mheshimiwa Spika, Tarehe 30 Novemba 2013, Marais waAfrika Mashariki walitia sahihi Itifaki ya Umoja wa Fedha ya Afrika Mashariki. Tukio hili, ndilo limeanzisha safari yetu ya kwenda kwenye hatua ya kuwa na sarafu moja ifikapo mwaka 2024. Chini ya Itifaki hii, tumekubaliana vigezo ambavyo tutatakiwa tufikie kabla ya kuingia kwenye umoja huo na road map ya miaka 10 ambayo itaanza kutekelezwa mara tu baada ya nchi zote kuridhia utekelezaji wake. Katika mpango huo, mambo muhimu ni; kukamilisha utekelezaji wa Umoja wa forodha na Itifaki ya soko la pamoja; kuoanisha mifumo ya kifedh, sera za ubadilishaji wa fedha za kigeni, sera za bajeti, na mifumo ya malipo; uhuisha mifumo ya takwimu na; kuhuisha sheria zote zinazohusiana na uanzishwaji wa umoja wa kifedha

 
Benki ya Maendeleo TIB
 
59. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, TIB Development Bank (zamani Benki ya Rasilimali) iliendelea na marekebisho ya ndani ambapo shughuli za Benki zimegawanywa katika kampuni mbili ambazo ni TIB Development Bank Limited inayohusika na shughuli za maendeleo na TIB Corporate Finance Limited inayohusika na shughuli za biashara.

 
60. Mheshimiwa Spika, maelezo ya utekelezaji wa majukumu ya Benki ya Maendeleo TIB, Benki ya Maendeleo ya Kilimo, Twiga Bancorp na Benki ya Posta kwa mwaka 2013/14 ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 37 hadi ukurasa 40.
 
Benki ya Maendeleo ya Kilimo - TADB
 
61. Mheshimiwa Spika, kufuatia uamuzi wa Serikali kuanzisha Benki ya Kilimo, Wizara imetekeleza yafuatayo: kuzindua Bodi ya Wakurugenzi wa Benki; kukamilisha zoezi la upatikanaji wa Mtendaji Mkuu na Wakuu wa Idara; kuandaa Muundo wa Benki na Muundo wa Utumishi; kuandaa majukumu ya wafanyakazi; kuandaa rasimu ya Mpango wa Biashara; na kupatikana kwa ofisi za Benki. Mwaka 2014/15, Benki ya Maendeleo ya Kilimo inatarajia kupata leseni ya biashara, kuajiri wafanyakazi na kuanza kutoa huduma.

Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Kifedha
 
62. Mheshimiwa Spika, Wizara imeanza kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Kifedha - National Microfinance Policy, 2000 ili kuondoa mapungufu ya kisheria yaliyojitokeza katika utekelezaji wake kwa lengo la kuzingatia mabadiliko ya kiuchumi na kijamii pamoja na kuweka mazingira mazuri katika ukuaji wa sekta hiyo. Aidha, katika mwaka 2014/15, Wizara itakamilisha maandalizi ya Sera ya Taifa ya Taasisi Ndogo za Huduma za fedha pamoja na kutunga Sheria ya Taasisi ndogo za huduma za kifedha - Microfinance Act.
 
Huduma za Bima
 
Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima – TIRA
 
63. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima imekamilisha na kutoa Mkakati wa Kuendeleza Bima ya Watu wa Kipato cha Chini - National Micro Insurance Strategy 2014-2017. Aidha, hadi kufikia Aprili 2014, kampuni 30, madalali 100 na mawakala 500 wa bima walisajiliwa. Vile vile, mauzo ya bima yaliongezeka kwa asilimia 18.5 hadi kufikia shilingi bilioni 481.7 ukilinganisha na shilingi bilioni 406.7 ambazo ni mauzo ya mwaka uliopita.

 
64. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, TIRA inatarajia kutekeleza yafuatayo: kuendelea na maandalizi ya kufungua ofisi nyingine za kanda; kuendelea na utaratibu wa uoanishaji (harmonise) sheria na kanuni za soko la bima katika eneo la Afrika Mashariki na lile la nchi za SADC; kuendelea na tafiti za bima ya kilimo, mifugo, pamoja na bima za watu wa kipato cha chini (micro – insurance); na kukamilisha taratibu za kuanzisha bima ya Takaful.
 
Shirika la Bima la Taifa – NIC
 
65. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2013/14, Wizara ilikamilisha urekebishaji wa Shirika la Bima la Taifa na usimikaji wa mfumo wa TEHAMA kwa lengo la kuongeza ufanisi. Utendaji wa Shirika kibiashara uliendelea kuimarika ambapo mapato ya bima yaliongezeka kutoka shilingi bilioni 27.38 mwaka 2012, hadi kufikia shilingi bilioni 31.53 mwaka 2013, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 15. Mapato haya yalitokana na makusanyo ya bima za mtawanyo, vitega uchumi na mapato mengine. Utekelezaji zaidi na malengo kwa mwaka 2014/15 yapo ukurasa wa 41 wa kitabu cha hotuba ya bajeti.

