DK.MAGUFULI ABAINI UBADHILIFU MIZANI IRINGA
WAZIRI wa Ujenzi, Dk. John Magufuli,
amebaini kuwapo na ubadhirifu mkubwa wa fedha kwenye vituo vya mizani
vilivyopo maeneo mbalimbali nchini. (HM)
Dk. Magufuli, aligundua ubadhirifu mkoani Iringa, baada ya kupewa taarifa za fedha zinazotokana na tozo ya magari yanayokamatwa kwenye mizani kwa makosa mbalimbali, yakiwamo ya kuzidisha uzito.
Msemaji wa Wizara ya Ujenzi, Martin Ntemo, alisema imebainika baadhi ya mameneja wa Mamlaka ya Barabara Tanzania (TANROADS) wanajihusisha na ubadhirifu wa fedha.
Alisema, Dk. Magufuli ametupilia mbali taarifa aliyosomewa na Meneja wa Tanrods Mkoa wa Iringa, Mhandisi Poul Lyakurwa, kwa kuwa umejaa udanganyifu na haina uwiano kati ya gari zilizokamatwa na fedha zilizotozwa.
Alisema meneja huyo, aliwasilisha taarifa kwa Dk. Magufuli inayoonesha amekusanya Sh milioni 31.9 kwa mwezi, huku magari yaliyokamatwa yakiwa ni 20,700.
Alisema kati ya magari hayo 20,700, yaliyokamatwa kwenye mizani kwa makosa mbalimbali, ni magari 735 tu yaliyotozwa faini, sawa na asilimia 3.5, kiasi ambacho ni kidogo.
"Waziri alishtushwa na takwimu hiyo na kukataa isiendelee kusoma kwa sababu ukiangalia wastani wa magari yanayokamatwa nchi nzima ni zaidi ya asilimia 40, sasa iweje barabara kuu ikamate magari 20,700 kwa mwezi kisha itoze asilimia 3.5.
"Kutokana na hali hiyo, aliagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa nchini (TAKUKURU), Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya uchunguzi katika vituo vyote vya Mkoa wa Iringa.
"Waziri amekasirishwa na hali hiyo na kusema hawezi kuruhusu hali hiyo kuendelea ndani ya wizara yake, taarifa aliyosomewa ilikuwa ya Julai, mwaka huu, katika kituo cha mizani cha Wenda, kilichopo kati ya Iringa na Ifunda, katika barabara kuu ya TANZAM. Chanzo: Mtanzania
No comments:
Post a Comment