Dk Salim: Sina mpango na urais 2015  
            
Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Dk
 Salim Ahmed Salim amesema hana mpango na hafikirii tena kuwania urais 
katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Akizungumza katika mahojiano maalumu 
na gazeti hili nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam jana, Dk Salim 
alisema alipowania nafasi hiyo mwaka 2005, hakuwa na ufahamu mzuri 
kuhusu mchakato huo lakini baadaye alibaini kwamba, mbali na rekodi ya 
utendaji, kuna mambo mengine yanayohitajika katika kinyang'anyiro hicho 
na kwamba hata watu wanaomfikiria na kutaja jina lake miongoni mwa 
wanaoweza kuwania tena nafasi hiyo, wanakosea.
"Sifikirii tena, hii ni zamu ya kizazi
 kingine. Ila nitaendelea kuisaidia nchi yangu katika nyanja mbalimbali 
kadri ya uwezo wangu," alisema.
Dk Salim ambaye mbali na uwaziri mkuu 
amewahi kushika nafasi nyingine mbalimbali kitaifa na kimataifa, alisema
 uzoefu alioupata katika kinyang'anyiro cha urais unatosha.(E.L).
         
                        
        
        
        
            
Alipoulizwa kama uzoefu huo ni mbaya au mzuri kwake, alisema ni mchanganyiko.
Dk Salim aliwahi kugombea nafasi ya 
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) na kushindwa kutokana na kura ya 
veto ya Marekani, pia aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi
 Huru za Afrika (OAU), sasa Umoja wa Afrika (AU). Pia aliwahi kuwa Rais 
wa Bunge Kuu la UN mwaka 1979 na 1980.
Licha ya kujitokeza mara moja kuomba 
uteuzi wa CCM kuwania urais 2005, nyota yake katika nafasi hiyo ilianza 
kuwaka tangu mwaka 1985 akiwa Waziri Mkuu pale aliposhindanishwa katika 
Kamati Kuu ya CCM na aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashidi Kawawa pamoja 
aliyekuwa Makamu wa Rais wakati huo, Ali Hassan Mwinyi ambaye 
alipitishwa kiitifaki na kushinda kiti hicho.
Akizungumza na gazeti hili hivi 
karibuni, Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa alisimulia jinsi
 Mwinyi alivyopita, kwa sababu alikuwa Makamu wa Rais, hivyo wajumbe wa 
Kamati Kuu walikosa hoja na sababu za kumwacha na kumchukua Waziri Mkuu 
aliyekuwa chini yake kiitifaki.
"Makamu wa Rais ukimruka maana yake hatoshi, wakaona hawana maelezo hayo, ikabidi wamteue Mwinyi," alisema Msekwa.
Sifa za viongozi
Katika hatua nyingine, Dk Salim 
alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuandaa viongozi hasa mtu anayekwenda 
kushika nafasi ya urais atakayekwenda sambamba na mahitaji ya kizazi cha
 sasa alichokiita cha 'dot com'.
"Hapa sizungumzii viongozi wa CCM au 
wa Chadema au chama kingine, nazungumzia viongozi wa nchi watakaoweza 
kufanyia kazi matatizo ya Watanzania.
"Ni vizuri viongozi wakaandaliwa, 
isiwe mtu anaibuka tu anagawa hela halafu anashinda. Anatakiwa mtu 
atakayeweza kushughulikia matatizo hayo. Watanzania ni wapole na 
wavumilivu lakini wanazungumza. Hivyo anahitajika kiongozi 
atakayesikiliza mahitaji yao na kutoa suluhisho, si kutoa ahadi za 
uongo," alisema. Dk Salim alisema katika kipindi hiki, anahitajika 
kiongozi atakayekuwa juu ya tofauti za kisiasa, kidini, asili.
"Unajua hapa nchini kama ilivyo mahali
 pengine, ukiingiza mgawanyiko wa kidini wakati familia nyingi zina watu
 wa dini tofauti, wote wataathirika."
Viongozi na rushwa
Akizungumzia tatizo la rushwa, Dk Salim alisema ni kubwa na kadri linavyoongezeka, linakuwa adui wa uwajibikaji, demokrasia.
Alisema katika enzi za utumishi wake 
nje ya nchi, alikuwa akiona rushwa ilivyokithiri katika nchi mbalimbali,
 lakini hapa nyumbani pakiwa salama hadi akawa anasema Tanzania ina 
bahati, kauli ambayo hawezi kuisema sasa.
Dk Salim alibainisha kuwa uongozi 
unaoingia madarakani kwa rushwa hauwezi kuwa mzuri kwa nchi na athari 
zake zinaonekana hadi ngazi ya chini katika huduma za jamii kama 
mahakamani, polisi na hospitalini.(E.L)