Polisi wachana bango la walimu linalohoji posho Bunge Maalumu
Wafanyakazi
wakiwa na bango wakiingia kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam
palipofanyia maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Wafanyakazi Duniani,
juzi. Picha na Silvan Kiwale
Maandamano
ya walimu kuingia katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kuadhimisha
Siku ya Walimu Duniani, jana yalipata mtafaruku baada ya polisi
kuyaingilia na kuchana bango mojawapo lililohoji posho za wajumbe wa
Bunge la Katiba.
Bango
hilo la kitambaa cheupe lilikuwa na maandishi yanayohoji posho ya
Sh300,000 waliyokuwa wanapata wajumbe wa Bunge la Katiba,
yakilinganishwa na kazi kubwa wanayofanya walimu.
Ujumbe
wenyewe ulisomeka hivi: "Haki iko wapi usawa uko wapi, posho ya mjumbe
wa Bunge la Katiba kwa siku shilingi laki tatu, mshahara wa mwalimu
shilingi 370 kwa mwezi. No big results without big salary (Hakuna
matokeo makubwa bila mshahara mkubwa)".
Ujumbe
huo ulikuwa ukifanya rejea ya viwango vya malipo ya Sh300,000 kwa siku
ambazo walikuwa wakilipwa wajumbe wa Bunge Maalumu zikiwa ni Sh230,000
kama posho ya kujikimu na Sh70,000 ambazo ni posho ya vikao.(P.T)
Hata
hivyo bango hilo lilichanwa hatua chache kabla ya walimu hao hawajaingia
uwanjani humo, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Mwenyekiti
wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), mkoani Kagera Dauda Bilikesi,
alisema amesikia habari za bango hilo kuharibiwa lakini akasema
asingezungumza kwa kina kuhusu suala hilo kwa kuwa hayo yamepita.
Waibuka na shairi
Muda
mfupi baada ya polisi kuharibu bango hilo lisionekane uwanjani, walimu
hao walipiga chenga kiana wakaibuka na ujumbe ule ule kwa njia ya
shairi.
Kupitia
shairi hilo liliposomwa mbele ya Pinda, walimu walihoji ukubwa wa posho
za wajumbe wa Bunge la Katiba zikilinganishwa na mshahara wanaopata,
hali iliyosababisha umati wa walimu uliokuwa uwanjani hapo kulipuka kwa
sauti kubwa za shangwe.
Shairi
hilo lililosomwa na Mwalimu Betwel Magoso kutoka Wilaya ya Biharamulo,
lilisababisha kuvurugika kwa muda kwa utaratibu uliopangwa kwa mujibu wa
ratiba, pale alipohoji wajumbe wa Bunge la Katiba kupata Sh1 milioni
kwa siku tatu ambazo ni mkopo wa mwalimu kwa miaka mitatu.
Mwalimu
Magoso alimgusa Pinda ambaye kabla ya kuanza hotuba yake alianza kwa
kusema kuwa mwalimu huyo alitumia ujanja kufikisha ujumbe wake na kuwa
baadhi ya maneno katika shairi lake yalikuwa ni mazito.
Kanuni za mafao zasitishwa
Katika
hatua nyingine, Serikali imesitisha matumizi ya kanuni mpya za
ukokotoaji mafao ya pensheni ambao umeibua malalamiko kuwa malipo ya
mkupuo yalipunguzwa kutoka asilimia hamsini hadi ishirini na tano.
Kanuni
hizo ni zile zilizotungwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii (SSRA) na kutangazwa Agosti 6, mwaka huu mjini Dodoma na Waziri
wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka.
Tangu
kutangazwa kwake kanuni hizo zilizua malalamiko kutoka kwa wadau
mbalimbali hususan wafanyakazi ambao walisema kuwa hayalengi kuboresha
wala kuhuisha mafao, bali yanapunguza stahili hiyo tofauti na ilivyokuwa
mwanzo.
Akihutubia sherehe hizo, Pinda alisema suala hilo linarejeshwa tena serikalini kuangaliwa upya.
"Acha
suala hili tulirejeshe serikalini tukalitazame upya kwa sababu
halikubaliki na hatuwezi kulishurutisha kwa sababu nyie ndiyo wadau,
siyo sisi. Tutawaambia walitazame tena na warudi wawashirikishe vizuri
wawaeleze mlikubali au mlikatae," alisema Pinda.
Waziri
Mkuu alisema pamoja na kuwa lengo lilikuwa ni kuboresha maisha ya
wafanyakazi kwa kuleta mfumo mpya wa ukokotoaji wa mafao ya pensheni,
suala hilo lilihitaji ushirikishwaji mpana zaidi ikiwa ni pamoja na
wadau wenyewe.
Katika
kuunga mkono kilio cha walimu, Pinda alitoa mfano wa wabunge wanaopata
mafao yao yote wanapomaliza kipindi cha uwakilishi kwa miaka mitano na
kuwa kabla ya hapo mafao hayo yalitolewa baada ya kumaliza miaka kumi,
jambo ambalo halikupendelewa na wabunge.
Kauli
hiyo ilitokana na risala ya walimu iliyosomwa na Katibu Mkuu wa CWT,
Yahya Msulwa aliyesema mabadiliko hayo yamezua manung'uniko makubwa hasa
kwa walimu wanaobeba idadi kubwa ya watumishi.
Alisema
mfumo wa ukokotoaji wa mafao wa zamani, pamoja na kuwa mishahara yao ni
midogo, ulifanya mafao yao ya uzeeni yawe na unafuu kwa kiwango fulani,
ikilinganishwa na mfumo mpya ambao ukokotoaji unafanyika kwa kuangalia
wastani wa mishahara ya miaka mitatu ya mwisho.
Kabla ya
mapendekezo hayo, ukokotoaji wa mafao ulifanyika kwa kuangalia mshahara
wa mwisho wa mtumishi na malipo yalitolewa kwa asilimia hamsini ya mafao
yote baada ya ukokotoaji kufanyika.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment