SERIKALI YATANGAZA VIWANGO VIPYA VYA ALAMA ZA UFAULU ELIMU YA SEKONDARI
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Sifuni Mchome
akifafanua kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya upangaji wa
viwango vya alama, matumizi ya alama endelevu ya mwanafunzi na ufaulu
leo jijini Dar es Salaam, kulia ni Kamishna wa Elimu Profesa Eustella
Bhalasesa.
_ Baadhi
ya Maafisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakimsikiliza Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo Profesa Sifuni Mchome (hayupo pichani).
Waandishi
wa habari na maafisa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Profesa Sifuni Mchome(hayupo pichani).(P.T)
Picha zote na Eliphace Marwa (MAELEZO)
UPANGAJI WA VIWANGO VYA ALAMA, MATUMIZI YA ALAMA ENDELEVU YA MWANAFUNZI NA UFAULU
UTANGULIZI
Wizara imekusanya maoni ya Wadau wa
Elimu kuhusu Upangaji wa Viwango vya Alama (Grade Ranges) katika
Mitihani ya Kuhitimu Kidato cha Nne na cha Sita pamoja na Matumizi ya
Alama za Tathmini Endelevu ya Mwanafunzi (Continuous Assessment ama CA)
kwa ajili ya kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi. Maoni ya wadau
yamekusanywa kwa sababu kwa muda mrefu sasa upangaji wa viwango vya
alama vinavyotumika na utaratibu wake katika mitihani ya kuhitimu Kidato
cha Nne na Kidato cha Sita umekuwa haufanani pamoja na kwamba mitihani
hiyo yote ni ya elimu ya sekondari. Pia mfumo masuala mbalimbali ya
mitihani katika elimu ya sekondari umekuwa na miundo tofauti ikiwemo ule
unaotumika shuleni na ule wa Baraza la Mitihani la Taifa. Kwa sasa kuna
miundo mikuu miwili katika mfumo huo.
Muundo wa Kwanza ni upangaji wa
viwango katika ngazi ya Shule ambapo Alama Mgando (Fixed Grade Ranges)
zifuatazo hutumika kupanga madaraja: A = 81 – 100; B = 61 – 80; C = 41 –
60; D = 21 – 40 na F = 0 – 20. Muundo huu umetumika kwa muda mrefu na
umezoeleka kwa walimu na wanafunzi wa elimu ya sekondari kwa ujumla.
Muundo wa Pili ni wa viwango
vinavyotumiwa na Baraza la Mitihani la Taifa ambapo ambapo kabla ya
mwaka 2012 muundo wa viwango nyumbufu (flexible grade ranges) ulitumika.
Katika muundo huu uwigo wa alama ulibadilika badilika kulingana na hali
ya matokeo ilivyokuwa kwa mwaka husika. Lakini kuanzia mwaka 2012,
Serikali iliamua kutumia mfumo wa Upangaji wa Alama Mgando (Fixed Grade
Range) kwa Kidato cha Nne na Kidato cha Sita. Katika mtihani wa Kidato
cha Nne mwaka 2012 Baraza lilitumia mfumo huu wa alama mgando ambapo: A =
80 – 100, B = 65 – 79, C = 50 – 64, D = 35 – 49, F = 0 – 34. Kwa upande
wa Kidato cha Sita Baraza lilitumia mfumo wa A = 80 – 100; B = 75 - 79;
C = 65 – 74; D = 55 – 64; E = 45 – 54; S = 40 – 44 na F = 0 – 39.
Mifumo hii ya Baraza haikuwa inafahamika kwa wadau na hivyo kuwa sehemu
ya malalamiko katika sekta ya elimu na mafunzo.
Vilevile, Sera ya Elimu na Mafunzo ya
mwaka 1995 imeelekeza kwamba katika kuamua kiwango cha ufaulu wa
mwanafunzi wa elimu ya sekondari, Alama za CA zitachangia asilimia
hamsini (50%) na Mtihani wa mwisho utachangia asilimia hamsini (50%).
Kwa upande wa Zanzibar, CA zimekuwa zikiandaliwa kwa mfumo wa asilimia
arobaini (40%) na mtihani wa mwisho asilimia sitini (60%). Pamoja na
kwamba Baraza halijawahi kuutumia mifumo hii tangu ilipowekwa, kumekuwa
na mitazamo, maoni na mapendekezo tofauti katika muundo na matumizi ya
alama za CA. Kuna mawazo pia kwamba mfumo wa CA kuchangia matokeo ya
mwisho ya mwanafunzi pia utumike kwa watahiniwa wa kujitegemea (private
candidates). Kwa sasa matokeo ya mitihani ya watahiniwa hawa yamekuwa
yakitumia alama za mtihani wa mwisho tu na hivyo kutafsiriwa kama
utaratibu ambao unamwonea mwanafunzi ambaye anahamu ya kujiendeleza
kielimu lakini anakwama kwa sababu mfumo unaotumika siyo rafiki kwa
mtahiniwa.
Kwa mantiki hii, Wizara imedhamiria
kufanya harmonization ya masuala ya alama katika mitihani ya Kidato cha
Nne na Kidato cha Sita ili kupata muundo mmoja na ulio wazi kwa wadau
wote wa elimu ya sekondari. Lakini pia serikali imedhamiria kuhakikisha
tathmini za wanafunzi katika ngazi mbalimbali zinakwenda sambamba na
matarajio ya mitaala inayotumika na ambayo inahuishwa mara kwa mara ili
iendane na wakati na mahitaji ya elimu katika ngazi mbalimbali.
VIWANGO NA UTARATIBU KUANZIA MWAKA 2013 KWA KIDATO CHA NNE NA
MWAKA 2014 KIDATO CHA SITA
Baada ya kufanya tathmini ya maoni
mbalimbali ya wadau, misingi ifuatayo ilizingatiwa katika maamuzi kuhusu
makundi ya alama na muachano wake:
a) Alama zitakazotumika zitakuwa A, B,
C, D, E na F. Muachano wa alama kati ya kundi moja hadi jingine
utafanana, isipokuwa tu pale ambapo itaonekana kuna sababu na hakuna
athari za kuwa na muachano tofauti na ule ambao umetumika katika makundi
mengine.
b) Makundi ya alama hayatakuwa na
clusters isipokuwa pale ambapo itaonekana kufanya hivyo kunaleta tija
katika kupata picha ya wahitimu kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Kwa
mantiki hii
(i) makundi ya alama A, C, D, E na F
yabaki na cluster moja moja bali kundi la alama B litakuwa na clusters
mbili. Kundi la kwanza litakuwa la wale ambao wamepata alama kati ya 50
mpaka 59 na litaitwa B na lingine litakuwa la wale ambao wamevuka uwigo
wa 50 hadi 59 na kuelekea uwigo wa 60 hadi 74 na hili litaitwa B+
(angalia jedwali hapo chini).
(ii) Pamoja na kuwa na muachano wa
alama 26 kama jedwali linavyoonesha hapo chini, alama A kwa miaka mingi
imekuwa ikianzia alama 75 hadi 100 na kwamba pamoja na uwigo huo bado
wanaofaulu kwa kiwango hicho ni wachache sana. Kwa mantiki hii, hakuna
haja ya kubadilisha uwigo ila juhudi ziendelee katika ufundishaji na
ujifunzaji ili kiwango cha ufaulu kiongezeke na kupata wanafunzi wengi
zaidi wanaofaulu katika kundi hili.
(iii) Pia, pamoja na kuwa na muachano
wa alama 20 kama jedwali linavyoonesha hapo chini kwa miaka mingi, huko
shuleni mwanafunzi aliyepata alama 21 na hadi 30 alihesabiwa kuwa na
ufaulu wa chini kabisa au hafifu kwa kiwango cha alama D na ingawa
ilikubalika ufaulu wa aina hiyo kwa mazingira ya nchi yetu unaridhisha.
Alama F ilikuwa ni kwa wale waliopata chini ya hapo. Hivyo, alama F
itaendelea kuwepo na itaanzia alama 0 hadi 19 na E itaanzia alama 20
hadi 29 na D – 30 -39. Lengo la muundo huu ni kuwa alama mbalimbali,
isipokuwa kwa makundi machache, zianzie kwenye 0 yaani 0, 10, 20, 30, 40
na kuendelea badala ya kuanzia kwenye moja yaani 1, 11, 21, 31, 41 na
kuendelea. Hii ni kwa ajili ya kuleta mtizamo unaofanana katika ngazi
mbalimbali za elimu ambapo kwa sasa ngazi ambazo siyo za elimu msingi na
sekondari zinatumia muundo wa kuanzia kwenye 0 badala ya 1.
