UKOSEFU WA ELIMU WASABABISHA UJINGA, MARADHI NA UMASKINI
Watoto wengi katika nchi zinazoendelea
wanakabiliwa na tatizo la ujinga, maradhi na umaskini hivyo basi
kupatikana kwa elimu bora kutawasaidia kujikwamua na matatizo hayo pindi
watakapomaliza masomo yao na kupata ajira na hivyo kujikwamua na hali
ngumu ya maisha. (HM)
Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na walimu walioshiriki katika warsha ya elimu iliyoandaliwa na Taasisi ya Malaika na kufanyika katika chuo kikuu cha Nebraska kilichopo mjini Lincoln .
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema jamii nyingi inajitahidi kupambana na matatizo yanayozakabili watoto wao lakini kama kutakuwa na ushirikiano wa pamoja itasaidia matatizo hayo kutatulika kirahisi.
"Warsha hii inaonyesha kuwa Dunia ni moja, ni kama kijiji bila ya kuangalia mipaka iliyopo , kutokana na hili tunatakiwa kutumia utaalamu wetu katika kushirikiana kwa pamoja ili kutatua matatizo yanayotukabili na kutumia pamoja rasilimali zilizopo", alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Mwanzilishi na Rais wa Taasisi ya Malaika Dk. Natalie Hahn alimshukuru Mama Kikwete kwa kukubali kushiriki katika warsha hiyo kwa kuwa ni wanawake wachache kama yeye wanaoweza kuwa karibu na jamii inayowazunguka.
Alisema kuwa elimu ni nyenzo muhimu katika maisha mtu akiwa na elimu anaweza kwenda popote pale apatakapo kutokana na hilo ndiyo maana anachangisha vitabu kwa ajili ya wanafunzi katika mabara yote ili nao waweze kupata elimu kama aliyoipata yeye.
"Walimu mnatakiwa kuwa wa kimataifa ili muweze kufundisha na wengine wajivune na kutaka kuwa kama nyinyi, mtafute wafadhili wa masomo yenu ili muweze kusoma zaidi pia muwasaidie watoto ambao wanahitaji kusaidiwa kwani kama mtoto akikosa ada au nguo za shule Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikia watoto (UNICEF) linawasaidia watoto wa aina hii", alisema Dk. Natalie.
Aliwataka walimu walioshiriki katika kongamano hilo wajitahidi kuwa na shule dada nchini Tanzania na kujenga mahusiano nao ili waende kufundisha kule watajifunza mambo ambayo ni tofauti, watumie rasilimali walizonazo kuwasaidia wanafunzi ili nao wawakufundishe wengine.
Katika warsha hiyo Mama Kikwete alikabidhiwa hati ya ukazi wa jimbo la Nebrasca na Dk. Marjorie Kastelnin ambaye ni mlezi wa wanafunzi katika kitivo cha Elimu na Sayansi ya Jamii.
Mama Kikwete pia alikutana na Mke wa Gavana wa jimbo hilo Mama Sally Ganem ambaye alimpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya nchini Tanzania ya kuwasaidia kina mama na watoto wa kike kupata elimu.
"Kazi unayoifanya ni kubwa kwani inagusa maisha ya watu, elimu ni kitu cha muhimu sana katika maisha ya binadamu mtu bila ya kuwa na elimu hawezi kufanya kitu chochote wewe unawasaidia watoto wa kike kupata elimu na kuwaandalia maisha yao ya baadaye, nakupongeza sana kwa hilo", alisema Mama Ganem.
Alisema kuwa fani yake yeye ni mwalimu kutokana na majukumu aliyonayo hafundishi kwa sasa, lakini kwa kuwa anawapenda watoto ameanzisha program ya kutoa chakula cha asubuhi kwa wanafunzi wa shule za msingi jambo ambalo mme wake Gavana Dave Heineman amemuunga mkono kwa kutoa chakula cha mchana kwa watoto hao. Chanzo: Anna Nkinda
No comments:
Post a Comment