 
Masoko ya Mitaji na Dhamana
 
66.   Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa majukumu yaMamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana, Soko la Hisa Dar es Salaam na Dhamana ya Uwekezaji Tanzania pamoja na malengo kwa mwaka 2014/15 ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti ukurasa wa 42 hadi ukurasa wa 46.
 
67.   Mheshimiwa Spika, kuhusu credit rating, wizara ikokatika hatua za mwisho za kupata taasisi mbili zitakazoendesha zoezi la tathmini ya kupima uwezo wa nchi wa kukopa na kulipa madeni yake. Mwezi Februari 2014, Wizara iliziandikia kampuni za Fitch, Moody’s Investment Services na Standard and poors kuwasilisha fomu zao za mikataba kwa hatua za uchambuzi.
 
Tayari  kampuni  ya  Fitch  na  Moody’s  zimewasilisha  fomu  za mikataba kupitia kwa mshauri mwelekezi Citi Group. Aidha, kuchelewa kwa zoezi hili kulitokana na kampuni hizi za upimaji (Rating Agencies) kutokukubaliana na aina ya fomu za mikataba zinazoandaliwa na serikali pamoja na kuleta nyongeza ya gharama nje ya makubaliano yaliyosainiwa awali.

 
Taasisi za Kitaalam na Huduma Nyinginezo
 
68. Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa majukumu kwa mwaka 2013/14 pamoja na mipango kwa mwaka 2014/15 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu, Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, Bodi ya Michezo ya Kubahatisha pamoja na taasisi za mafunzo za Taasisi ya Uhasibu Arusha, Chuo cha Usimamizi wa Fedha, Taasisi ya Uhasibu Tanzania, Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba ya bajeti kuanzia ukurasa wa 46 hadi ukurasa wa 52.
 

CHANGAMOTO
 
69. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara ilikabiliwa na changamoto zifuatazo:
 
i.        Kuongeza mapato ya ndani ya Serikali ili kukidhi mahitaji ya matumizi ya maendeleo na ya kawaida;
 
ii. Mabadiliko ya hali ya uchumi na uongozi katika nchi za washirika wa maendeleo ambapo zimepelekea kushindwa kutimizwa kwa baadhi ya miadi;
 
iii.  Uwezo wa kusimamia mikataba katika kutekeleza baadhi ya miradi na programu za maendeleo; na
 
iv. Upatikanaji wa mikopo ya kibiashara kwa wakati kunakotokana na kubadilika kwa masharti kutoka kwa wakopeshaji.
 
70.       Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamotohizo, Wizara imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na:
 
i.        Kubuni vyanzo vipya vya mapato na kudhibiti matumizi pamoja na kupunguza upotevu wa mapato;

ii.        Kuboresha ushirikiano na washirika wa maendeleo yenye lengo la kuwa na uelewa sawa kuhusu masuala mbali mbali katika ushirikiano wetu;
 
iii.        Kuendelea kuzijengea uwezo Wizara, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kusimamia na kutekeleza mikataba ya miradi na programu za maendeleo;
 
iv.        Kuendelea kutekeleza Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma - “Public Financial Management Reform Programme (PFMRP)”; na
 
v.        Kushauri Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuzingatia vipaumbele wakati wa kupanga na utekelezaji kulingana na bajeti iliyotengwa.
 
vi.        Kuanza mazungumzo mapema na wakopeshaji wa mikopo ya kibiashara.
 
Mapitio ya Mapato na Matumizi ya Mafungu ya Wizara kwa Mwaka 2013/14
 
71. Mheshimiwa Spika, mapitio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2013/14 ya mafungu ya wizara ya fedha ambayo ni fungu 7,10,13,21,22,23 na 50 pamoja na fungu 45 ni kama inavyooneshwa katika kitabu cha hotuba kuanzia ukurasa wa 52 hadi ukurasa wa 56.

 
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2014/15
 
Mapato
 
 
72. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/15, Wizara ya Fedha Fungu 50 inakadiria kukusanya mapato yasiyo ya kodi yapatayo shilingi 126,188,104,000 (bilioni 126.19)
 
Maombi ya Fedha
 
 
Fungu 50 – Wizara ya Fedha.
 
73. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
 

(a) Matumizi ya kawaida Shilingi 66,239,790,000 (bilioni 66.23). Kati ya hizo mishahara ni shilingi shilingi 5,620,668,000 (bilioni 5.62) na matumizi mengineyoshilingi 60,619,122,000 (bilioni 60.61).
 
(b) Miradi ya Maendeleo Shilingi 29,803,232,000 (bilioni 29.71).Kati ya hizo:
 
(i) Fedha za Ndani - Shilingi 19,350,000,000 (bilioni 19.35).
 
