HOTUBA YA JK,WAKATI WA KULIHUTUBIA BUNGE MAALUM LA KATIBA
Mheshimiwa Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Pongezi
Nakushukuru
sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa ya kuja kuzungumza na
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge letu Maalum la Katiba katika siku hii
muhimu na ya kihistoria kwa nchi yetu. Nimekuja kuwatakia heri na
naungana na Watanzania wenzetu wote kuwaombea baraka za Mwenyezi Mungu,
ili muweze kuifanya kazi yenu kwa utulivu, hekima, umakini mkubwa na
kuimaliza kwa salama na kwa mafanikio yanayoyatarajiwa na Watanzania.
Natoa
pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza
Bunge hili maalumu na la kihistoria. Ushindi mkubwa mliopata ni
kielelezo tosha cha imani kubwa na matumaini waliyonayo Wajumbe wenzenu
kwenu. Matumaini yao ndiyo matumaini ya Watanzania wote, kwamba
mtaliongoza vizuri Bunge hili, ili liweze kutimiza kwa ufanisi mkubwa
jukumu lake muhimu sana katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Niruhusu
pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa
bahati ya aina yake waliyopata ya kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania. Fursa hii hutokea mara chache sana katika historia
ya nchi yo yote na watu wake. Mkifanikiwa kuipatia nchi yetu Katiba
nzuri majina yenu yataandikwa kwa wino wa dhahabu, katika kumbukumbu za
historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni
matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga Katiba itakayokubalika na wengi.
Katiba inayotekelezeka. Katiba itakayoimarisha Muungano wetu kwa kuondoa
changamoto zilizopo sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu mfumo bora wa
kuongoza na kuendesha mambo yetu. Katiba itakayoimarisha umoja, upendo,
ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania, licha ya
tofauti zao za asili za upande wa Muungano na maeneo watokako, au
tofauti za jinsia, rangi, kabila, dini na ufuasi wa vyama vya siasa.
Katiba itakayodumisha amani, usalama na utulivu nchini. Katiba
itakayostawisha zaidi demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria,
utawala bora na kudhibiti maovu.
Na,
mwisho ingawaje siyo mwisho kwa umuhimu, Katiba itakayoweka mazingira
mazuri kwa uchumi wa nchi kukua, na wananchi wengi kunufaika sawia na
maendeleo yatayopatikana.
Historia ya Katiba Nchini
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Hii
itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Aprili 26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato wa kutunga Katiba mpya.
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya Muda na mara ya
pili ni mwaka 1977 ilipotungwa Katiba ya Kudumu tuliyonao sasa. Tofauti
na mara mbili zilizopita, safari hii mchakato unahusisha watu wengi
zaidi. Wananchi wameshiriki moja kwa moja kutoa maoni yao kwa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, na ndio watakaofanya uamuzi wa mwisho kuhusu
Katiba mpya kwa kura ya maoni. Wananchi pia walipata nafasi ya kuchagua
Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyojadili Rasimu ya Kwanza ya
Katiba. Pia walipata nafasi ya kutoa maoni yao kupitia Mabaraza ya
Katiba ya taasisi. Katika Bunge hili wapo wananchi 201 kutoka makundi
mbalimbali.
Katika
mchakato wa kutunga Katiba za mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo Tume za
Kuandaa Rasimu na Bunge Maalum la Katiba kama ilivyo katika mchakato
huu. Hata hivyo, kwa Katiba zilizopita Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano pekee ndio waliounda Bunge Maalum. Safari hii Bunge Maalum
linajumuisha Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi 201
wanaotoka kwenye jamii, wakiwakilisha asasi na makundi mbalimbali ya
Watanzania kutoka Zanzibar na Tanzania Bara. Mchakato wa sasa utaishia
kwenye kura ya maoni itakayoshirikisha wananchi wote wa Tanzania
wanaoruhusiwa kupiga kura. Michakato iliyopita iliishia Bunge Maalum
pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tangu
kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili, 1977, mpaka sasa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko takriban mara 14.
Mabadiliko hayo yalitokana na kufanyika au kutokea kwa mabadiliko muhimu
ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika nyakati mbalimbali hapa nchini
na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa ruksa yako naomba nitaje baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:-
Mabadiliko
ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa
Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya
Afrika Mashariki mwaka 1977.
Mabadiliko
ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya Zanzibar,
hivyo kulazimu Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya Jamhuri ya
Muungano
Mabadiliko
ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa vipindi vya Urais ambao
haukuwepo kabla ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za Binadamu (Bill of
Rights) yaliingizwa kwa mara ya kwanza katika Katiba. Vilevile, Mahakama
ya Rufani ya Tanzania na mambo mengine ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika
Mashariki yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
Mwaka
1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi vya
Siasa badala ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia utaratibu
wa uchaguzi wa Rais na Wabunge ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa
vyama vingi vya siasa. Vilevile utaratibu wa kuwa na viti maalum vya
wanawake katika Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia 15 ya
Wabunge wote. Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu
Bunge lilipewa mamlaka ya kumwajibisha Rais na Waziri Mkuu kupitia kura
ya kutokuwa na imani.
Mabadiliko ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais kupitia Mgombea Mwenza.
Mwaka
2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika mabadiliko yaliyopanua
wigo wa Haki za Binadamu na kuongeza uwakilishi wa wanawake.
Umuhimu wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kufanyika
kwa mabadiliko hayo kunathibitisha utayari wa Serikali kufanya
mabadiliko kila ilipoonekana inafaa kufanya hivyo. Pamoja na kufanya
yote hayo na Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo na madai
yaliyokuwa yanajirudia ya kutaka Katiba ya Tanzania iandikwe upya. Wako
watu walioimithilisha Katiba yetu na nguo yenye viraka vingi mno kiasi
kwamba ingefaa kununua mpya badala ya kuendelea kuivaa.
Madai ya
kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama
vingi vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai Katiba mpya kwa imani, eti
kwamba, itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo tu, hata katika
mchakato wa Serikali zetu mbili kushughulikia kero za Muungano,
imedhihirika kuwa baadhi ya changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya
Katiba ili kuzipatia ufumbuzi wa uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
kutambua ukweli huo na baada ya kushauriana na kukubaliana na viongozi
wenzangu wakuu wa Chama tawala na Serikali zetu mbili wakati ule, ndipo
tarehe 31 Desemba, 2010, nikatangaza dhamira ya kuanzisha mchakato wa
kutunga Katiba mpya. Nilieleza siku ile kuwa katika mchakato huo
tutakuwa na ushirikishwaji mpana wa wananchi wa Tanzania kwa makundi yao
ya jinsia, dini, siasa na shughuli wazifanyazo kujipatia riziki na kwa
maeneo wanayotoka katika pande zetu mbili za Muungano.
Mchakato wa Katiba Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tarehe 16
Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa kwa Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba ya kuliongoza taifa katika mchakato wa kutunga
Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 18 Novemba, 2011
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Muswada wa Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, mchakato wa kutunga
Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza maoni ya wananchi mmoja mmoja na
kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao na kupitia Mabaraza ya Katiba.
Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya Katiba mpya
itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kujadiliwa na Katiba mpya
kutungwa. Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa wananchi kupiga kura ya
maoni ya kuamua kama wanaikubali au kuikataa Katiba mpya.
Tarehe 6
Aprili, 2012 nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
na kuwaapisha tarehe 13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi tarehe 2 Mei,
2012 na kuikamilisha kwa mafanikio, hatua zote zilizoihusu na kukabidhi
kwangu na kwa Rais wa Zanzibar, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba
tarehe 30 Desemba, 2013. Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa
Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo mbele ya Bunge hili tukufu tarehe
18 Machi, 2014, kinahitimisha rasmi kazi ya Tume ya Mabadiliko ya
Katiba. Kazi inayofuatia ni ya Bunge hili kujadili, kuamua na kutunga
Katiba mpya. Baada ya hapo Katiba mpya itafikishwa kwa wananchi kwa
uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga kura ya NDIYO au HAPANA.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Rasimu ya
Katiba ilichapishwa kwenye gazeti la Serikali na magazeti mengine
yanayosomwa na wananchi kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha 20(2) cha
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa ya Tume na
Rasimu ya Katiba viliwekwa wazi kwenye tovuti ya Tume kwa kila mtu
kusoma. Inafurahisha kuona kuwa watu wengi wameisoma Taarifa ya Tume na
Rasimu ya Katiba na kumekuwa na mjadala mpana kuhusu nyaraka zote hizo
muhimu. Watu wengi wametoa maoni yao na wanaendelea kufanya hivyo. Kwa
maoni yangu hili ni jambo jema sana na ni kielelezo thabiti kuwa
demokrasia imestawi na inazidi kuota mizizi Tanzania. Pia, kwamba,
Watanzania wako huru kushiriki na kutoa maoni yao kwa mambo
yanayowahusu.
Pongezi kwa Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa mara
nyingine tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa Wajumbe wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba
akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani, kwa kazi kubwa na
nzuri waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi hasa ukizingatia ukubwa wa
nchi yetu, wingi wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la kumpoteza
Mjumbe mwenzao muhimu Dkt. Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya haki
katikati ya mchakato.
Pamoja na
hayo, kwa bidii kubwa Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote
nchini na kuwafikia watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa mdomo na kwa
maandishi. Halikadhalika, walipokea na kuchambua maoni 772,211 kutoka
kwa wananchi na taasisi mbalimbali. Baada ya kupokea maoni ya wananchi,
kufanya utafiti na kwa kutumia maarifa na uzoefu wao, Wajumbe wakafanya
kazi ngumu, kuliko yote, ya kutengeneza Rasimu ya Katiba iliyoko mbele
ya Bunge hili. Ni kweli kwamba Wajumbe hawakuweza kuwafikia wananchi
wote wa Tanzania, lakini wameweza kuwafikia wananchi wengi, ambao kwa
kiasi kikubwa wanawakilisha taswira na mitazamo mipana ya jamii yetu.
Baadhi ya Masuala Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume
imefanya kazi nzuri, yenye thamani kubwa na ya manufaa kwa taifa la
Tanzania. Rasimu imeandikwa vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume
imetoa mapendekezo ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha
Katiba ya nchi yetu, kwa namna ya pekee. Katiba inayopendekezwa,
imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati
tulionao na kuweka msingi mzuri kwa huko mbele tuendako. Kwa taratibu za
kawaida za marekebisho ya Katiba tuliyonayo, isingekuwa rahisi kuingiza
mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Rasimu ya
Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi. Kina kurasa 106,
sura 17 na ibara 271. Wajumbe wa Bunge hili mnatakiwa kusoma na kuelewa
vizuri kila kilichoandikwa ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi.
Mnawajibika kuchambua kwa kina na umakini mkubwa kila kilichomo, sura
kwa sura, ibara kwa ibara, sentensi kwa sentensi na hata neno kwa neno.
Hamna budi kujiridhisha kuhusu uandishi wa vifungu vya Rasimu ya Katiba
na kufaa kwa dhana mbalimbali zilizoingizwa na kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kile
ambacho Wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au kufutwa
msisite kufanya hivyo ili Watanzania wapate Katiba iliyo bora.
Msipofanya hivyo kuna hatari ya kupata Katiba ambayo ni ngumu
kuitekeleza. Aidha, tunaweza kuwa na Katiba ambayo itanung'unikiwa na
watu wengi na kusababisha madai ya kutaka ifanyiwe marekebisho muda
mfupi baada ya kupitishwa. Bunge hili linao wajibu maalum wa kuzuia
balaa hilo lisitokee katika nchi yetu. Ngazi mbalimbali zilizowekwa
katika mchakato huu ni kama chujio la kuepusha hali hiyo isitokee. Kile
ambacho hakikuonekana katika hatua moja kitaonekana katika hatua
inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo muitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza
kuwa moja ya jambo mnalotegemewa kufanya ninyi wenzetu mliopewa dhamana
ya kutunga Katiba ya nchi yetu ni kujiridhisha na uandishi wake. Yapo
maoni yaliyotolewa kuhusu uandishi ambayo naomba myatafakari na kuamua
ipasavyo. Kwa mfano, kuna baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa
vimekuwa na mambo mengi mno kuliko inavyostahili Katiba kuwa (too
prescriptive). Pia kuna mawazo kwamba baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa
katika Katiba bali yawe kwenye Sheria zinazotafsiri utekelezaji wa
Katiba yenyewe.
Yako
mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu
hatakwenda mahakamani kuidai Serikali impatie (non justiciable). Mambo
yaliyotajwa kwenye Katiba ni mazuri na yanavutia, lakini lazima yaendane
na uwezo wa nchi na uchumi wake kuhimili. Simaanishi kwamba tuyatoe
kwenye Katiba, bali yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi
utakaporuhusu yatekelezwe. Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali
kujikuta inalaumiwa au hata kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai
ya jambo moja au jingine ambayo haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo
kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na Katiba ambayo ni ngumu
kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Yapo pia
maoni kuwa baadhi ya vifungu vina upungufu katika uandishi wake, hivyo
kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza kuwepo
athari na nyingine zinaweza kuwa mbaya. Kwa mfano, Ibara ya 2 ya Rasimu
inayotambulisha eneo na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo inasomeka kuwa
"Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanganyika
likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar likijumuisha
sehemu yake ya bahari".
Maelezo
hayo yameacha kutambua, kwa upande wa Tanzania Bara, sehemu yetu ya
maziwa na mito ambayo ni kubwa sana. Kwa nini tuache kuitaja? Je hatutoi
nafasi kwa nchi tunazopakana nazo siku moja wakaja kupora sehemu zetu
hizo na sisi kukosa utetezi kwa kuwa hata Katiba yetu haikuyatambua
maeneo hayo kuwa ni yetu? Hili ni jambo kubwa ambalo Bunge hili lazima
mlirekebishe. Wakati ndiyo huu hakuna mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo
jingine kuhusu uandishi ni mgongano kati ya pendekezo la msingi la Tume
la kuwa na muundo wa Serikali tatu na majukumu ya Serikali ya Muungano
ambayo kimsingi ni majukumu ya Serikali za nchi washirika. Katika Rasimu
hii malengo ya taifa yameainishwa na Serikali ya Muungano inatakiwa
kuhakikisha kuwa malengo hayo yanatekelezwa na itoe taarifa Bungeni.
Katika mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa na Tume masuala yahusuyo
uchumi na maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo, ufugaji, uvuvi,
viwanda, biashara, pembejeo, elimu, hifadhi ya jamii na kadhalika yako
chini ya mamlaka ya Serikali za nchi washirika. Mamlaka ya Serikali ya
Muungano ni kwa mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na Mamlaka ya Jamhuri
ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na
Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa,
Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya
Muungano.
Kwa
Rasimu kupendekeza muundo wa Serikali tatu na kuipa Serikali ya Muungano
majukumu ambayo haina mamlaka nayo, ni kuzusha utata na migongano kati
ya Serikali ya Muungano na nchi washirika. Mkichagua mfumo wa Serikali
tatu, inawalazimu muyaondoe mambo hayo kwani Serikali ya Muungano
haistahili kuyatekeleza na wala haina uwezo wa kuweka masharti kwa
Serikali za nchi washirika kwa mambo yaliyo kwenye mamlaka ya nchi hizo.
Lakini kama mtaamua tuendelee na muundo wa Serikali mbili, mambo haya
mazuri yanatekelezeka na Serikali ya Muungano bila ya matatizo. Katika
uandishi wa Rasimu Utumishi katika Serikali ya Muungano haumo katika
Orodha ya Mambo ya Muungano. Ni lazima liwemo. Hayo ni baadhi tu ya
masuala yahusuyo uandishi katika Rasimu. Naamini mkiisoma Rasimu kwa
makini mnaweza kuyagundua mengineyo.
Dhana Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
Rasimu kuna dhana mpya na mambo mapya kadhaa yaliyoingizwa ambayo
yanabadili utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa nchi na mambo mbalimbali.
Nawaomba mfanye uchambuzi wa kina kwa kila kinachopendekezwa na
kujiridhisha kuhusu kufaa kwake na manufaa yake. Fanyeni hivyo ili
tujihakikishie kuwepo kwa mambo mazuri na uendeshaji mzuri wa shughuli
katika taifa letu changa.
Mambo ni
mengi na kwa ufinyu wa muda sitaweza kuyazungumzia yote. Niruhusuni
nizungumzie baadhi ya dhana na mambo mapya yaliyomo katika Rasimu. Jambo
la kwanza, kwa mfano, linahusu Ibara ya 128 (2)(d) inayoleta dhana ya
"Mbunge kupoteza Ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi za Mbunge kwa
miezi sita mfululizo kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza".
Watu
hawana tatizo na Mbunge kuwa kizuizini ndani ya gereza kama amepatikana
na hatia Mahakamani na kuhukumiwa kifungo. Lakini, isijekuwa yuko
rumande kwa tuhuma akisubiri kesi kusikilizwa. Je akija kuonekana hana
hatia na kuachiliwa? Naungana na wale wanaoshauri kuwa jambo hili
lifafanuliwe vizuri na kutambua Mbunge kutiwa hatiani na kupata adhabu
ya kifungo cha kipindi hicho. Ni bora ifanyike hivyo sasa ili kuondoa
mikanganyiko. Hakuna haja ya kusubiri mpaka jambo hili lije kufafanuliwa
baadaye kwa Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
upande wa mtu kupoteza Ubunge kwa sababu ya "kuugua kwa miezi sita
mfululizo" ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili ambao haustahili
kufanywa na Katiba. Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine Mbunge
anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake. Anaweza kuugua
kwa miezi sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi chake cha Ubunge
kufika mwisho. Kwa nini awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba ya mwaka
1977 tunayotumia sasa haina sharti hilo. Watu wanauliza hoja na haja ya
kuwa na sharti hili kwenye Katiba mpya ni ipi? Wanasema kwa kweli
anachostahili Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake iimarike ili
aendelee kutumikia watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake. Tusiwatie
watu kishawishi cha kukatiza matibabu ili kukwepa sharti hilo. Ni vyema
jambo hili mkalitazama kwa makini, na muone kama linastahili kuwepo au
hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
Rasimu hii imeingizwa dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa
Wabunge. Tena mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu mfululizo au la!.
Jambo hilo limezua mjadala motomoto katika jamii. Ni vizuri
mkajiridhisha juu ya sababu za msingi na manufaa ya kufanya hivyo hapa
Tanzania. Mazoea yetu na ya kwingineko duniani ni kuweka ukomo kwa Wakuu
wa Nchi kwa sababu nzuri na rahisi kuzielezea. Lakini, kuwawekea ukomo
Wabunge ni jambo jipya na huenda Tanzania tukawa wa kwanza. Nashawishika
kuungana na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema mno kuanzisha
utaratibu huo hapa kwetu.
Nachelea
kuwa tutainyima nchi yetu fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu
mzuri wa uongozi kwa nafasi ya Ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa
bila ya sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo
lingine jipya linalopendekezwa na Tume ni utaratibu wa kumuondoa Mbunge
katikati ya kipindi chake cha uongozi. Kwa hoja linaonekana kuwa jambo
jema lakini naomba athari zake mzitafakari vizuri. Kuna hatari ya
kuanzisha misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha Wabunge wasifanye kazi
zao kwa utulivu bali wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao
kuwatengenezea fitna za kuwatoa. Utaratibu unaopendekezwa wa Chama chake
kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi katika mazingira hayo nao
unaweza kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha vuguvugu la kumuondoa Mbunge.
Walioshindwa kwenye kura ya maoni wanaweza kufanya kazi ya kuwachimba
wenzao mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima faida na hasa thamani
inayoongezwa na kuanzisha utaratibu huo. Naomba tujiridhishe kama jambo
hili jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi kila miaka mitano kurudi kwa
wananchi hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo wa Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo
lingine kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo limevuta hisia za karibu
watu wote nchini linahusu muundo wa Muungano wetu kuwa wa Serikali tatu
badala ya mbili za sasa. Pendekezo hili limezua mjadala mkubwa tangu
lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza na kurudiwa katika Rasimu ya pili.
Wakati mwingine mjadala umekuwa mkali na wa hisia kali kwa kila upande.
Kwa kweli
hili ndilo jambo kubwa kuliko yote katika Rasimu kwa sababu
linapendekeza kuanzishwa kwa muundo na mfumo mpya wa kuendesha nchi
yetu. Hii ndiyo agenda mama ya Bunge hili ambayo kila Mtanzania
anasubiri kwa hamu uamuzi wenu utakuwa upi. Ombi langu kwenu ni kuwa
watulivu mnapojadili suala hili. Epukeni jazba ili mfanye uamuzi ulio
sahihi. Lazima mtambue uamuzi usiokuwa sahihi kwa jambo hili una hasara
kubwa. Tunaweza kupoteza kitu tulichokijenga kwa gharama kubwa kwa nusu
karne iliyopita. Tanzania inaweza kuwa nchi iliyojaa migogoro na
matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe;
Kama
alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba,
mara kadhaa, mjadala au madai ya kutaka muundo wa Serikali tatu si jambo
jipya. Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo ya kuunganisha nchi zetu
mbili mwaka 1964. Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya hewa ya
kisiasa Zanzibar mwaka 1984. Muundo huu uliwahi kupendekezwa na Tume ya
Nyalali mwaka 1992, ndiyo hoja ya G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia na
Tume ya Jaji Kisanga ya mwaka 1998. Lakini mara zote hizo mapendekezo
hayo hayakukubaliwa.
Waasisi
wa taifa letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri
ya Tanganyika wakati ule na Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa
Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wakati ule, waliamua kuchagua Muungano wa
Serikali mbili tulionao sasa. Walitoa sababu mbili kuu: "ni muundo
unaoihakikishia Zanzibar kuwa haimezwi na Tanganyika; na pia unaiepusha
Tanganyika kubeba mzigo mkubwa wa kugharamia Serikali ya Tanganyika na
ile ya Muungano".
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Natambua
kuwepo kwa rai ya kutaka Mwalimu Nyerere asitumiwe katika mjadala huu.
Nionavyo mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na
Sheikh Karume katika jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo kujadili na
kukubaliana kuwa mfumo wa Serikali mbili ndiyo bora kwa nchi yetu. Iweje
leo tunapozungumzia kuubadili, mawazo yao yawe hayafai kutumika au hata
kuzungumzwa. Hivi hasa mawazo ya nani pekee ndiyo bora zaidi kutumika?
Tutakuwa hatuutendei haki mjadala huu na sisi wenyewe tunaoshiriki
katika mchakato huu. Rai yangu kwenu ni kuwa mzitazame hoja zote kwa
marefu na mapana yake ili mpime kama zipo sababu za kuubadili muundo wa
sasa wa Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa Serikali tatu. Na, kama
zipo mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye uamuzi kwa utambuzi na hoja
zenye mashiko. (you must make an informed decision).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume
imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu. Sababu
ya kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote Zanzibar na
Tanzania Bara. Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania waliotoa maoni,
yaani asilimia 60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga mkono muundo wa Serikali
ya Mkataba, na asilimia 61.3 wa kutoka Tanzania Bara wanaunga mkono
muundo wa Serikali tatu. Sababu ya pili ni kwamba muundo huo unatoa
majawabu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa
Serikali mbili zinazonung'unikiwa na watu wa pande zetu mbili za
Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sababu
hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii.
