TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Tuesday, October 1, 2013

SERIKALI KUANZA UCHIMBAJI WA MADINI YA URANI

msemaji_9fa2a.jpg
Naibu Kamishna wa Madini toka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Ally Samaje (KULIA) Akieleza kwa waandishi wa Habari kuhusu uanzishwaji wa Mradi wa Uchimbaji Madini ya Urani eneo la mto Mkuju, Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma, wakati wa Mkutano uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Idara ya Habari(MAELEZO).Kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Assa Mwambene.
Picha na Georgina Misama-Maelezo(P.T)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
UANZISHAJI WA MRADI WA UCHIMBAJI MADINI YA URANI ENEO LA MTO MKUJU, WILAYA YA NAMTUMBO
Utangulizi
Kulingana na shughuli za utafutaji madini zilizofanywa miaka ya nyuma hadi sasa zimebainisha madini ya urani kuwepo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Maeneo hayo ni pamoja na Mto Mkuju (Namtumbo); Madaba (Liwale); Bahi (Dodoma); Gallapo (Babati); Milima ya Uluguru (Morogoro); na Itigi (Manyoni). Madini hayo yanaweza kugundulika katika maeneo zaidi kutokana na shughuli za utafutaji zinazofanywa pamoja na taarifa zaidi za kijiolojia zinazoendelea kutayarishwa na Wakala wa Jiolojia Tanzania. Hata hivyo, hadi sasa eneo la Mto Mkuju ndilo limeonekana kuwa na mashapo ya madini ya urani yanayoweza kuchimbwa kibiashara. Pamoja na matokeo ya awali kuonesha kuwa yapo madini ya urani yanayoweza kuchimbwa kibiashara bado utafutaji zaidi unahitajika ili kupata mashapo zaidi yatakayoweza kuchimba kwa muda mrefu.
Mradi wa Urani wa Mto Mkuju
Kulingana na utafiti wa kina wa madini ya urani uliofanywa katika eneo la mradi huu umegundua mashapo yanayoweza kuchimbwa kibishara. Hadi sasa kiasi cha tani milioni 175.8 za mashapo (Measured, Indicated na Inferred) ya urani kimegunduliwa. Kiasi hicho ni sawa na pound milioni 115.8 (kilo milioni 52.5) za urani kwa grade ya 298.8 U3O8ppm. Kulingana na mashapo haya uhai wa mgodi kwa sasa ni miaka 12.
Mradi wa Mto Mkuju unamilikiwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Limited, Kampuni tanzu ya URMZ ya Urusi. Kampuni ya URMZ ni Kampuni ya Serikali ya urusi. Mradi wa Mto Mkuju uko ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Selous (Selous Game Reserve). Pia eneo hilo ni Sehemu ya Urithi wa Dunia (World Heritage Site). Mwezi Julai, 2012, World Heritage Committee iliyoko chini ya UNESCO ilitoa idhini ya kuondoa eneo la Mradi wa Mto Mkuju kwenye Eneo la Urithi wa Dunia ili uchimbaji wa urani uweze kufanyika. Hata hivyo, eneo hilo litaendelea kuwa ndani ya eneo la Hifadhi ya Wanyamapori la Selous.
Kutokana na hatua hiyo, uchambuzi wa masuala ya mazingira ulikamilika mwezi Oktoba, 2012 ambapo Hati ya Mazingira (Environmental Impact Assessment Certificate) ilitolewa na Baraza la mazingira la Taifa (NEMC). Baada ya hatua hizo kukamilika, Wizara ya Nishati na Madini ilitoa leseni ya uchimbaji madini ya urani tarehe 05 Aprili, 2013. Leseni hiyo inaruhusu shughuli za uchimbaji kufanyika katika mradi huo. Majadiliano kuhusu mkataba wa kuendeleza uchimbaji madini kuhusu mradi huo yanaendelea.
Uchimbaji wa madini ya urani katika mradi wa Mto Mkuju utafanyika hadi hatua ya yellow cake. Baada ya hapo urani hiyo itasafirishwa kwenda nje ya nchi katika maeneo ambayo urutubishaji wa madini hayo kwa matumizi mbalimbali kama vile kuzalisha umeme, kutengeneza vifaa vinavyotumika kwenye sekta za Afya, Kilimo, Ujenzi na Mifugo utafanyika.
Manufaa mbalimbali yanatarajiwa kutokana na uchimbaji wa urani katika mradi huo ikiwa ni pamoja na mrabaha (Dola za marekani zaidi ya milioni 190); Kodi (Dola za Marekani zaidi ya milioni 363); PAYE (Dola za marekani zaidi ya milioni 50). Mapato mengine ni pamoja na Kodi ya zuio (Withholding taxes), gawio (dividend), Import duties, Service levy kwenye Halmashauri ya Namtumbo, n.k. Hata hivyo, mapato haya yatatokana na hali ya bei ya urani katika soko la dunia. Manufaa mengine ni ajira kwa watanzania zaidi ya 690.
Udhibiti wa shughuli za urani
