KURA YA MAONI, NI TURUFU YETU WANANCHI, TUSIICHEZEE
Mwandishi Eric Shigongo
NIWASALIMU wote
kwa jina la Mwenyezi Mungu, kwani bila yeye hakuna lisilowezekana.
Nimekuwa nikiwahimiza siku zote ndugu zangu, bila kujali imani
mbalimbali za dini tunazoziabudu, tutenge muda kwa ajili ya kumshukuru
Mungu, kwa sababu yeye ndiye kila kitu.
Sisiti
kurudia, tena na tena kusisitiza kuwa tuko hivi tulivyo leo kwa sababu
ya mapenzi yake, kwa sababu kama angetaka, wewe usingepata muda wa
kusoma maandishi haya, ama ungekuwa umeshakufa, au uko katika hali mbaya
ukiteseka. Lakini yeye kwa mapenzi yake, amekufanya uwe na amani na
mzima wa afya.
Lakini
siyo kwetu tu tuliopewa afya leo, hata wale walio katika mateso,
mitikisiko na manyanyaso, bado wanapaswa kumuomba Mwenyezi Mungu kwa
sababu anao uwezo wa kuondoa maumivu waliyonayo, kama tu wataamini
katika yeye.
Baada ya
kusema hayo, naomba sasa nije kwenye mada yangu ya leo. Wiki iliyopita
niliandika kuhusu umuhimu wa busara kutumika wakati wa kumalizia
mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, uliokuwa ukiendelea mjini Dodoma
ambao ulikuwa katika hatua zake za mwisho.GPL(P.T)
Ninashukuru
Mungu kwamba kazi ile kubwa na muhimu kwa taifa letu ilifanyika na
kukamilika, licha ya changamoto za hapa na pale maana kesho, Rais Jakaya
Mrisho Kikwete atakabidhiwa rasmi rasimu ya katiba hiyo kwa hatua zaidi
zinazopaswa kuendelea.
Kwa kuwa
jambo hili limekuwa ni muhimu sana kwa taifa letu, sina budi kuendelea
tena kulizungumzia, kwa sababu kitu hiki kama hatutakwenda nacho sawa,
ipo hatari ya kuigawa au hata kuisambaratisha nchi yetu ambayo kwa
kipindi chote tokea uhuru tumekuwa na amani, upendo na mshikamano
unaowanyima raha maadui zetu.
Hatua
itakayofuata baada ya Rais Kikwete kukabidhiwa katiba hiyo ni kwa
wananchi kupiga kura ya maoni ya kuikubali au kuikataa. Ingawa kwa macho
ya kawaida inaonekana kama ni kitu chepesi na kitakachokwenda vizuri,
ni vyema tukakumbushana kwamba kama hatutakuwa makini, tunaweza kujikuta
tukianza utengano wakati au baada ya zoezi hilo.
Kura ya
maoni ni kura kama zilivyo kura zingine na hatimaye mshindi anapatikana.
Tofauti ya ushindi wa kura ya maoni na chaguzi zingine ni kwamba
mshindi wa kura ya maoni siyo chama cha siasa, bali ni Watanzania wa
makundi yote, wenye vyama na wasio na vyama.
Tusikae
tukafikiri kwamba wanaopaswa kupiga kura hii ni wana CCM, Chadema, CUF
au NCCR-Mageuzi. Hapana, Mtanzania yeyote aliyefikisha umri wa kuanzia
miaka 18 ana haki na kimsingi anatakiwa kuipigia kura katiba hii.
Lakini
wakati tukijiandaa kupiga kura ya kuikubali au kuikataa, ni vizuri pia
tukajipa muda wa kujua kitu tunachokwenda kukichagua. Pamoja na kwamba
kila makundi, yawe ya kidini, kiharakati, wanasiasa, kijamii na
kadhalika yana viongozi wao, lakini ni jambo jema sana kwa kila mtu
mmoja mmoja kujiridhisha na anachokiamini badala ya kufuata mkumbo.
Katiba
hii inashikilia uhai wako, iangalie kama itakutendea haki au la. Ukiona
haki zako nyingi za msingi zimewekwa pembeni, ikatae hata kama kiongozi
wako atasisitiza kuwa ni nzuri na inakufaa. Ukiona mambo mengi
unayoyaamini yapo, huna sababu ya kuikataa.
Binafsi
ninawaheshimu viongozi wa makundi yote, kuanzia ya kidini, wanaharakati
wa haki za binadamu, wanasiasa na kijamii, lakini ni lazima niwe mkweli
kuwa mwisho wa siku, ningependa kila Mtanzania apige kura ya maoni kwa
kuzingatia utashi wake binafsi yeye kama mwananchi na siyo kwa utashi wa
viongozi wa makundi tajwa.
Viongozi
wamefanya kazi kubwa sana wakati wa mchakato na hata sasa tunapoelekea
kwenye kura ya maoni. Hapa tulipofikia ni wakati muafaka sasa wa
wananchi kuachiwa wafanye uamuzi wa mwisho.
Ninafahamu wapo baadhi ya viongozi wetu, pengine kwa nia njema au hila, wamekuwa wakitaka wananchi wawasikilize na kuwafuata kwa kila wanachokisema kuhusu katiba.
Ninafahamu wapo baadhi ya viongozi wetu, pengine kwa nia njema au hila, wamekuwa wakitaka wananchi wawasikilize na kuwafuata kwa kila wanachokisema kuhusu katiba.
Ni kweli
kwamba wao wana ufahamu mpana kidogo kuhusu katiba pengine kuliko
wananchi, lakini siyo jambo zuri kuwalazimisha kufuata matakwa yao,
wakati kilichomo ndani ya katiba hiyo ni vitu vyao wanavyopaswa kuvijua
na kuvielewa vizuri kabla ya kukubali au kukataa.
Lengo
langu hapa ni kutaka wananchi wajue kuwa kukubali au kukataa kupitisha
katiba inayopendekezwa maana yake ni kuwa kama itakuwa ni mbaya halafu
wao wakaikubali, watateseka nayo kwa miaka mingi ijayo na hawatakuwa na
jinsi tena ya kubadili kwa sababu wakati huo hautakuwepo.
Lakini
bahati mbaya zaidi ni kuwa wanaweza kuikataa katiba ambayo ina mambo
mazuri sana kwa ajili ya ustawi wetu kama taifa na hata kwa mtu mmoja
mmoja, kwa sababu tu tutakubali kuwasikiliza viongozi wetu wa dini,
siasa au makundi mengine ya kijamii.
Nimalizie
kwa kuwasisitizia tena wananchi wenzangu, kabla ya kwenda katika
sanduku la kura, tuwe tumejua nini tunataka, tujiondoe kuwa katika kundi
la wafuata mkumbo. Msikilize kiongozi wako lakini uamuzi wa mwisho uwe
wako!
No comments:
Post a Comment