Wapo wanaokubaliana na Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema
Tume imesema kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono muundo wa
Serikali tatu, hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki. Ndiyo matakwa
ya wengi hivyo msemo wa Kiswahili usemao wengi wape uheshimiwe.
Lakini
wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo. Wanasema kuwa
taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa Tume
kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi 47,820 au
sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo
wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa
Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa.
Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni
wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanasema
pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na
67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu
Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo
waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali
mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7
walipendekeza Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka
Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Takwimu
za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211.
Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano
na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine. Hivyo basi
wanahoji pia kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo
linalowakera Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu
waliotoa maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo
hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya
watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia
10.4 ya maoni yote. Hivyo basi, wanauliza "usahihi wa hoja ya Watanzania
wengi kutaka Serikali tatu uko wapi?"
Changamoto za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Kama
nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa kuhusu kufaa
kwa muundo wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu unajibu changamoto
nyingi za muundo wa Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri changamoto za
muundo wa Serikali mbili. Kwa upande wa Zanzibar wanalalamikia kile
kinachoitwa Tanzania Bara kuvaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na hivyo kutumia mamlaka ya Serikali ya Muungano kujinufaisha yenyewe.
Fursa hiyo Zanzibar hainayo. Aidha, wanasema mipaka na mamlaka ya
Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na kwa mambo ya Tanzania
Bara haijaainishwa vizuri ikaeleweka. Wazanzibari pia, wanazungumzia
mkanganyiko kuhusu ugawanaji wa mapato, na jinsi ya kuchangia shughuli
za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia Rais wa Zanzibar kuondolewa kuwa
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Aidha,
kuna malalamiko kuwa orodha ya mambo ya Muungano iliyoongezwa kutoka
mambo 11 mwaka 1964 mpaka 22 mwaka 1992 imepunguza uhuru wa Zanzibar kwa
mambo yake ya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa
upande wa Tanzania Bara, Tume inaeleza kuwepo kwa manung'uniko kuwa
Muungano wa Serikali mbili umepoteza utambulisho wa kihistoria wa
Tanganyika na fursa ya watu wa upande wa Tanzania Bara kutetea maslahi
yao ndani ya Muungano. Wanasema Zanzibar sasa imekuwa nchi huru; ina
bendera yake, wimbo wake wa taifa na Serikali yake. Aidha, wanasema
Zanzibar imebadili Katiba na kujitambulisha kama nchi na kuchukua
madaraka ya Bunge la Muungano, kwa vile Sheria zinazotungwa na Bunge
lazima zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi kupata kibali cha kutumika
Zanzibar. Wananchi wa Tanzania Bara pia wanalalamikia kutokuwa na haki
ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa kutoka Zanzibar wanayo haki
hiyo Tanzania Bara. Na wao vilevile wananung'unikia mkanganyiko kuhusu
ugawaji wa mapato na jinsi ya kuchangia gharama za uendeshaji wa
shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Zanzibar. Hizi ndizo baadhi ya changamoto ambazo Tume inaona jawabu lake
ili kuzitanzua ni kubadili muundo wa Muungano kuwa wa Serikali tatu
badala ya mbili za sasa.
Faida za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume ya
Mabadiliko ya Katiba imefafanua kwamba mfumo wa Serikali tatu utagawanya
vizuri madaraka kati ya mamlaka tatu za Muungano. Unawezesha Washirika
wa Muungano kubaki na utambulisho wao wa kihistoria na kiutamaduni na
hivyo, utawezesha kuondoa hisia za Zanzibar kumezwa na Muungano. Pia
unawezesha kila upande wa Tanzania kuendesha mambo yake yasiyo ya
Muungano kadri wanavyoona inafaa. Vile vile unaweza ukaleta ushindani wa
kimaendeleo baina ya washirika na hivyo kusaidia kukuza maendeleo ya
nchi.
Faida za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na
kuainisha changamoto za muundo wa Serikali mbili na kupendekeza kuwa
muundo wa Serikali tatu ndio utakaosaidia kuzitatua, Tume haikuacha
kutambua manufaa na mchango muhimu uliotolewa na muundo wa Serikali
mbili kwa nchi yetu. Tume inasema kuwa muundo wa Serikali mbili
unapunguza gharama za uendeshaji wa shughuli za umma. Umesaidia kujenga
uhusiano na ushirikiano mzuri katika nyanja mbalimbali baina ya wananchi
wa pande zetu mbili za Muungano. Umezuia mkubwa kummeza mdogo; na
umedumisha Muungano mpaka kuufikisha hapa ulipo tangu kuasisiwa kwake
takriban miaka 50 iliyopita (1964). Aidha, umesaidia kudumisha amani,
umoja na utulivu hapa nchini.
Changamoto za Muundo wa Serikali Tatu
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Pamoja na
kuelezea ubora wa muundo wa Serikali tatu kama jawabu kwa changamoto za
Serikali mbili, Tume inakiri kuwa hata muundo huu nao una changamoto
zake. Kwanza kabisa, Taarifa ya Tume inaeleza kuwa kutakuwa na gharama
kubwa za uendeshaji wa shughuli za umma. Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba
alitutoa hofu kuhusu gharama ingawaje mwaka 1993, Mwalimu alikuwa na
mawazo tofauti. Alisema kwamba: "watu ...wanaodhani kuwa gharama ya
Serikali yo yote kati ya hizo ingekuwa ndogo, (Waulizeni Wazanzibari) na
wala gharama ya Serikali ya Shirikisho isingekuwa ndogo hata bila
gharama ya mambo yasiyo ya Shirikisho". Ni matumaini yangu kwamba katika
mjadala wenu mtajipa nafasi ya kulitafakari suala hili kubwa na nyeti.
Tume
imesema pia kwamba, Muundo huu, unaweza kuibua tatizo la uchangiaji wa
gharama za uendeshaji wa shughuli za umma baina ya nchi washirika.
Vilevile, kuna uwezekano wa kuwepo sera zinazokinzana au kutofautiana
juu ya masuala ya msingi ya nchi na kuzua mgogoro kati ya washirika wa
Muungano na baina ya nchi washirika na Serikali ya Muungano. Aidha, upo
uwezekano mkubwa kwa muundo huu kuleta tofauti za kimaendeleo baina ya
pande mbili za Muungano kutokana na kila upande kuwa na sera na mipango
tofauti.
Tume pia
imeelezea hatari ya muundo wa Serikali tatu kukuza hisia za utaifa
(nationalistic feelings) kwa nchi washirika, hivyo kuweza kudhoofisha
Muungano. Muundo huu pia unaweza kuleta misuguano (paralysis and
deadklocs in decision making) katika kufanya uamuzi juu ya masuala
muhimu ya kitaifa. Changamoto hizo si tu zinaweza kuwa tishio kwa ustawi
wa Muungano bali pia hata uhai wake. Kwa ajili hiyo kuchagua muundo wa
Serikali tatu kuna maana ya kufanya kazi ya ziada ya kuzikabili
changamoto hizi ili zisiue Muungano wenyewe. Changamoto ambazo si ndogo
hata kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanaounga
mkono muundo wa Serikali mbili wanasema kuwa kwa mlolongo huu wa
changamoto zilizoainishwa na Tume yenyewe, unadhihirisha kuwa muundo wa
Serikali tatu hautapunguza matatizo ya Muungano wetu bali utayaongeza
maradufu kuliko ilivyo sasa. Wanakiri kuwepo kwa changamoto katika
muundo wa sasa wa Muungano. Hata hivyo, wanaamini zinaweza kushugulikiwa
na kupatiwa ufumbuzi bila ya kuhitaji kuwa na Serikali ya tatu. Wanatoa
mifano kadhaa ya jinsi Serikali zetu zilivyoshughulikia changamoto za
Muungano katika kipindi cha uhai wake na mafanikio yaliyopatikana.