c) Uwigo wa jumla wa alama kwa Kidato
cha Nne na Kidato cha Sita utaendelea kuwa wa alama 0 hadi 100 na kila
kundi katika uwigo huu limepewa tafsiri kwa ajili ya kuamua mambo
mbalimbali yanayohusu maendeleo ya mwanafunzi kulingana na malengo ya
mtihani husika. Kimsingi, tafsiri zifuatazo zitakatumika
(i) Alama A itakuwa na maana ya ufaulu uliojipambanua (distincion or outstanding performance),
(ii) Alama B+ itakuwa na maana ya ufaulu bora sana (excellent performance),
(iii) Alama B itakuwa na maana ya ufaulu mzuri sana ( very good perfomance),
(iv) Alama C itakuwa na maana ya ufaulu mzuri (good performance);
(v) Alama D itakuwa na maana ya ufaulu wa wastani (low performance),
(vi) Alama E itakuwa na maana ya ufaulu hafifu (very low performance), na
(vii) Alama F itakuwa na maana ya ufaulu usioridhisha (unsatisfactory performance).
Wataalamu katika maeneo mbalimbali ya
elimu na ulimwengu wa kazi, kwa kushirikiana na Wizara, watatoa maana ya
tafsiri hizi kiutendaji katika maeneo yao kulingana pia na mahitaji
yao.
d) Alama C iwe ndiyo alama ya ufaulu
mzuri ambao hauhitaji urekebu wa lazima, wakati alama D na E ni alama za
ufaulu unaohitaji urekebu kadri mwanafunzi atakavyokuwa anaendelea na
masomo ili kuthibitisha kama mlengwa anaweza na kulingana na mahitaji ya
eneo husika (targeted remediation). Alama F iwe alama ya eneo
linalohitaji urekebu wa hali ya juu (intesive remediation) ili
mwanafunzi huyo aweze kumudu masomo kadri anavyoendelea kukua kielimu
ama atakapoingia katika ulimwengu wa kazi.
e) Makundi ya alama yatajumuisha CA
kwa kiwango cha asilimia isiyozidi 40 na mtihani wa mwisho kwa asilimia
isiyozidi 60 kwa makundi yote ya watahiniwa ikiwemo wale wa kujitegemea
(private candidates). Hii ni kwa kuzingatia kwamba CA siyo vizuri izidi
uwigo wa alama ya ufaulu mzuri unapoanzia ambayo ni C au 40.
f) CA kwa upande wa Kidato cha Nne
zitokane na mtihani wa Kidato cha Pili (alama 15), matokeo ya Kidato cha
Tatu (alama 5 kwa kila muhula, na hivyo jumla ya alama 10), mtihani wa
Mock (alama 10) na kazi mradi au Projects (alama 5). Kwa upande wa
Kidato cha Sita, CA iendelee kutokana na muundo unaotumika sasa.
g) CA zitumike pia kwa watahiniwa wa
kujitegemea. Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegmea ambao wanarudia
Mitihani, CA zao zitumike zile zilizotumika kutoa matokeo yake ya
mitihani ya awali. Kwa watahiniwa wa kujitegemea waliopitia mfumo wa
Qualifying Test (QT), matokeo ya QT yatumike kama CA na mtihani wa
mwisho uchangie alama 60.
h) Kwa vile alama endelevu kwa mwaka
2013 kwa wanafunzi wa Kidato cha Nne tayari zimeshawasilishwa Baraza la
Mitihani Tanzania, alama hizo zichangie asilimia 40 katika mtihani wa
Kidato cha Nne mwaka 2013.
i) Muundo wa wastani wa alama katika
ufaulu (Grade Points Average ama GPA) utaandaliwa na kuanza kutumika
pale utakapokuwa tayari na wadau wataelimishwa kuhusu muundo huo ili
wapate kuufahamu na manufaa yake katika elimu ya sekondari.
j) Muundo huu mpya wa alama utatumika
kwa mzunguko wa miaka minne kabla haujahuishwa tena ili kuupa muda wa
kutosha kuona aina ya changamoto zinazojitokeza na jinsi ya
kuzishughulikia. Aina hii ya muda itaruhusu vidato vinne vya elimu ya
sekondari ya kawaida na nane ya elimu ya sekondari ya juu kupimwa. Hata
hivyo, uhusihaji wa masuala ya mitihani unaweza ukafanyika iwapo matokeo
ya uhuishaji wa mitaala kwa ujumla utahitaji pia eneo la mitihani
liguswe na kuhuishwa pia.
Kwa mantiki hii, viwango vya alama na ufaulu ni kama inavyooneshwa kwenye jedwali la 1 hapa chini