Mwandishi Uingereza aja kuona vita dhidi ya ujangili
Mwandishi huyo jana alitembelea ghala
la meno ya tembo yaliyohifadhiwa katika Wizara ya Maliasili na Utalii
kumwonyesha juhudi ambazo zimekuwa zikifanyika kupambana na ujangili
nchini.
Dar es Salaam. Serikali imeanza juhudi
za kujinasua kwenye lawama kwamba haifanyi juhudi za kutosha kupambana
na ujangili kwa kuwaalika waandishi wa habari wa kimataifa ili kujionea
kazi inayofanyika.
Tayari mwandishi wa Habari wa
Uingereza aliyeandika habari katika Gazeti la Daily Mail, Martin
Fletcher kuwa Tanzania haifanyi jitihada zozote kukabiliana na ujangili
amewasili nchini.
Mwandishi huyo aliandika habari kwenye
gazeti hilo toleo la Februari 8 na 9, mwaka huu kwamba Serikali ya
Tanzania imeshindwa kutimiza wajibu wake katika kuwalinda faru na tembo
ambao wako hatarini kutoweka.
Mwandishi huyo jana alitembelea ghala la meno ya tembo yaliyohifadhiwa katika Wizara ya Maliasili na Utalii kumwonyesha juhudi ambazo zimekuwa zikifanyika kupambana na ujangili nchini. Akizungumza muda mfupi baada ya kuona ghala hilo, Fletcher alisema ni jambo jema kwa kuwa ameona sehemu ya hazina hiyo.
"Nimeona kwa sehemu kubwa hifadhi iliyopo, bado ninaendelea kufuata utaratibu kwa kuwa nimealikwa, siwezi kusema lolote kwa sasa," alisema Fletcher. Kwa mujibu wa ratiba, leo atapelekwa katika Mbuga ya Selous ambako atajionea 'utajiri wa wanyama kwenye mbuga hiyo'.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alikutana na mwandishi huyo lakini akakanusha kuwa Serikali imemwalika, akisema hiyo ilikuwa ni sehemu ya mpango wake akitaka kujionea mambo yanayotendeka nchini kuhusu suala la ujangili.
Alisema mbali na mwandishi huyo, wengine wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na CNN ya Marekani nao wameomba kufanya hivyo.
Habari zilizoandikwa na mwandishi huyo ziliwapa wakati mgumu Rais Jakaya Kikwete na Waziri Nyalandu kwa kuwa zilichapishwa wakati Rais akihudhuria mkutano kuhusu ulinzi wa wanyama walio hatarini kutoweka.
Chanzo, mwananchi (R.M)
No comments:
Post a Comment