YANGA YAWALIPA NSAJIGWA NA MWASIKA
Baada ya vuta ni kuvute huku
ikitishiwa kulimwa adhabu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), klabu
Yanga imekubali matokeo na kumalizana na wachezaji wake wa zamani,
Stephano Mwasika na Shadrack Nsajigwa 'Fusso' waliokuwa wakiidai klabu
hiyo zaidi ya Sh15 Milioni. (HM)
Wachezaji hao walikuwa wanaidai Yanga fedha hizo kutokana na malimbikizo ya ada ya usajili, ambapo uongozi wa klabu hiyo ulikuwa ukiwapiga danadana kuwalipa wakati walipokuwa waikiitumikia.
Kutokana na hali hiyo wachezaji hao baada ya kuachwa na klabu hiyo katika usajili wake wa msimu huu waliamua kuishtaki Yanga ili iweze kuishinikiza na kuwalipa haki zao.
Nsajigwa, alikuwa akiidai Yanga kiasi cha Sh 9 milioni wakati Mwasika ambaye sasa anaitumika Ruvu Shooting alikuwa akiidai Yanga Sh 6.5 milioni.
Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako ameliambia gazeti hili jana kuwa wamemalizana na wachezaji hao siku tatu zilizopita.
Alisema Yanga haikuwa na nia ya kuwadhulumu wachezaji hao isipokuwa malipo yao yalichelewa kutokana na kuwepo kwa sababu mbalimbali za kiutawala.
"Tumemalizana nao, lakini ni vema ukawauliza na wenyewe kwa uhakika zaidi," alisema Mwalusako.
Hata hivyo Nsajigwa alipouliwa alikubali kuwa tayari wamemalizana na klabu hiyo tangu siku ya Jumatatu na sasa hana kitu chochote anachoidai klabu hiyo. Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment