TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Wednesday, March 12, 2014

KANUNI BUNGE MAALUM ZAPITA

 BungeMaalumKatiba_d9be9.jpg

HATIMAYE Bunge Maalumu la Katiba, limepitisha rasimu ya Kanuni zitakazotumika kuongoza majadiliano, pamoja na vifungu ambavyo havikutaja aina ya upigaji kura kama utakuwa wa wazi au wa siri. Hata hivyo, wakati Bunge likipitisha azimio hilo, baadhi ya wajumbe wamelaani kitendo cha Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho, kuridhia kupitishwa kwa ‘kanuni nusu’ za Bunge kwa maelezo kuwa jambo hilo halitaleta muafaka.
Wajumbe hao pia wameonya kuwa Bunge Maalumu la Katiba, linaweza kushindwa kupata muafaka wa njia ya kufanya uamuzi iwapo wajumbe ndani ya Bunge hilo watang’ang’ania ushabiki na itikadi za vyama vyao.
Azimio la Kutunga na Kupitishwa kwa Kanuni hizo liliwasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Profesa Costa Mahalu ambaye alitaka kanuni zipitishwe pamoja na aina ya upigaji kura kwa ajili ya kupata uamuzi wa Bunge Maalumu unaendelea kushughulikiwa.
“Suala la upigaji kura, litawekwa katika kanuni husika baada ya kuamuliwa kama ambavyo Bunge hili maalum litaona inafaa,” alisema Profesa Mahalu akizungumzia vifungu vya 37 na 38 vinavyoelezea namna ya upigaji kura ambapo kanuni hizo zimeelezea uamuzi utakaopitishwa kwa upigaji wa kura.
Wakichangia wakati wa kupitishwa kwa kanuni hizo, Profesa Ibrahim Lipumba alisema: “Kanuni nzuri zinakidhi mahitaji ya kuendesha vizuri Bunge la Katiba. Kanuni zimetuhakikishia haki na kinga za kila mjumbe na kutakuwa na uhuru bila kushurutishwa au kupokea maelekezo kutoka kwa yeyote au chombo chochote, naomba tuzipitishe.”
Naye James Mbatia aliomba vifungu vya 37 na 38 ambavyo havijakamilishwa vichukue muda mfupi vikamilishwe. Kwa upande wa Idrisa Kitwana Mustafa alisema:
“Mshikamano wetu ndiyo utakaowapa moyo wananchi walio nje ya Bunge hili. Tukubali kuwa hakuna kazi ya mwanadamu itakayoridhisha kila mtu na tuchukulie upungufu uliojitokeza kama ni mambo madogo kwani tuna kazi kubwa mbele yetu”. Panya Ali Abdallah alisema anaamini tunu ya hekima na busara itatumika katika kupata Katiba. Shehe Mussa Kundecha alisema:
“Hakuna kazi ya mwanadamu ikakosa kasoro…ni busara kuona watu wakikubaliana kwa yale waliyotofautiana , tuliombee Bunge hili”.
Kwa upande wa Freeman Mbowe wakati anaunga mkono azimio hilo, aliwataka wajumbe washirikiane, kuheshimiana na kuvumiliana.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alilaani hatua ya Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu, Pandu Ameir Kificho, kukubali kanuni kupitishwa ‘nusu’ kwa sababu ya kuzidiwa nguvu na vyama vya siasa ambavyo vimesimamia itikadi zao na vinatoa vitisho kwa wabunge wake wakubaliane na misimamo ya vyama.
“Hii Katiba tunayoenda kuitunga hapa ni Katiba ya vyama vya siasa na sio Katiba ya wananchi, maana vyama vya siasa vyote vina misimamo kwenye kuandika Katiba hiyo na ndicho kinafanya tushindwe hadi kuafikiana ndani ya Bunge hili,” alisema.
Mbunge huyo ambaye jana alisimama ukumbini kutaka kuzungumza lakini hakupewa nafasi, alidai iwapo jambo hilo litakwama hapo baadaye, Kificho ndiye wa kulaumiwa maana wiki ijayo ni wiki ya kufanya uamuzi lakini Kanuni zimekaa kimya.
Alisema kwa mara ya kwanza Tanzania itapata Katiba ya vitisho kutokana na vyama vikubwa vya CCM, Chadema na CUF kuwalazimisha wabunge wake kuwa na msimamo katika suala ambalo linahusu masuala ya wananchi na sio ya vyama hivyo.
“Watanzania wapo wengi hawana vyama, lakini hivi vyama vya siasa vimeng’ang’ana kuwatisha wajumbe wake wasiende kinyume na misimamo ya vyama hivyo, hii sio haki hata kidogo, tunachoandika hapa ni Katiba ya wananchi sio ya vyama,” alisema mbunge huyo.
Alionya kuwa wabunge wengi kwenye vyama vya siasa ni waoga hasa wa viti maalumu, maana wanaamini kuwa wakienda nje ya misimamo ya vyama vyao, watafukuzwa na hawatapata ubunge tofauti na wabunge wa majimbo.
Mbunge wa Muhambwe Felix Mkosamali, alisema hata wajumbe ambao wamepitisha Kanuni hizo watajilaumu kwa vile vikao vya Bunge haviwezi kuanza bila kuafikiana namna ya kufanya uamuzi.
Mkosamali ambaye awali alimlalamikia Kificho kwa kutompa nafasi ya kuzungumza, licha ya kusimama mara nyingi, badala yake Mwenyekiti huyo wa muda alikuwa anaruhusu wajumbe aliowataka.
“Toka nimefika hapa sijapewa nafasi ya kuzungumza, nimesimama mara kwa mara; lakini Mwenyekiti haniruhusu kwa vile tu anafahamu msimamo wangu ni kupinga kanuni hizi kupitishwa nusu,” alisema Mkosamali.
Alipoulizwa iweje apinge suala hilo wakati Mwenyekiti wake wa NCCR-Mageuzi Taifa, James Mbatia alisimama kuunga mkono na kuwasihi wajumbe wote kuunga mkono suala hilo, alisema Mbatia ana uamuzi wake katika Bunge la Katiba.
“Kwa maoni yangu, Mbatia amekosea kuunga mkono suala hilo, huo ni mtazamo wangu maana hapa hakuna mbunge wa chama bali sote sisi ni wajumbe, hakuna mnadhimu wa chama hapa,” alisema Mkosamali.
Alisema katika Bunge Maalumu la Katiba, mambo yote yanahitaji maridhiano hivyo haipendezi Mwenyekiti kupendelea baadhi ya watu. Alisema anamsubiri Mwenyekiti atakayechaguliwa ili awasilishe maoni yake.
Mchungaji Christopher Mtikila kwa upande wake alisema alipinga kupitishwa kwa azimio hilo la kuazimia Kanuni za Bunge Maalumu kwa vile limepitishwa kwa hila na akashangaa wajumbe wengine kutoka kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kuunga mkono kanuni hizo.
Mtikila alisema suala la kanuni hizo kutokuwa na namna ya kupiga kura, linaonesha dhahiri kuwa wajumbe hawana nia ya dhati ya kutunga Katiba mpya kwa vile suala hilo litarudishwa kwa wajumbe hao lipate uamuzi.
Alisema kuliahirisha ni kutoa fursa kwa baadhi ya watu kuwarubuni baadhi ya wajumbe ili waweze kubadilisha misimamo yao na wanapoenda kupiga kuwa wapigie kundi ambalo linang’ang’ania kura ya wazi.
“Ndio maana wameliweka kiporo suala hili wanataka tukirudi hapa tuwe tumepowa na watunywe vizuri kama uji wa ulevi,” alisema Mtikila.
Mbatia kwa upande wake alisema wiki tatu zilikuwa ngumu kwa wajumbe, lakini akasema kwenye Katiba ili jambo lipite ni lazima lipate maridhiano hivyo kitendo cha kupitisha kanuni hizo kunatoa fursa ya mambo mengine kuendelea na baadaye warudi kufanya uamuzi.
“Dola linaundwa kwa njia ya maridhiano na ndio hatua tuliyofikia sasa, wahenga wanatuasa pambana wakati mnazungumza, kisheria kanuni hizi ziko sahihi,” alisema Mbatia.
CHANZO:HABARILEO

No comments:

Post a Comment