SERIKALI BADO HAIJATOA SH.143 BIL KIGAMBONI
Serikali
 imeingia kwenye lawama ikidaiwa kukwamisha kasi ya ujenzi wa Daraja la 
Kigamboni kutokana na kushindwa kutoa Sh.143.5 bilioni sawa na asilimia 
40 ya fedha za mradi huo hadi kukamilika.
Lawama hizo zimekuja ikiwa miezi 15 imebaki kabla ya muda uliopangwa ujenzi huo kukamilika Juni mwakani.
Kwa 
upande wake, Serikali imesema haina taarifa ya kusuasua kwa kasi ya 
ujenzi na kwamba suala la utoaji wa asilimia 40 litatekelezwa kulingana 
na taratibu.
Mmoja wa 
wafanyakazi waandamizi wa mradi huo, ambaye hakutaka jina lake kuandikwa
 kwenye gazeti, alisema kuwa kasi ya ujenzi imepungua kutokana na fedha 
kidogo zinazotolewa kwa ajili ya uendelezaji.
"Kuna kazi hazijafanyika hivi sasa na zingine zimesimama kabisa," alisema.
        
                        
        
        
        
Kwa 
upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Gerson Lwenge alisema hawajapokea 
malalamiko yoyote kutoka kwa makandarasi kuhusu suala la fedha kuchelewa
 kutoka serikalini.
"Suala la
 fedha kuchelewa ni 'logistic' za Serikali na siyo hoja ya msingi sana 
kama daraja linaendelea kujengwa na hakuna kazi zilizosimama," alisema.
Lwenge 
alisema kuwa fedha ambazo ni sehemu ya mchango wa Serikali zitapatikana 
na kuna kila dalili ujenzi ukakamilika kabla ya muda uliopangwa.
Mkuu wa 
Idara ya Uhusiano Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eunice 
Chiume alikiri kuwa fedha kutoka serikalini hazijatolewa mpaka sasa.
Alisema 
fedha za Serikali zinapaswa kutumika kujenga barabara zinazounganisha 
daraja hilo na maeneo ya Kigamboni kwa upande mmoja na Barabara ya Shimo
 la Udongo.
"Fedha za
 Serikali ni kwa ajili ya ujenzi wa barabara zenye urefu kilomita 1.5 
kila upande kwa kiwango cha lami, lakini hadi sasa hatufahamu ujenzi wa 
barabara hizo utaanza lini," alisema.
Aliongeza:
 "Halitakuwa jambo zuri daraja kukamilika bila barabara hizo kujengwa, 
kwani hali hiyo inaweza kuchangia msongamano usio wa lazima. Kwanza siyo
 vizuri kwa daraja lenyewe kuwa na lami, kisha likaunganishwa na 
barabara za vumbi."
Mradi huo
 ulizinduliwa Septemba 2012 na unatekelezwa chini ya makandarasi wawili,
 Kampuni ya China ya Railway Jiangchang (T) Ltd na China Major Bridge.(P.T)
No comments:
Post a Comment