Meli ya Korea Kaskazini yanaswa Libya
Wakuu nchini Libya, wamesema kuwa
wameikamata meli moja iliyokuwa na bendera ya Korea Kaskazini, ikiwa na
shehena haramu ya mafuta katika bandari inayodhibitiwa na waasi.
Msemaji wa shirika la kitaifa la
mafuta, amesema kuwa meli hiyo ilisimamishwa ilipokuwa ikijaribu kungoa
nanga na kwa sasa inasindikizwa katika bandari inayodhibitiwa na
serikali ya Libya.
Maafisa
wa serikali ya Libya waliisimamisha Meli hiyo ya Korea Kaskazini
ilipokuwa ikiondoka kutoka bandari inayodhibitiwa na waasi siku ya
Jumatatu ikiwa imesheheni mzigo usio rasmi wa mafuta ghafi.
Jeshi la nchi hiyo limethibitisha tukio hilo.
Waasi wa zamani wanaotaka kuitenga
eneo la Libya Mashariki, wamekuwa wakimiliki bandari ya Al-Sidra na
vituo vingine muhimu vya kuuzia bidhaa nje katika eneo hilo tangu Julai
mwaka uliopita.
Mnamo siku ya Jumamosi, walianza
kupakia shehena ya mafuta yasiyosafishwa ndani ya meli hiyo ya Korea
Kaskazini iitwayo Morning Glory, iliyokuwa imetia nanga katika bandari
ya Al-Sidra.
Viongozi walaani wizi wa mafuta
Kiwanda cha mafuta nchini Libya
Siku ya Jumatatu jeshi la wanamaji
lilizuilia meli hiyo ilipokuwa ikiondoka bandarini, huku amri ikitolewa
ielekezwe hadi katika bandari inayodhibitiwa na serikali.
Chama kikuu cha kisiasa nchini humo cha General National Congress, GNC, kimethibitisha kuzuiliwa kwa meli hiyo.
Runinga ya taifa Nchini Libya Al-Nabaa pia imeripoti tukio hilo kwa undani.
Walid al-Tarhuni, ambaye ni msemaji wa
zamani wa kundi la waasi ambalo limekuwa likidhibiti bandari hiyo,
ameiambia runinga ya Al-Nabaa kuwa meli hiyo ya mizigo ilikuwa ikielekea
katika bandari ya Zawiyah, kilomita 50, Magharibi mwa mji mkuu Tripoli,
kupakua mafuta hayo.
Utawala wa Washington umesema kuwa
umeshangazwa na tukio hilo na kukariri kuwa mafuta inayotoka Libya ni
mali ya raia wa nchi hiyo na wala sio ya makundi fulani.(P.T)
No comments:
Post a Comment