Operesheni maalumu ya GIBOIA yakamata dawa bandia 273

Jumla ya dawa bandia za aina 273 zenye
thamani ya shilingi 49,634,733/= zimekamatwa katika operesheni maalumu
iliyoendeshwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Shirikisho la
Polisi la Kimataifa (Interpol), Baraza la Famasi, TAMISEMI, Bohari ya
Dawa (MSD), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Shirika la Viwango
(TBS), Tume ya Ushindani (FCC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi
ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Rais na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
katika maeneo 138 nchini.(P.T)
Operesheni hiyo ijulikanayo kama 'Giboia' iliendeshwa kwa lengo la kufuatilia, kukamata na kuwafikisha katika vyombo vya
sheria wanaojihusisha na biashara ya dawa bandia, zisizosajiliwa, zisizo na ubora na zilizoisha muda wa matumizi.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba alisema hayo alipozungumza na
waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana wakati akitangaza matokeo
ya operesheni hiyo. Alisema operesheni hiyo ilifanyika kwa siku tatu,
Oktoba 1-3 mwaka huu, kwa kukagua maduka ya dawa ya jumla na rejareja,
waingizaji wa dawa nchini, vituo vya afya na maabara binafsi.
Aliyataja maeneo , ambayo ukaguzi huo
ulifanyika na idadi ya vituo kwenye mabano kuwa ni Dar es Salaam (67),
Mbeya (6), Kilimanjaro (8), Arusha (5), Mwanza (11), Geita (7),
Shinyanga (6) na Dodoma (20).
"Dawa bandia zilizokamatwa zilikuwa
aina mbili (Asdoxin na Penizin-V), zilizoisha muda wa matumizi zilikuwa
76, dawa za serikali na miradi mbalimbali ya serikali 28, zisizosajiliwa
86 na zenye ubora duni 40," alisema.
Alisema dawa nyingine ni zilizofutiwa
usajili 41 na 19 zinazohisiwa kuwa ni bandia, ambazo zilikamatwa na
kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara kuhakiki ubora wake.
Manumba alisema hatua zimechukuliwa, ikiwa ni pamoja na majalada 42 ya kesi kufunguliwa katika vituo mbalimbali nchini.
Manumba alisema hatua zimechukuliwa, ikiwa ni pamoja na majalada 42 ya kesi kufunguliwa katika vituo mbalimbali nchini.

MAELEZO
YA UTANGULIZI YA MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA (TFDA)
BW. HIITI B. SILLO KATIKA MKUTANO WA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU MATOKEO
YA OPERESHENI "GIBOIA" KATIKA UKUMBI WA MIKUTANO WA TFDA TAREHE 10
OKTOBA, 2013
Naomba nichukue fursa hii kwa niaba ya
Menejimenti na Wafanyakazi wa TFDA kuwakaribisha, katika ofisi za
Mamlaka ya Chakula na Dawa. TFDA ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii yenye jukumu la kudhibiti ubora na usalama wa
vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.
Naamini wote tunaelewa dhima ya TFDA
ambayo ni kulinda afya za wananchi kwa kuzuia athari zinazoweza
kujitokeza kutokana na matumizi ya vyakula, dawa, vipodozi na vifaa
tiba. Katika kufikia dhima hii, changamoto kubwa tunayokabiliana nayo
katika udhibiti ni uwepo wa bidhaa duni, bandia na zisizosajiliwa kwenye
soko.
Ndugu wanahabari,
Tumewaalika ili tuwape taarifa juu ya
matokeo ya Operesheni Giboia iliyofanyika hapa nchini kwa pamoja baina
ya Mamlaka ya Chakula na Dawa na Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana
na Shirikisho la Polisi la Kimataifa (Interpol) na taasisi na idara
nyingine za Serikali. Taasisi na idara nyingine za Serikali ambazo
majukumu yake yanagusa masuala ya dawa au udhibiti zilizoshiriki
operesheni hii ni mpamoja Baraza la Famasi, TAMISEMI, Bohari ya Dawa
(MSD), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Shirika la Viwango (TBS),
Tume ya Ushindani (FCC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya
Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU), Ofisi ya Rais na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Napenda kuzishukuru taasisi hizi kwa
ushirikiano wao katika kufanikisha operesheni mbalimbali za kupambana na
biashara haramu ya dawa bandia na kwa namna ya pekeeOperesheni Giboia.