Katika
kushughulikia kero za Muungano, Serikali zetu mbili ziliunda Tume ya
Shelukindo mwaka 1992 na Kamati ya Pamoja ya Serikali zetu mbili mwaka
1993. Mambo mengi yaliyoainishwa katika Tume ya Shelukindo na Kamati ya
Pamoja yameshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi. Kwa upande wa kero
zilizoelezwa kwenye Tume ya Shelukindo, ilipofikia mwaka 2006 yalikuwa
yamebakia mambo 13 kati ya 31. Kwa jumla, kwa kero zilizoibuliwa na Tume
ya Shelukindo na Kamati ya Pamoja, hivi sasa yamesalia mambo sita tu.
Kimsingi ni mambo yahusuyo maslahi ya kiuchumi na yote yapo katika hatua
nzuri za kuyamaliza. Mambo hayo ni:
Mgawanyo wa mapato:
Hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki
Mgawanyo wa Mapato yatokanayo na faida ya Benki Kuu.
Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano.
Usajili wa vyombo vya moto.
Tume ya Pamoja ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali
zetu mbili zimeamua kwa dhati kutumia fursa ya mchakato huu wa
mabadiliko ya Katiba kuyamaliza yale yanayohitaji kuingizwa kwenye
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mambo hayo ni matatu
yafuatayo:
Utafutaji na uchimbaji mafuta na gesi asili.
Ushirikiano wa Zanzibar na taasisi za nje.
Tume ya Pamoja ya Fedha.
Matatu
mengine yatamalizwa kwa kutumia taratibu za kiutawala. Hali kadhalika,
katika kipindi cha mpito kinachopendekezwa na Tume yaani 2015 – 2018 ni
nafasi nzuri ya kushughulikia masuala yenye migongano kati ya Katiba ya
Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano. Mimi naishi kwa matumaini na kwa
vile tunayo dhamira njema ya kuimarisha Muungano wetu, naamini tutaweza
kuziondoa tofauti zilizopo.
Orodha ya Mambo ya Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kuhusu
orodha ya mambo ya Muungano kuwa 22 badala ya 11 ya awali, napenda
kuwahakikishia kuwa Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar hazina kigugumizi wala upungufu wa dhamira ya kisiasa ya
kuyapunguza yale yanayopunguzika. Napenda kwanza kabisa, ieleweke kuwa
kilichoongeza orodha hiyo si hila za Serikali ya Muungano kutaka
kupunguza madaraka ya Zanzibar kwa mambo yake ya ndani. Na, wala siyo
udhaifu wa viongozi wa Zanzibar katika kutetea maslahi ya nchi yao. La
hasha.
Pili,
naomba ieleweke kuwa, kila kilichoongezwa katika Orodha ya Mambo ya
Muungano kilikuwa na sababu inayoeleweka, inayoelezeka na iliyokubalika
na pande zote mbili za Muungano. Hakuna hata jambo moja lililoingizwa
kwenye Katiba kwa kificho. Taratibu stahiki za kikatiba na kisheria
zilifuatwa. Hoja ziliwasilishwa Bungeni na kujadiliwa kwa uwazi na
uamuzi ulifanywa na Bunge kwa kuzingatia kanuni ya theluthi mbili ya
kura za kila upande wa Muungano. Kumbukumbu zipo katika Hansard za Bunge
la Muungano, ambazo ziko wazi kwa kila mtu anayetaka kuzisoma asome.
Nashauri mkazisome ili mpate kujua ukweli na undani wa kila
kilichoongezwa na sababu za kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nchi zetu
mbili zilipoungana mwaka 1964 na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
kulikuwa na mambo 11 kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Mambo hayo ni
haya yafuatayo:
Katiba ya Jamhuri ya Muungano,
Mambo ya Nje,
Ulinzi,
Polisi,
Hali ya Hatari,
Uraia,
Uhamiaji,
Biashara ya nje na mikopo,
Utumishi katika Serikali ya Muungano,
Kodi ya Mapato, Kodi ya Makampuni, Ushuru wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa,
Bandari, Mambo ya Anga, Posta na Simu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kati ya
mwaka 1965 na 1992 mambo ya Muungano yaliongezeka kutoka 11 hadi kufikia
22, kimsingi kutokana na mambo mbalimbali yaliyotokea nchini na kwenye
ukanda wetu wa Afrika Mashariki. Pande zetu mbili za Muungano
zilikubaliana kuwa mambo hayo yaongezwe katika Katiba na taratibu za
kisheria na Kikatiba zilifuatwa. Kwa idhini yako naomba nitoe maelezo
kwa ufupi kwa yale yaliyoongezwa na kitu kilichosababisha mabadiliko
hayo kufanywa.
Jambo la
kwanza kuongezwa, yaani la 12 lilikuwa ni "sarafu, mabenki na fedha za
kigeni". Hii ilifanyika tarehe 10 Juni, 1965 kufuatia kuvunjika kwa Bodi
ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Board) mwaka 1964.
Kwa ajili hiyo, kila nchi mwanachama wa Jumuiya ililazimika kuwa na
sarafu yake na mipango yake ya kusimamia mambo yake ya kibenki na fedha.
Serikali zetu mbili zilikubaliana masuala hayo yashughulikiwe na
Serikali ya Muungano na Muswada husika wa Bunge uliidhinishwa kuwa
Sheria na Mzee Abeid Amani Karume aliyekuwa akikaimu Urais tarehe 10
Juni, 1965.
Tarehe 11 Agosti, 1967 yaliongezwa mambo yafuatayo kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano:-
Leseni za Viwanda na Takwimu, (Jambo la 13)
Elimu ya Juu, (Jambo la 14)
Jambo la
15 lilikuwa ni mambo yote yaliyokuwa kwenye Nyongeza ya 10 ya Mkataba wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nyongeza hiyo ilikuwa na mambo 27 ambayo
Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la uratibu. Mambo hayo ni pamoja na
Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, Utabiri wa Hali ya Hewa,
Utafiti, Vipimo na Mizani, Huduma ya Usafiri wa Reli, Barabara, Usafiri
wa Majini na kadhalika.
Tarehe 22
Julai, 1968 "rasilimali ya mafuta, petroli na gesi asilia" iliongezwa
kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa jambo la 16. Kimsingi
Serikali ya Muungano ilipewa jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na gesi
asilia kwa ajili ya nchi nzima. Baada ya kupanga upya Orodha ya Mambo
ya Muungano, suala la rasilimali ya mafuta likawa la 15.
Tarehe 22
Novemba, 1973 Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa na kuwa jambo la
16. Hii ilifuatia kuvunjika kwa Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki
mwaka 1971 na hivyo nchi yetu kulazimika kuunda Baraza la Mitihani la
Taifa mwaka 1973.
Mwaka
1984 yalipofanyika mabadiliko makubwa katika Katiba ya mwaka 1977,
Orodha ya Mambo ya Muungano ilipangwa upya. Mambo yaliyokuwemo kwenye
Nyongeza ya 10 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuorodheshwa kama Jambo
la 15 katika Orodha ya Mambo ya Muungano yalipunguzwa na kubaki matano.
Mambo hayo yalipewa namba kama ifatavyo:- Usafirishaji wa Anga kuwa
Jambo la 17, Utafiti kuwa la 18, Utabiri wa Hali ya Hewa kuwa la 19 na
Takwimu kuwa la 20 na Mahakama ya Rufani ya Tanzania ikawa jambo la 21.