Tungependa kuwahakikishia Watanzania na wananchi wanaoishi karibu na maeneo yaliyogundulika kuwepo na madini ya urani kwa kiwango cha kuchimbwa kibiashara, kwamba Serikali imechukua hatua kadhaa za kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya shughuli za utafutaji, uchimbaji na usafirishaji nje ya nchi madini ya urani. Hatua hizo ni pamoja na zifuatazo:-
Kuwepo kwa Sheria za Madini, 2010 ambapo madini ya urani na madini mengine yanayotumika kuzalisha nishati, mfano makaa ya mawe yanatambuliwa kama kundi pekee la energy minerals. Tofauti na madini mengine, sheria imezuia utoaji wa leseni ya biashara ya madini (Dealer Licences) kwa madini ya urani kutokana na unyeti wa madini hayo.Kuwepo kwa Kanuni maalum za the Mining (Radioactive Minerals) Regulations, 2010 zimetungwa (GN. 407 dated 22/10/2010) kuhakikisha kuwa kampuni zinazowekeza katika utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani zinafuata maelekezo maalum yanayohusu utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji, usafirishaji na uuzaji wa madini hayo. Vilevile, Kanuni hizo zinaelezea majukumu ya mamlaka mbalimbali ikiwa ni pamoja na taasisi za TAEC na NEMC, na Wizara zinazosimamia rasilimali za Maji na Madini. Madhumuni makuu ni kuhakikisha kuwa shughuli hizo haziathiri usalama, afya na mazingira yetu na uhusiano wetu na jumuia za kimataifa, ikiwa ni pamoja na IAEA.
Kuwepo kwa Sheria na kanuni chini ya Tanzania Atomic Energy Commission (TAEC) ambazo zinahakikisha kuwa kunakuwepo na uthibiti wa viwango vya mionzi ambavyo vinaweza kuathiri binadamu. Aidha, watahakikisha kuwa ufungaji katika mapipa na usafirishaji wa urani unafanyika kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vinavyokubalika.
Kanuni za Usalama, Afya na Mazingira Migodini zilizotungwa kwa GN Na. 408 ya tarehe 22/10/2010 zimehifadhi kanuni namba 187 – 190 zilizokuwa kwenye kanuni za mwaka 1999 zinazokusudia kusimamia usalama wa shughuli za utafutaji wa madini ya urani na mengineyo yenye mionzi ayonisha. Kanuni hizo zimeweka mfumo wa kushirikisha jamii inayozunguka maeneo yanayofanyiwa utafiti wa madini hayo.
Taarifa Potofu kuhusu urani
Wapo watu mbalimbali hasa Wanaharakati kama vile Mtaalam wa Uranium Network Organization ya Ujerumani Bw. Gunter Wippel ambao wamekuwa wakieneza taarifa potofu kuwa uchimbaji wa madini ya urani nchini Tanzania utasababisha madhara mbalimbali ikiwa ni pamoja na:-
a) Kansa ya ini;
b) Kuzaliwa watoto wenye viungo pungufu au zaidi; na
c) Kubadilika kwa DNA.
Madai hayo sio ya kweli ukizingatia kuwa Tanzania baada ya kuyachimba madini hayo na kuyasafisha kwa kiwango cha yellow cake haitaendelea na hatua zinazofuata za kurutubisha madini hayo na kuyafikisha katika kiwango na mfumo wa kuwezesha kuzalisha umeme ama kutengeneza vifaa vinavyotumika kwenye sekta za Afya, Kilimo, Ujenzi na Mifugo. Hatua hizi za urutubishaji na matumizi yake katika kutengeneza vifaa hivyo zitafanyika katika nchi zilizoendelea kama vile Japan, Ufaransa, Urusi, n.k. Katika hatua hizo ndipo huzalishwa mabaki (highly enriched uranium wastes) ambayo yasipodhibitiwa kwa kiwango cha kuridhisha huweza kusababisha madhara yanayoongelewa.
Uchimbaji na usafirishaji wa madini ya urani katika hali ya yellow cake hayana madhara kwa kiwango hicho kinachoelezwa na Wanaharakati. Madhara yanayoweza kujitokeza katika shughuli hizo za uchimbaji na usafirishaji ni madhara ya kawaida kwa kila eneo ambapo shughuli za uchimbaji madini yawe ya dhahabu, urani, chokaa ama makaa ya mawe huweza kujitokeza. Ni madhara ya kiusalama kama vile ajali ama mazingira kuchafuliwa na kemikali ikiwa wawekezaji na Serikali watazembea katika usimamizi wa shughuli hizo.
Madhara pekee maalum kwa shughuli za uchimbaji urani ni wizi unaoweza kutokea wa mapipa ya urani wakati wa usafirishaji na hivyo uzagaaji wa madini hayo nje ya mkondo wa Serikali na udhibiti wa Kimataifa kupitia Shirika la IAEA. Ndio maana katika usafirishaji wa madini hayo, Taasisi ya TAEC, Jeshi la Ulinzi, Usalama wa Taifa, Idara ya Polisi na Idara ya Madini watahusika kwa pamoja kuhakikisha madhara kama hayo hayatokei na yakitokea hatua za haraka kudhibiti madhara hayo zinachukuliwa.
IMETOLEWA NA:
WIZARA YA NISHATI NA MADINI

No comments:

Post a Comment