WARIOBA : JADILINI RASIMU SI TUME
MWENYEKITI
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amewataka
wanasiasa kujielekeza katika kuijadili rasimu ya Katiba iliyotolewa
badala ya kuijadili tume na wajumbe wake.
Jaji
Warioba alisema tume yake siku zote imekubali kukosolewa kwa kuamini
kuwa ni jambo la kawaida lakini akaongeza kwamba ni vema wananchi na
wanasiasa wakajadili rasimu ya Katiba iliyotolewa. (hd)
"Nadhani wangezungumzia rasimu wangetusaidia sana, badala ya kuzungumzia tume na watu.
"Na siamini kama kauli za viongozi hao wa kisiasa ndiyo misimamo ya vyama vyao," alisema.
Jaji
Warioba alitoa kauli hiyo jana wakati akikanusha tuhuma zilizoelekezwa
kwa tume yake na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi
(CCM), Abdallah Bulembo, kwamba tume hiyo imeacha kutekeleza majukumu
yake na kuingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni.
Alisema
kuwa siku zote tume yake imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa
kuzingatia sheria na kuwataka wanasiasa hao kujadili rasimu iliyotolewa
badala ya kuishambulia tume au wajumbe wake.
"Moja ya kazi za kisheria za tume ni kutoa elimu kwa umma, na ni kazi ya wakati wote," alisema.
Bulembo
alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari juzi akiwa mkoani Tanga
ambapo alisema kuwa Tume ya Warioba imeacha kutekeleza majukumu yake na
kuingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni.
Akijibu
upotoshaji huo, Jaji Warioba alisema kuwa katika mikutano ya mabaraza ya
Katiba ya Wilaya, wananchi ambao walikuwa ni wajumbe wa mabaraza hayo
walikuwa na fursa ya kuuliza maswali na wajumbe wa tume walitoa elimu
kuhusu hoja na maswali yaliyoulizwa kwa mujibu wa sheria.
"Sasa
Bulembo anaona kutoa elimu ni dhambi?" aliuliza Warioba ambaye amewahi
kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa
Rais.
Jaji
Warioba alikumbusha kuwa tume yake imekuwa ikifanya kazi katika
mazingira magumu kutokana na kauli za wanasiasa mbalimbali na kuongeza
kuwa pamoja na kauli hizo tume yake inafarijika na kauli za kutia moyo
wanazozipata kutoka kwa wananchi wa kawaida.
"Nilisema
mwishoni mwa mwezi uliopita wanasiasa wamekuwa wakitoa matamshi
yaliyoifanya kazi ya tume kuwa ngumu katika mikutano ya mabaraza ya
Katiba.
"Matamshi
mengine yalilenga tume na wakati mwingine yalinilenga mimi binafsi au
wajumbe wa tume badala ya kuzungumzia rasimu," alisema.
No comments:
Post a Comment