Tarehe 17
Mei, 1992 likaongezwa jambo la "Uandikishaji wa Vyama vya Siasa" na
kuwa jambo la 22. Hii ilifuatia kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama Vingi vya
Siasa na hasa uamuzi kuwa vyama vitakuwa vya kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Bila ya
shaka maelezo haya yatasaidia kuelezea nini kimeongezwa na mazingira ya
kuongezwa kwake ni yepi. Kulikuwepo na sababu za msingi na wala siyo
hila ya namna yo yote ile iliyofanywa na mtu ye yote mwenye nia mbaya na
Zanzibar. Kama tulivyoona mambo mengi yalihusu kilichokuwa kinatokea
ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kila yalipotokea mabadiliko katika
uendeshaji wa shughuli za Jumuiya ya Afrika Mashariki, huduma
zilizokuwa zikitolewa na Jumuiya zilikabidhiwa Serikali ya Muungano
kubeba kwa sababu ya uwezo wake mkubwa wa kiuchumi. Yale yaliyokuwa
yanagusa sehemu zetu mbili za Muungano yaliingizwa katika Orodha ya
Mambo ya Muungano. Mengineyo yaliachiwa kila upande kushughulikia
ilivyoona inafaa. Kwa maana hii basi, mambo ambayo yalitokana na uamuzi
wetu wenyewe ni mawili tu. Mambo hayo ni rasimali ya mafuta na gesi
asilia (1968), na uandikishaji wa vyama vya siasa (1992).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni
msimamo wa Serikali zetu mbili, tangu mwanzo mpaka leo kwamba, iwapo
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshajenga uwezo wake wa kufanya
baadhi ya mambo katika Orodha ya Mambo ya Muungano ipewe uhuru wa
kufanya hivyo. Lililo muhimu ni kuwa zisiondolewe tunu zenyewe za
Muungano wetu. Ndiyo maana, mambo kama vile bandari, takwimu, kodi ya
mapato, leseni za biashara, utafiti na mengineyo, yanasimamiwa na
kuendeshwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuwemo kwenye
Orodha ya Mambo ya Muungano. Imekuwa hivyo kwa miaka kadhaa sasa na
imethibitika kuwa Zanzibar inayamudu. Ni makusudio yetu kutumia fursa ya
mchakato huu sasa kuyaondoa rasmi mambo hayo na mengineyo
tutakayokubaliana kutoka kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano.
Rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa ajili
hiyo tumekubaliana kuliondoa suala la rasilimali ya mafuta na gesi
asilia lisiwe jambo la Muungano. Jambo hili tulishakubaliana tangu
wakati wa Rais Amani Abeid Karume tuliondoe na hata alipokuja Rais Shein
msimamo haukubadilika. Kilichotuchelewesha kutekeleza ni kuibuka kwa
fikra za kuwa na mchakato huu wa Katiba mpya. Tuliona kuwasilisha
Bungeni Muswada wa Sheria wa kuondoa jambo hili katikati ya mchakato
huu, ingeweza kuzua matatizo yasiyokuwa ya lazima. Tungeulizwa haraka ni
ya nini tungeweza kukosa majibu.
Hatimaye
wakati wake wa kulimaliza suala hili sasa umefika. Misemo ya wahenga ya
"subira yavuta heri" na "kawia ufike" imetuongoza vyema tumefika mahali
tunaweza kufanya hivyo. Zipo sababu mbili zilizotushawishi kuamua kuitoa
rasilimali hii kwenye Orodha ya Mambo ya Muungano. Kwanza kwamba, siku
hizi Serikali haiagizi mafuta. Kazi hiyo hufanywa na makampuni binafsi.
Pili, kwamba, rasilimali ya mafuta na gesi yakipatikana Zanzibar ni
suala la kiuchumi ambalo lipo kwenye mamlaka ya Zanzibar kama ilivyo
karafuu, hiliki, mwani na kadhalika. Au kama ilivyo dhahabu, gesi,
pamba, kahawa na kadhalika kwa upande wa Tanzania Bara. Hivyo, Zanzibar
iachwe kumiliki rasilimali yake ya kiuchumi.
Zanzibar na Ushirikiano wa Kimataifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo
lingine muhimu ambalo Serikali zetu mbili zimelizungumza na kukubaliana
tulitafutie ufumbuzi ni kuhusu Zanzibar kupata fursa ya kujiunga na
mashirika ya kimataifa, kukopa na kupata misaada kutoka nchi za nje bila
kizuizi. Kwa sasa fursa hiyo ina vikwazo vya namna mbalimbali. Ni
ukweli usiopingika kuwa jambo hili limechangia kwa kiasi kikubwa kujenga
hisia hasi kuhusu Muungano kwa upande wa Zanzibar. Aidha, limechangia
sana kuchafua hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar kwa nyakati mbalimbali.
Hata zile kauli kwamba Tanzania Bara imejificha kwenye koti la Serikali
ya Muungano, na kutaka itoke ionekane ili iache kunufaika isivyostahili,
zinazochangiwa sana na mazingira haya iliyonayo Zanzibar. Serikali zetu
mbili zinaamini kuwa mambo haya yakipatiwa ufumbuzi tutakuwa tumeondoa
kizingiti kikubwa katika ustawi wa Muungano wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
tumekubaliana kuwa, tutumie fursa za mchakato huu kuyamaliza mambo haya
yaishe! Bahati nzuri dhana iliyopo katika Ibara ya 65(2) ya Rasimu
inatoa jawabu mwafaka kwa tatizo hili. Tukikubaliana, itaipa Zanzibar
"uwezo na uhuru wa kuanzisha uhusiano na ushirikiano na jumuiya au
taasisi yo yote ya kikanda na kimataifa kwa mambo yaliyo chini ya
mamlaka yake kwa mujibu wa Katiba ya nchi" bila kizuizi. Ni maoni ya
Serikali zetu mbili kuwa fursa hiyo inaweza kutolewa kwa Zanzibar bila
ya kulazimika kuwa na muundo wa Serikali tatu. Hatuuoni ulazima huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa maoni
yangu kitu kingine muhimu cha kufanya ni kuongeza msukumo,
utakaohakikisha kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha inatimiza ipasavyo majukumu
yake. Wanaohusika na utekelezaji wa maamuzi yake wabanwe ipasavyo
kutimiza wajibu wao. Iwekwe mifumo na masharti katika sheria au Katiba
ya kuwabana watekelezaji kwa ajili hiyo. Hali kadhalika ihakikishwe
kuwa, Akaunti ya Pamoja inaanzishwa bila ajizi na kutumika na pande
zote. Aidha, mfumo wa mawasiliano na ushirikiano baina ya Serikali zetu
mbili yaani Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar, upewe nguvu ya kisheria na kama hapana budi upewe
nguvu ya Kikatiba. Tukifanya hivyo tutafanikiwa kuyaweka mambo yote sawa
hata bila ya kuhitaji kuunda Serikali ya tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Katika
mjadala kuhusu mapendekezo ya kuwa na muundo wa Muungano wenye Serikali
tatu, wananchi wametoa maoni na mapendekezo mengi mazuri kuhusu
changamoto za Serikali tatu zilizoainishwa na Tume na namna ya
kuzitatua. Tena yapo maoni ya watu wanaopenda muundo wa Serikali tatu na
wasiopenda muundo wa Serikali tatu. Nawaomba myatafakari kwa uzito
unaostahili. Yapo mambo muhimu ya kuyatafutia ufumbuzi. Kwanza, kwa
mfano ni ile hoja kwamba Serikali ya Muungano inayopendekezwa
haikujengeka kwenye msingi imara. Haina nguvu yake yenyewe za kusimama.
Inategemea mno ihsani ya nchi washirika. Kwa sababu hiyo inaweza
kuanguka wakati wowote, na Muungano kusambaratika, iwapo itakosa ihsani
ya nchi washirika. Tena inaweza kuwa hivyo hata kama ni mmoja wa
washirika amefanya hivyo.
Pili,
kwamba, haielekei Serikali hiyo ina chanzo cha uhakika cha mapato ya
kuiwezesha kusimama yenyewe na kutekeleza majukumu yake. Ushuru wa
bidhaa unaopendekezwa unatiliwa shaka kuwa hautatosheleza mahitaji. Pia,
kwamba, hakuna uhakika wa fedha hizo kupatikana kwa vile, Serikali ya
Muungano haina chombo chake chenyewe cha kukusanya mapato hayo.
