Viwango vya Fifa vinatupa ukweli tunaouficha
KATIKA
siku za hivi karibuni vyombo vya habari hasa vya michezo vimepambwa na
taarifa za Tanzania kupanda viwango vya soka kwa mujibu wa takwimu za
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Habari
hizo zimepokewa katika namna nzuri ya kuonyesha kwamba Tanzania imepiga
hatua na hivyo jambo hilo kuonekana ni la kujivunia.
Si nia
yetu kubeza wanaojivunia mafanikio hayo kwani ndio ukweli wenyewe hasa
unapoviangalia viwango hivyo na kuvifananisha na vilivyopita.
Kwa mfano
takwimu za Fifa za mwezi Septemba, zilionyesha kwamba Tanzania ilikuwa
ya 115 na takwimu zilizotolewa mwezi huu zinaonyesha kwamba Tanzania
sasa ni ya 110.
Wengi
waliopata taarifa hizo walijifariji hasa baada ya kuona Tanzania imepiga
hatua hiyo na kuizidi hata nchi ya Kenya ambayo kwa mujibu wa viwango
hivyo inashika nafasi ya 116.(P.T)
Kwa
kuziangalia takwimu hizo hizo utaona kwamba Kenya imepata pigo kwa
kuporomoka kutoka nafasi ya 111 iliyokuwa mwezi uliopita hadi kufikia ya
116 iliyopo sasa.
Hata
hivyo tungependa kutoa tahadhari kwamba pamoja na hatua tuliyoipiga kwa
mujibu wa viwango hivyo lakini bado wadau wanatakiwa kuviangalia viwango
hivyo kwa mapana zaidi jambo ambalo tunaamini litawafanya watafakari
kwa kina.
Tunasema
hivyo kwa sababu ukivichambua kwa kina viwango hivyo utaona kama
Tanzania haijapiga hatua yoyote ya kutisha, badala yake imeendelea
kupanda na kushuka.
Kuna
usemi wa siku hizi uliozoeleka wa homa za msimu, si vibaya kulifananisha
soka la Tanzania na homa za msimu kama utaamua kuvichambua viwango vya
Fifa.
Unaizungumziaje
nchi ambayo rekodi zilizotolewa na Fifa mwezi Agosti zilionyesha kwamba
ilikuwa ya 110, Septemba ikawa ya 115, Oktoba ikarudi nafasi ya 110?
Je ni
vibaya kuzingatia takwimu hizo na kuliona soka letu kuwa ni mfano wa
homa za msimu. Hatulisemi hili kwa nia mbaya bali tunachotaka ni kuona
wadau wanavitumia vizuri viwango hivi kwa kujichambua na si tu kujivunia
kupanda.
Katika
kipindi chote cha mwaka huu, wakati pekee ambao Tanzania ilionyesha
matumaini kwa mujibu wa rekodi za Fifa ni mwezi Julai kwa kushika nafasi
ya 106 wakati ambao jirani zetu Kenya walishika nafasi ya 95.
Mwezi Juni ripoti zilionyesha kwamba Tanzania ilikuwa ya 113, Mei 122, Aprili 122, Machi 117, Februari 116 na Januari 118.
Kwa
mantiki hiyo tangu tuuanze mwaka 2014, Tanzania haijawahi kuwa miongoni
mwa timu 100 bora kwa mujibu wa rekodi za Fifa jambo ambalo linatosha
kutufanya tuukubali ukweli kwamba soka letu bado.
Katika
viwango vya Fifa Tanzania mara zote inashindanishwa kati ya nchi 207,
kati ya nchi hizo Tanzania inazishinda baadhi ya nchi ambazo
hazijulikani katika ulimwengu wa soka na tuna hakika wapo Watanzania
ambao hawajawahi hata kuzisikia.
Mfano nchi kama Macau, Anguilla, Bhutan, Visiwa vya Cayman, Visiwa vya Cook, Montserrat, Vanuatu, Guam, Belize na nyinginezo.
Tunachotaka
kukisisitiza hapa ni kwamba tufurahie kupanda lakini tuukubali ukweli
kwamba soka letu bado lina kazi ya kufanya ili walau tuwe chini ya timu
100 bora duniani na tudumu katika nafasi hizo si kupanda na kushuka.
Chanzo:Mwanaspoti
No comments:
Post a Comment