 
(ii) Fedha  za  Nje  -  Shilingi  10,453,232,000  (bilioni 10.45).
 
 
Fungu 23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali:
 
74. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
 
(a)       Matumizi ya kawaida - Shilingi 82,170,024,000 (bilioni 82.17). Kati ya hizo mishahara shilingi 5,012,762,000 (bilioni 5.01) na matumizi mengineyo shilingi 77,157,262,000 (bilioni 77.16).
 
 

(b) Miradi ya Maendeleo Shilingi 7,950,000,000 (bilioni 7.95) Kati ya hizo:
 
(i) Fedha  za  Ndani  -Shilingi  4,800,000,000  (bilioni 4.80).
 
 
(ii) Fedha  za  Nje    -Shilingi  3,150,000,000  (bilioni 3.15).
 
 
Fungu 22- Deni la Taifa
 
75. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 4,354,865,076,000 (bilioni 4,354.86). Kati ya hizomishahara ni shilingi 10,341,136,000 (bilioni 10.34), Deni la Taifa shilingi 3,650,612,000,000 (bilioni 3,650.61) namatumizi mengineyo ni shilingi 693,911,940,000 (bilioni 693.91).
 

 
Fungu 21 - HAZINA
 
76. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a) Matumizi ya kawaida Shilingi 790,325,216,000 (bilioni 790.32). Kati ya hizo mishahara ni shilingi 4,015,511,000 (bilioni 4.01) na matumizi mengineyoshilingi 786,309,705,000 (bilioni 786.31) ambazo ni kwa ajili ya matumizi ya Idara na Taasisi zilizo chini ya Fungu hili, nyongeza ya mishahara ya Watumishi wa Serikali na matumizi maalum.
(b)       Miradi ya maendeleo ni shilingi 57,417,015,000 (bilioni 57.42). Kati ya hizo;
 
(i)  Fedha za Ndani- Shilingi 17,000,000,000 (bilioni 17.0)
 
 
(ii) Fedha  za  Nje-  Shilingi  40,417,015,000  (bilioni 40.42)
 
 

Fungu 13 –  Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu:
 
77. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
(a) Matumizi ya kawaida - Shilingi 2,000,000,000  (bilioni 2.0).
 
 
(b) Miradi ya Maendeleo, fedha za nje Shilingi 195,000,000 (bilioni 0.19).
 
 
Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha:
 
78. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 2,318,661,000 (bilioni 2.32) kwa matumizi ya kawaida. Katiya fedha hizo, shilingi 318,661,000 (bilioni 0.32) ni kwa ajili 
ya mishahara na shilingi 2,000,000,000 (bilioni 
2.0) ni
matumizi mengineyo.
 
 

Fungu 7 – Ofisi ya Msajili wa Hazina:
 
79. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2014/15, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
 
 
(a) Matumizi ya kawaida - Shilingi 88,455,278,000 (bilioni 88.45). Kati ya hizo shilingi 670,328,000 (bilioni 0.67)   ni   kwa ajili   ya   mishahara   na   shilingi 87,784,950,000 (bilioni 87.78) ni matumizimengineyo.
 
 
(b) Miradi ya Maendeleo Shilingi 1,943,000,000 (bilioni 1.94) Kati ya hizo:
 
(i) Fedha  za  Ndani  –Shilingi  650,000,000  (bilioni 0.65).
 
 
(ii) Fedha  za  Nje   -Shilingi  1,293,000,000  (bilioni
 
1.29).
 
Fungu 45 - Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi

 
 
80. Mheshimiwa Spika, katika fungu hili kwa mwaka wa fedha 2013/14, Wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha fedha kama ifuatavyo:
 
  
(a)    Matumizi ya kawaida shilingi 69,843,825,000 (bilioni 69.84). Kati ya hizo mishahara ni shilingi 10,408,402,000 (bilioni 10.41) na matumizi mengineyoshilingi 59,435,423,000 (bilioni 59.43).
 
(b)    Miradi ya maendeleo shilingi 13,011,432,000 (bilioni 13.01), kati ya hizo:
 
(i)        Fedha  za  ndani  shilingi  8,000,000,000  (bilioni
 
8.0).
 
(ii)  Fedha  za  nje  shilingi             5,011,432,000  (bilioni
 
5.01).
 
HITIMISHO
81. Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Wakuu wa Idara na Vitengo, Wafanyakazi wa Wizara ya Fedha wakiongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Servacius B. Likwelile na Naibu Makatibu Wakuu Ndugu Elizabeth J. Nyambibo, Prof. Adolf F. Mkenda na Ndugu Doroth S. Mwanyika kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Vile vile, napenda kuwashukuru Wakuu wa Taasisi na Wakala wa Serikali chini ya Wizara kwa michango yao katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

 

82.       Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuruWaheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Hotuba hii pia inapatikana katika tovuti ya Wizara ( www.mof.go.tz)

 
83.       Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja
(A.I)

No comments:

Post a Comment