Itategemea vyombo vya nchi washirika kuikusanyia na kuipelekea. Kuna
hatari ya shughuli za Serikali ya Muungano kusimama wakati wo wote au
hata kusimama kabisa kwa sababu ya nchi washirika kuchelewa au kushindwa
kuwasilisha makusanyo ya kutoka kwao.
Bahati
mbaya Serikali ya Muungano haina uwezo wala nyenzo za kuhakikisha kuwa
mapato yake yanawasilishwa. Serikali hiyo haina mamlaka ya kuzibana nchi
washirika kuwasilisha au kuziwajibisha zisipofanya hivyo. Katika
mazingira hayo ni rahisi kwa Serikali ya Muungano kukwama na kushindwa
kutekeleza majukumu yake. Huu ni muundo ambao inakuwa ni rahisi sana kwa
Muungano kuvunjika.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
Rasimu ya Katiba, Serikali ya Muungano inapewa fursa ya kukopa kama
chanzo cha kujipatia mapato ya kuendesha shughuli zake. Lakini, kwa
sababu ya kukosa rasilimali zake yenyewe, huenda ikawa vigumu kwa
Serikali hiyo kukopesheka. Kwa jumla hii ni Serikali ambayo ukuu wake
hauna nguvu iliyo thabiti, na watu wengine wanaona kama vile ukuu huo
haupo kabisa. Akitokea kiongozi ye yote wa nchi washirika akatunisha
misuli dhidi ya Rais wa Muungano au kupinga maamuzi ya Serikali au
chombo cha Muungano, Rais na Serikali yake watakuwa hawana lo lote la
kufanya. Kwa kweli uhai wa Muungano katika muundo wa Serikali tatu ni wa
mashaka makubwa.
Hofu hizi
kuhusu udhaifu wa Serikali ya Muungano chini ya mfumo wa Serikali tatu
unaopendekezwa, zinawasumbua hata wale wanaopendelea mfumo wa Serikali
tatu kuwepo. Wao wangependa iwepo Serikali ya Muungano yenye nguvu na
inayoweza kusimama yenyewe kwa kujitegemea. Wanaona kilichopendekezwa
hakitoi matumaini hayo. Hii ina maana kuwa lazima mawazo bora zaidi
yatolewe ili kupata Serikali ya tatu yenye ukuu unaoonekana na inayoweza
kusimama yenyewe bila kuwa tegemezi na egemezi kwa nchi washirika. Pia
inaweza kuwa nguzo ya kutegemewa na nchi washirika. Bila ya shaka Bunge
hili likiamua tufuate mfumo huo linaweza kuonyesha njia ya kuondoa hofu
hizo. Kwa waumini wa Serikali mbili wanaona kuwa huu ni uthibitisho wa
ubora wa muundo wa Serikali mbili.
Changamoto za Hisia za Utaifa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika
kuainisha changamoto za muundo wa Serikali tatu, Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imeyataja mambo mengine mawili makubwa ambayo ningependa
Waheshimiwa Wajumbe muyape tafakuri stahiki. Mambo hayo ni mosi,
misuguano na mikwamo (deadlocks and paralysis) katika kujadili na
kufanya uamuzi kuhusu mambo muhimu ya Muungano. Na pili, ni kuibuka kwa
hisia za utaifa (nationalistic sentiments) wa zamani kwa nchi washirika.
Nawaomba myatafakari kwa makini sana mambo haya, kwa sababu ya uwezo
wake mkubwa wa kuhatarisha siyo tu ustawi na uhai wa Muungano, bali hata
usalama wa raia na mali zao. Naona hata Tume haikuweza kupata ufumbuzi
ulio mwafaka kabisa kwa changamoto hizi. Bila ya shaka katika mijadala
yenu Waheshimiwa Wajumbe mnaweza kusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ni lazima
lifanyike kila linalowezekana kuhakikisha kuwa maamuzi hayakwami kwani
yakikwama maana yake shughuli za Muungano zitakuwa zimekwama. Kama
hazitakwamuliwa kwa wakati ustawi wa Muungano utaathirika. Ikishindikana
kabisa kupatikana ufumbuzi Muungano unaweza kuvunjika. Kuibuka na kukua
kwa hisia za utaifa (nationalistic feelings) kwa nchi washirika, yaani
Utanganyika na Uzanzibari ni tishio kubwa sana kwa uhai wa Muungano.
Hebu fikiria, watu walioishi pamoja kidugu na kwa kushirikiana, kama
watu wamoja na raia wa nchi moja yaani Watanzania kwa miaka 50, kuja
kujikuta uhusiano wao kuwa ni kati ya Watanganyika na Wazanzibari na
siyo kati ya Watanznaia. Kwa mujibu wa sensa iliyopita takriban asilimia
90 ya Watanzania waliopo sasa wamezaliwa baada ya mwaka 1964. Nchi
wanayoijua ni Tanzania. Litakuwa ni jambo lenye mshtuko mkubwa na athari
zisizoweza kutabirika, watu hao watakapojikuta ni wageni wanaotakiwa
kutengenezewa utaratibu maalum wa kusafiri na kuishi wakiwa upande wa
Muungano ambao siyo kwao kwa asili. Wanakuwa wageni na fursa walizokuwa
wanazipata waendapo popote haiwi rahisi tena kuzipata.
Katika
mazingira hayo ni rahisi sana chuki kupandikizwa na watu waliokuwa ndugu
mara moja watajikuta maadui. Aidha, watu wanaweza kujikuta wakilazimika
kurudi kwao kwa asili ama kwa kufukuzwa au kwa sababu ya mazingira kuwa
magumu kiasi cha kuona bora waondoke. Watu hao wanaweza kulazimika
kuondoka huku wakiacha nyuma kila kitu walichokichuma maishani.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Changamoto
hizi kubwa mbili za mfumo wa Serikali tatu ambazo Tume imeziona, ni za
kweli. Si mambo ya kufikirika. Yale yaliyowakuta watu wenye asili ya
Tanzania Bara ya kuchomewa moto biashara zao Zanzibar mwaka 2012 na watu
wenye hisia kali za Uzanzibari, na kuwataka watu wa Bara waondoke
Zanzibar, huenda yakawa madogo. Matukio ya namna hii yanaweza kutokea
pande zote mbili na kusababisha maafa makubwa. Itaanza baina ya watu,
baadaye itakuwa baina ya Serikali zetu mbili na kuzifikisha nchi zetu
mbili zilizokuwa ndugu na rafiki, kwa nusu karne, ghafla kuwa maadui
wasioombana chumvi na wasiotakiana heri. Umoja wetu utatetereka na
Muungano wetu unaweza kuvunjika. Kwa nini tufike huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sisi
viongozi tuliopewa dhamana ya kuamua kwa niaba ya wananchi wetu, hatuna
budi kuyapima mambo haya kwa umakini mkubwa ili tufanye uamuzi ulio
sahihi. Tusije tukajutia uamuzi wetu tutakapoona watu wanafukuzana,
wanauana na mali zao kuporwa. Na, tukifikia hatua hiyo Muungano
kusambaratika halitakuwa jambo la ajabu.
Kwa
kweli, unapoyatafakari haya, ni rahisi kuelewa kwa nini wazee wetu
waasisi waliamua walivyoamua. Waliona mbali. Tusipuuze fikra zao na
maono yao. Kuna hatari ya nchi yetu na watu wake kupoteza kila kitu
tulichokijenga kwa miaka 50. Badala ya kujenga tunaweza kujikuta
tumebomoa hata msingi katika nchi washirika. Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Nyerere mwaka 1993 alituasa kuhusu hatari hiyo: "Hamuwezi kutenda
dhambi kubwa namna hiyo bila adhabu... na adhabu nyingine zimo mle mle
ndani ya kitendo hazisubiri."
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Siku moja
kiongozi mmoja wa juu wa madhehebu ya dini nchini aliniuliza: "Hivi
Serikali mbili zikiwa na matatizo jawabu ni kuongeza ya tatu? Si
matatizo ndiyo yatazidi? Je, matatizo yakizielemea hizo Serikali tatu si
kila mtu atachukua njia yake? Mtakuwa mmepoteza kila kitu. Mimi
nawashauri msichoke kutafuta majawabu kwa matatizo ya hizi mbili! Huko
mnakotaka kwenda kuna hatari nyingi".
Pengine na ushauri huu wa mtu wa Mungu nao ni vyema kuupa nafasi na kuutafakari.
Kazi Yenu Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Mambo ya
kuyasemea ni mengi mno lakini kwa sababu ya ufinyu wa muda, nisingeweza
kuyazungumzia yote. Naamini, mtayaona katika kuipitia Rasimu na kwenye
majadiliano yenu. Napenda kusisitiza kwenu kuwa kazi iliyo mbele yenu ni
kubwa sana. Ni kubwa kwa maana mbili. Kwanza, jukumu lenyewe la kutunga
Katiba ya nchi ni zito sana. Taswira ya nchi yetu itakuwaje na
itaendeshwa vipi kwa miaka mingi ijayo iko mikononi mwenu. Ipeni nchi
yetu hatima njema. Pili, ni kubwa kwa maana ya uzito wa mambo ya
kujadili na kuyafanyia uamuzi. Kwa ajili hiyo, ni muhimu sana kuisoma
Rasimu na Taarifa ya Tume kwa makini na kuzielewa. Jipeni muda wa
kutafakari kila neno, kila sentensi, na kila dhana ili muweze kufanya
uamuzi ulio sahihi. Mkifanya hayo mtakuwa mmeisaidia nchi yetu na
Watanzania wote kupata Katiba nzuri.
Nimefarijika
sana kusikia kuwa mtajigawa kwenye Kamati 12 wakati wa kujadili Rasimu.
Huu ni utaratibu mzuri kwani mkiwa katika vikundi vya watu wachache,
mtakuwa na mijadala ya kina zaidi. Watu wote wanaweza kupata fursa ya
kutoa maoni yao, kwa kila kifungu na kila jambo linaloibuliwa na
kuzungumzwa. Kwa kufanya hivyo, mtatimiza kwa ukamilifu jukumu lenu la
kutunga Katiba. Wote mtakuwa mmeshiriki kujadili kila sura na vipengele
vyake vyote. Mkimaliza kazi yenu mtapokea kwa haki sifa nzuri kama
Katiba itakuwa nzuri, au lawama stahiki iwapo itakuwa kinyume chake.
Pongezi kwa Mwenyekiti wa Muda
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama nitamaliza hotuba yangu bila ya kutambua kazi
nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la
Wawakilishi, alipokuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hili. Kazi yake
haikuwa rahisi hata kidogo, lakini kwa umahiri na ustadi mkubwa ameweza
kufanikisha mambo kwa kiasi ambacho anastahili pongezi zetu sote.
Anastahili pongezi kwa sababu yeye aliendesha Bunge hili bila ya kuwepo
kwa kanuni. Tatizo hili hatakuwa nalo Mwenyekiti wa Kudumu kaka yangu
Mheshimiwa Samuel Sitta.
Napenda
pia kuwapongeza Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa hatua
mliyofikia. Hata hivyo, mmechukua muda mwingi katika hatua ya awali
hivyo hamna budi kuongeza kasi. Naomba niwakumbushe kuwa mijadala yenu
hii inafuatiliwa kwa karibu sana na Watanzania. Wamewekeza sana
matarajio yao kwenu. Hamna budi, haiba na taswira ya uongozi muionyeshe
wakati wote wa kuendesha mijadala yenu kwa lugha na vitendo vyenu.
Wakati wa semina na mjadala wa kupitisha Kanuni za Bunge hili, baadhi ya
wananchi wamekwazika sana na mwenendo wa baadhi ya Wajumbe.
Hawakutegemea kuyaona matendo waliyoyaona mkifanya na kusikia maneno
waliyoyasikia kutoka kwenye vinywa vya baadhi yenu.
Ni
matumaini yangu na ya Watanzania wote kuwa hali ile haitajirudia tena
katika awamu hii. Tusiwafikishe mahali Watanzania wakakata tamaa na
Wajumbe wao au na hata chombo hiki muhimu sana kwa mustakabali wao na wa
nchi yao. Tutoe hoja badala ya kupiga kelele (argue don't shout) au
kuzomea. Hakuna haja ya kutumia lugha isiyokuwa ya staha katika
kujieleza. Hakuna haja ya kukingiana ngumi, kutishiana hili na lile au
hata kugombana. Ni utovu wa uungwana usiotegemewa kutoka kwenu.
Tusiwaangushe wananchi wa Tanzania wanaotutegemea sana.
Wekeni Maslahi ya Taifa Mbele
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Ombi
langu la mwisho kwenu ni kuwasihi kuwa wakati wote muongozwe na kujali
maslahi mapana ya nchi yetu na watu wake badala ya kujali maslahi yenu
binafsi au ya makundi yenu. Naomba kaulimbiu yenu iwe "Tanzania Kwanza".
Najua kila mmoja wenu amekuja na maoni yake au atakuwa nayo kwa kila
jambo litakalojadiliwa. Wengine wamepewa misimamo na vyama vyao au
makundi yao. Si jambo baya na ni hatua muhimu ya kuleta mafanikio, kama
misimamo hiyo na mawazo hayo ni ya kujenga.
Hata
hivyo, mnachotegemewa kufanya ni kuwa tayari kuwianisha na kuunganisha
mawazo yenu mazuri na ya wenzenu, ili kupata msimamo wa pamoja na uamuzi
wa pamoja ulio bora. Kwa sababu hiyo, hamna budi kuwa tayari kusikiliza
mawazo ya wengine, hata kama ni tofauti na yenu mliyokuja nayo.
Tafuteni kilicho chema kwa yale yanayosemwa na watu wengine hata kama ni
watu usiokubaliana nao au huwapendi au hampendani. Kunaweza kuwepo kitu
chenye manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Nawaomba
muwe hodari wa kushawishi badala ya kulazimisha. Mkifanya hivyo
hamtalazimika kutumia muda mwingi wa kula njama za namna ya kuwazidi
maarifa wale mnaotofautiana nao kwa mawazo. Lazima pia mtafute namna ya
kushirikiana na kuwasiliana na makundi mengine. Msitafute kushindana,
hili ni jambo ambalo lazima wote mtoke hapa mkiwa washindi. Yaani lazima
Watanzania wote washinde kwani wao ndiyo wenye Katiba yao. Nawapongeza
viongozi wa vyama vya siasa na asasi mbalimbali kwa kutambua na
kuthamini umuhimu wa kuwa na taratibu za mawasiliano, mashauriano na
ushirikiano. Daima muwe watu wa kutafuta maridhiano. Mmefanya vizuri
katika hatua ya awali. Mmejiwekea taratibu nzuri za kufanya hayo,
tafadhalini zitumieni. Jengeni madaraja imara zaidi katika awamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Naomba
nimalize kwa kuwaomba Watanzania wote tukiongozwa na viongozi wetu wa
dini tumuombe Mola wetu ajalie rehema zake ili mchakato wa kutunga
Katiba uende salama. Aliongoze Bunge hili na Wajumbe wake waweze kufanya
uamuzi ulio sahihi na wenye manufaa kwa taifa letu kwa kila
watakaloliamua.
Baada ya
kusema maneno yangu mengi hayo, nirudie kukushukuru Mheshimiwa
Mwenyekiti kwa kunipa fursa hii adhimu ya kulihutubia Bunge Maalum la
Katiba. Nawatakieni kila la heri na mafanikio mema. Katiba Mpya
Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Libariki Bunge Maalumu la Katiba!
Asanteni sana kwa kunisikiliza! (P.T)
No comments:
Post a Comment