Mamlaka itaendelea kushirikiana na taasisi hizi katika kukabiliana na
changamoto ya udhibiti wa bidhaa bandia na duni za chakula, dawa,
vipodozi na vifaa tiba bandia na vile ambavyo havisajiliwa na Mamlaka
ili kuwalinda wananchi dhidi ya madhara ya kiafya wanayoweza kuyapata.
Ndugu wanahabari,
Operesheni hii ni mwendelezo wa
operesheni za awali za kufuatilia dawa bandia na duni katika soko. Lengo
la Operesheni hii lilikuwa ni kukamata na kuwafikisha katika vyombo vya
sheria wale wote wanaojihusisha na biashara ya dawa bandia. Dawa
zilizolengwa zilikuwa ni dawa za kutibu ugonjwa wa malaria, dawa za
kupunguza makali ya virusi vya ukimwi, viuavijasumu (antibiotics), dawa
za kuongeza nguvu za kiume na dawa za kupunguza maumivu. Dawa hizi
zilichaguliwa kutokana na kuwa na matumizi makubwa zaidi hapa nchini na
hivyo kuwa na soko kubwa kiasi cha kuvutia biashara haramu ya dawa
bandia. Vile vile, katika Operesheni hii dawa za Serikali na miradi
mbalimbali ya Serikali, dawa zisizosajiliwa, dawa duni na dawa
zilizoisha muda wa matumizi zilifuatiliwa.
Ndugu wanahabari,
Operesheni Giboia imefanyika sanjari
katika nchi saba zilizopo kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo ni Afrika
Kusini, Angola, Malawi, Msumbiji, Swaziland, Zambia na Tanzania kwa muda
wa siku tatu kuanzia tarehe 1 hadi 3 Oktoba 2013.
Makubaliano ya kufanyika kwa
Operesheni Giboia yalifikiwa katika mkutano uliohusisha nchi
nilizozitaja uolifanyika jijini Luanda, Angola tarehe 10 hadi 12 Juni
2013. Pamoja na mambo mengine, mkutano huo uliweka mikakati ya namna ya
kuendesha Operesheni Giboia kwa mafanikio.
Napenda kuwajulisha kwamba ushirikiano
baina ya nchi mbalimbali katika vita dhidi ya dawa bandia ni
utekelezaji wa Azimio la Mawaziri wa Afya Duniani la mwaka 2012 (World
Health Assembly Resolution 65.19). Azimio hilo pamoja na mambo mengine
limeelekeza ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kupambana na
biashara haramu ya dawa bandia.
Kwa upande wa Tanzania, Operesheni
Giboia imefanyika katika mikoa tisa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Geita,
Mbeya, Arusha, Kilimanjaro, Dodoma na Dar es salaam. Maeneo
yaliyokaguliwa ni pamoja na famasi, maghala ya kutunzia dawa, vituo vya
afya na maabara binafsi na maeneo yote yaliyotiliwa mashaka ya kuwepo
kwa dawa hizo bandia.
Ndugu wanahabari,
Kwa kumalizia maelezo yangu, napenda
kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya
Jinai nchini, Kamishna wa Polisi, Bw. Robert Manumba na Jeshi la Polisi
kwa ujumla kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa TFDA katika kupambana na
tatizo hili kubwa la dawa bandia katika nchi yetu. Aidha, natoa
shukrani za dhati kwa taasisi na vyombo vyote vya dola kwa ushiriki wao
katika operesheni hii na vile vile kwa kuwa tayari wakati wote
kushirikiana na TFDA katika mapambano haya. Imani yangu ni kwamba
ushirikiano uliopo ukiendelezwa na kwa ushirikiano kutoka kwa wanahabari
na wananchi kwa ujumla tutashinda vita dhidi ya biashara haramu ya dawa
bandia.
Baada ya maelezo haya, ninayo heshima
kumkaribisha Kamishna wa Polisi, Robert Manumba, Mkurugenzi wa Makosa ya
Jinai nchini ili aweze kutoa matokeo ya Operesheni Giboia.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Source: http://www.wavuti.com
No comments:
Post a Comment